KWA kipindi kirefu sasa kiungo nyota wa Yanga, Athuman Idd maarufu ‘Chuji’ amekuwa katika matatizo yatokanayo na utovu wa nidhamu.
Hali imekuwa hivyo katika klabu yake pamoja na timu ya Taifa. Suala la nidhamu limekuwa likimuweka pabaya.
Katika miaka ile akiwa na tatizo Taifa Stars chini ya kocha Marcio Maximo wengi waliona kwamba uchanga wake nao ulichangia kuwapo matatizo hayo hivyo wakati wote kilichozungumzwa na kwamba anahitaji nafasi.
Wako ambao walimlaumu Maximo na kuona kwamba hakuwa sahihi kwa jinsi alivyoyasimamia matatizo ya Chuji.
Pamoja na yote ambayo Chuji amekuwa akikutana nayo bado nafasi yake katika klabu na hata Taifa Stars ni kubwa, makocha wanamhitaji, wachezaji wenzake wanamhitaji na mashabiki wanamkubali.
Yote hiyo ni kutokana na kipaji chake na uwezo wake wa kufanya kazi uwanjani kwa ufanisi jambo ambalo baadhi ya wachezaji limekuwa likiwashinda.
Hata hivyo tunadhani kwamba huu ni wakati sahihi kwa Chuji kufahamu kwamba imetosha na badala yake mashabiki watapenda kumuona akifanya mambo uwanjani tu na si vinginevyo.
Mashabiki hawatopenda kusikia habari za Chuji kusimamishwa kwa mambo ambayo kwa uzoefu alionayo haipendezi kuyafanya.
Matatizo yote yahusuyo nidhamu na mengineyo yamewachosha mashabiki na kwa muda ambao amekuwa katika soka ni wazi kwamba anatakiwa kubadilika, anatakiwa kuwa msaada kwa wachezaji chipukizi.
Tumekuwa tukishuhudia mara kadhaa wachezaji kukerwa mara wanapotolewa na makocha wao kabla ya dakika 90 za mchezo kumalizika.
Hili ni jambo la kawaida, si kwa wachezaji wa Bongo tu bali hata wale wanaocheza soka Ulaya kama kuna jambo hawalipendi basi ni kutolewa kabla ya muda.
Hata hivyo pamoja na kutolipenda jambo hilo lakini wachezaji hao wanafahamu ukweli kwamba wanatakiwa kwenda kwenye benchi kuungana na wenzao na si kwenda sehemu nyingine.
Mchezaji ambaye anatolewa kabla ya wakati na hapaswi kwenda kwenye benchi ni yule ambaye anapewa kadi nyekundu.
Hili tunaamini Chuji alilifahamu na hivyo tulishangaa kulikoni alipotolewa katika mechi ya Mtani Jembe kati ya Yanga na Simba akaacha kwenda kwenye benchi la Yanga kama utaratibu unavyotaka.
Ni vyema Chuji akatambua kwamba kinachomlinda sasa katika Yanga na hata Tafa Stars ni kipaji chake, kipaji ndicho kinachowafanya makocha wamhitaji na mashabiki wamhitaji na kumuunga mkono.
Hatuoni ni kwa nini anawaangusha makocha na mashabiki hawa kwa mambo ambayo yeye mwenyewe anayafahamu, Chuji anafahamu utaratibu wa mchezaji pindi anapotolewa na kocha wake.
Kutolewa na kocha na kutokwenda katika benchi si jambo zuri hata kidogo, ni kumdharau kocha na wachezaji wenzako ambao kwa kawaida wanapotolewa pamoja na hasira lakini wanajumuika na wenzao katika benchi.
Tunafahamu kwamba Chuji ni mzoefu na anazijua taratibu hizi na ndio maana tunashangaa ni kwa nini aliamua kuzipuuza kwa makusudi.
Kwa mantiki hiyo tunapenda kumkumbusha Chuji kwamba huu ni wakati wake wa kuwa mfano wa kuigwa katika klabu ya Yanga na hata Taifa Stars.
Bado anayo nafasi na ni vyema akaitumia nafasi hiyo kwa mambo yatakayomfanya akumbukwe vizuri.
kwenye mpira nidhamu inatangulia kipaji...huku kwetu tunajifanya tunajali vipaji zaidi kuliko nidhamu ndio maana wachezaji wetu hawachezi mpira kwa muda mrefu...they should learn from european players...nidhamu ya chuji ni ndogo sana, hastahili hata kupata namba...
ReplyDeleteMbona Baloteli nidhamu Zero
ReplyDeleteChuji anafanya yte hayo kwa sababu y bangi zake 2!hyo mambo hawezi kuyaacha mpk siku akiacha bangi
ReplyDelete