MZIMU WA POSHO WALITESA BUNGE LA KATIBU..WAKATAA POSHO YA SH LAKI TATU KWA SIKU

Siku mbili baada ya kuanza kwa Bunge hilo, baadhi ya wajumbe wametaka waongewe posho kwa maelezo kuwa kiasi wanachopewa sasa cha Sh300,000 kwa siku hakiwatoshi kutokana na kupanda kwa gharama za maisha Dodoma.

Wajumbe hao walitoa kauli hiyo jana katika kikao cha kuwasilisha na kujadili rasimu ya kanuni za Bunge hilo ambacho kilianza saa nne asubuhi.Kwa kiasi kikubwa, kikao hicho ambacho awali waandishi wa habari walizuiwa kuingia, kilitawaliwa na hoja ya kuongezwa kwa posho za wajumbe na kuungwa mkono na wajumbe wengi bila kufuata utaratibu maalumu uliokuwa ukisisitizwa na Mwenyekiti wa Muda wa Bunge la Katiba, Pandu Ameir Kificho.

“Wajumbe wengi walikuwa wakisimama na kutaka kuzungumza bila kufuata utaratibu maalumu. Jambo hilo liligeuza ukumbi wa Bunge kuwa kama soko,” kilisema chanzo chetu. Baadhi ya wajumbe waliopata nafasi ya kuzungumzia nyongeza ya posho hizo ni Mbunge wa Kishapu (CCM), Suleiman Nchambi na Mbunge wa Sumve (CCM), Richard Ndassa.

Katika ufafanuzi wake kwa waandishi wa habari, baada ya kikao hicho kuahirishwa kwa muda, Ndassa alisema: “Bunge ndiyo linalotengeneza Katiba ya nchi. Nasikitika kuwa kiwango cha fedha ambacho tunalipwa ni kidogo na hakitoshi kwa sababu kuishi katika Mji wa Dodoma ni gharama kubwa.”

Ndassa alisema kati ya Sh300,000 wanazolipwa wajumbe hao, posho ya kikao ni Sh220, 000 na 80,000 ya kujikimu na kwamba kiasi hicho hakitoshi.

“Mfano ni siku ya Jumamosi na Jumapili. Katika siku hizo mbili wajumbe wote hawalipwi Sh220,000 za posho za kikao na wakati huohuo wanatakiwa kuwalipa madereva wao, kununua mafuta ya gari, chakula na malazi,” alisema.

Aidha, alisema kitendo cha wajumbe kutakiwa kulipwa Sh220, 000 baada ya kusaini katika kitabu cha mahudhurio mara mbili kwa siku ni sawa na udhalilishaji.

“Nilimweleza mheshimiwa mwenyekiti kwamba wajumbe tupo 600 na kulingana na hali halisi wote hatuwezi kuhudhuria kikao kila siku, zipo siku ambazo baadhi yetu wanakuwa na shughuli nyingine na wapo watakaougua, sasa na hao wasilipwe Sh220,000 kweli?” alihoji.

Alisema Serikali inatakiwa kulitazama suala hilo kwa kina kwa maelezo kuwa linaweza kuibua mvutano unaoweza kusababisha wajumbe hao kushindwa kuijadili Rasimu ya Katiba kama inavyotarajiwa na wengi.

“Wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba walikuwa wakilipwa Sh500,00 kwa siku, lakini wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba wanalipwa Sh220,000 tena mpaka wahudhurie kikao. Hii siyo sawa kabisa,” alisema.

Alisema madereva wa Tume hiyo ya Katiba walikuwa wakilipwa Sh220,000 kwa siku... “Posho yangu ni sawa na aliyokuwa akilipwa dereva wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba. Sielewi kabisa maana hata viwango vyetu vya posho ni tofauti na wajumbe wa Bunge la Katiba kutoka Zanzibar, wao wameongezewa posho.”

Alisema jambo hilo litaibua ubaguzi kwa sababu wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wanaweza kuwasilisha malalamiko yao kwa Spika wa Bunge, Anne Makinda na kuongezewa posho lakini wajumbe 201 walioteuliwa na Rais hawana mahali pa kulalamika ili kuongezewa posho.

Pamoja na Ndassa kutotaka kuweka wazi, kumekuwa na madai kuwa wajumbe kutoka Zanzibar wameongezewa Sh120,000 na Baraza la Wawakilishi, hivyo kuwafanya kupata Sh420,000 kwa siku.

Hata hivyo, Katibu wa Baraza hilo, Yahya Khamis Hamad alikana madai hayo akisema hakuna fedha za ziada walizolipwa.

Alisema malipo waliyosaini wakiwa Dodoma yaliyotokana na kuhudhuria vikao vya Kamati za Baraza, lakini si nyongeza ya posho.

Akizungumzia suala hilo Nchambi alisema: “Sisi tumeshazoea maisha ya Dodoma na tunaishi hivyohivyo tu licha ya kuwa fedha ni ndogo. Ila hawa wenzetu ambao ni wageni hali zao ni mbaya.

“Wajumbe wapo hapa kwa ajili ya kutengeneza moyo wa nchi yao na wakati tunakuja hapa Dodoma tulielezwa wazi kuwa tusiende kuishi katika nyumba za wageni za vichochoroni. Sasa kwa mantiki hiyo hiki kiwango cha fedha tunacholipwa kitatosha kweli?

“Hapa bungeni wapo maprofesa walioacha kazi zao zinazowaingizia fedha nyingi na kuja kuandika Katiba. Kitendo cha kuwalipa fedha kidogo kinaweza kuwakatisha tamaa.”

Kificho alihitimisha mjadala huo kwa kusema suala hilo la posho litawasilishwa serikalini kuona namna ya kulifanyia kazi.

Baada ya wabunge kutoka kwenye mjadala huo, Mjumbe, Kabwe Zitto alisema anasikitika kwamba tangu siku ya kwanza, suala la posho linashika kasi... “Kiukweli inavunja moyo sana… Ni dhahiri wajumbe lazima walipwe lakini malipo ya posho ndiyo kipaumbele kweli?”

Imeandikwa na Mwinyi Sadallah, Raymond Kaminyoge Fidelis Butahe na Freddy Azzah.
Tags

Post a Comment

11 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
  1. eeeh mungu,laki tatu mshahara wa mtu mwez mzima wao wanakataa kwa siku??

    ReplyDelete
  2. umeona eeeeeeeee yani pesa mbele kushinda kitu chochote pesa shetani jamani mwe badala ya kujadili rasim wanajadili posho haki ya mungu hii dunia shetani kashika kasi mpaka parapanda ilie tumeumia

    ReplyDelete
  3. njaa,elimu,utaifa kipi ni kipi.....

    ReplyDelete
  4. mna hazi ipi nyie wabunge acheni kufulu.laki tatu ni mshahara wa mwalimu ambaye baadhi yenu amewazid elimu

    ReplyDelete
  5. Kweli waTZ uzalendo hatuna Huko nyuma mbunge liliwahi kuanza hivyo kwa kundai Posho mbele. Hawa nao wameanza posho ndogo Swali Je walifanya kampeni ya kuhonga na sasa wataka kurudisha waliko kopa au? Amini usia mini suku zitaongezeka sana tena sana za ku kukaa huko Dodoma ili kitita kitune

    ReplyDelete
  6. Wajumbe wapo 500 na wanadai malipo makubwa zidisha gharama itakuwa ngapi wakati wananchi wengne wanakosa huduma za afya elimu n.k kweli tutafika nchi hii kwa kuweka Pesa mbele

    ReplyDelete
  7. Mnatuvunja moyo watanzania kweli mtaweza kutuwakilisha?

    ReplyDelete
  8. Tanzania, nakulilia Tanzania. Wakati kila siku wanasimama majukwaani kutushawishi tuwachague waboreshe huduma za jamii, mioyoni mwao wanawaza mengine. Wakiongea na waandishi wa havari wako mbele kujipambanua na kutunisha vifua, moyoni mwao wanaugulia kwa kukosa posho. Wanakua imara sana kuiponda serikali kwa kushindwa kuboresha maisha ya watanzania, lakini ukweli wanaipenda hali hiyo, ndio maana kila siku hawaachi kulilia posho zaidi. Kuna wengine wanaenda kulala tu bungeni, wengine wameenda kujifunza na wengine wameenda kupumzika...lakini wnadai posho hazitoshi.
    Inauma sana kusikia hospitali zetu hazina gari za kubebea wagonjwa wala vitanda vya kutosha mawodini lakini leo mtu anasema laki 3 haitoshi. Hiyo laki 3 inanunua vitanda vingapi kwa ajili ya hospitali? Acheni ubinafsi. Acheni tamaa.

    ReplyDelete
  9. Mheshimiwa JK, tafadhali vunja hilo bunge la katiba haraka, watu waombe upya huku zikiainishwa posho watakazolipwa ili anayetaka aombe akijua atalipwa nini, atakayeona ndogo asiombe kabisa. Kwakweli hao wajumbe wanatia aibu.

    ReplyDelete
  10. yarudi tu nyumbani, nyambaf!!! hayana hata aibu!! haya majitu hayafai kwenye jamii, hayana huruma na binadamu wengine!!

    ReplyDelete
  11. navyojua mimi hili bunge halita hata tusaidia, halitakuwa la maana hata kidogo sababu limejaa walafi tu, dah TZ imekwisha.

    ReplyDelete

Top Post Ad

Below Post Ad