RAIS KIKWETE:WANASIASA ACHENI KUINGILIA NA KUROPOKA KWENYE MASWALA YA KITAALAMU

Rais Jakaya Kikwete amewataka wanasiasa kuacha kutoa majibu ya kisiasa katika masuala na changamoto za kitaalam na kiufundi.

Amesema matatizo na changamoto za kitaalam na kiufundi ziachiwe kutafutiwa majawabu ya kiufundi badala ya kupatiwa majawabu ya kisiasa.

Rais Kikwete alitoa rai hiyo mwishoni mwa wiki, wakati akizungumza na wajumbe wa Halmashauri ya CCM ya Mkoa wa Mbeya.

Alisema hayo kufuatia kauli ya Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Mbeya ambaye pia ni Naibu Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Godfrey Zambi kulalamikia ubora wa mbolea ya Minjingu.

Zambi aliuambia mkutano huo kuwa wakulima wa mkoa wa Mbeya wanakataa kutumia mbolea ya Minjingu kwa madai kuwa haifai kwa matumizi katika mkoa huo pamoja na kwamba ilifanyiwa utafiti wa kitaalam na kupitishwa na wataalam wa Kituo cha Utafiti cha Kilimo cha Uyole kilichoko Mbeya.

Baada ya kusikiliza kauli hiyo ya Zambi, Rais Kikwete alisema kama kuna tatizo la mbolea ya Minjingu litakuwa linatokana na hali ya udongo katika sehemu mbali mbali za mkoa huo lakini siyo kutokana na ushauri wa kitafiti wa Kituo cha Uyole.

“Kituo cha Uyole kilifanya utafiti na kuona kuwa mbole ya Minjigu inafaa kwa matumizi ya mkoa wa Mbeya. Nyie mnasema kuwa haifai.

Ushauri wangu ni kwamba kama mnaona kuna tatizo, nawashaurini rudini tena kwa wataalam wa Uyole waangalie tena ili wataalam hao warudi kwenye drawing board,” alisema Rais Kikwete na kuongeza:

“Utatifi wa udongo ni muhimu sana katika kuamua mbole ya aina gani inafaa katika eneo gani. Hivyo, nashauri kuwa warudieni wataalam wa Uyole waangalie kuna tatizo gani?.

Naamini kuwa utafiti wa Uyole hauwezi kuwa wa makosa. La msingi ni aina na ubora wa ardhi ambayo mbole hiyo inatumika.”

CHANZO: NIPASHE - 4th February 2014

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad