UJANGILI NCHINI UMETUVUA NGUO MBELE YA DUNIA

Ni jambo la kusikitisha kuona kwamba jina la Tanzania kwa muda mrefu sasa limetawala vichwa vya habari katika vyombo vingi vya habari duniani kutokana na Serikali kushindwa kukomesha vitendo vya ujangili dhidi ya wanyamapori walio katika hatari ya kutoweka, wakiwamo tembo.

Tanzania sasa inaonekana mbele ya jumuiya ya kimataifa kama taifa la watu wa ovyo, ambalo halitambui kwamba kuangamiza wanyamapori litakuwa maskini milele.

Pamoja na kushutumiwa na kusutwa kila kona ya dunia kutokana na kushamiri kwa vitendo vya ujangili ambavyo vinasababisha mauaji ya tembo 11,000 kila mwaka, Serikali imebaki kulalama dhidi ya vyombo vya habari vya kimataifa vinavyoinyooshea kidole, ikikanusha shutuma hizo na kutishia kuvichukulia hatua za kisheria.

Wiki iliyopita, kwa mfano magazeti ya Daily Mail na Mail on Sunday ya Uingereza yalichapisha habari za kuishutumu Serikali na kudai kuwa, pamoja na kuwafahamu fika majangili wanaoteketeza wanyamapori nchini imeshindwa kabisa kuwachukulia hatua.

Katika kile kinachoonekana kwa wachambuzi wa masuala ya maliasili kama kujaribu kupoza joto la shutuma hizo, Rais Jakaya Kikwete ambaye aliongoza ujumbe wa Tanzania kwenye kongamano hilo, juzi alifanya mahojiano jijini London na vyombo vikubwa vya utangazaji duniani, vikiwamo CNN na BBC kuhusu tatizo la ujangili nchini na juhudi za Serikali yake za kupambana na vitendo hivyo.

Wakati Rais akichukua hatua hiyo, Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu alikuwa tayari amefanya mazungumzo na wahariri wa magazeti ya Daily Mail na Mail on Sunday jijini London kutokana na magazeti hayo kuchapisha habari zilizoishutumu Serikali ya Tanzania kwa kutokomesha vitendo vya ujangili.

Hali hiyo ya nchi yetu kushutumiwa na kuaibishwa kwa kiwango hicho kikubwa ilichochewa na kongamano lililoitishwa na Serikali ya Uingereza na kumalizika mwishoni mwa wiki mjini London, ambapo wajumbe kutoka nchi 46 na mashirika 11 ya kimataifa yalihudhuria, wakiwamo marais wanne wa Afrika.

Katika kongamano hilo ambalo pia lilihudhuriwa na Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron na mtoto wa Malkia Elizabeth, Prince Charles wakuu wa nchi na wahifadhi kutoka kote duniani walibuni mikakati ya kukomesha uwindaji haramu wa wanyamapori walio katika hatari ya kuangamia.

Tanzania ndiyo iliyoonekana kuwa katikati ya masikitiko na shauku za wajumbe wa kongamano hilo kutokana na ukubwa wa tatizo la ujangili hapa nchini ambao mpaka sasa umeangamiza idadi kubwa ya faru na tembo.

Kwa sababu za kidiplomasia na kiitifaki, ujumbe wa Tanzania haukuwekwa kitimoto kwa maana ya kushinikizwa kuonyesha dhamira au kutangaza mikakati na sera mbadala za kupambana na ujangili.

Hata hivyo, Waziri Nyalandu alitangaza katika kongamano hilo kwamba Tanzania sasa imefuta mpango wake wa kutaka ipewe kibali cha kuuza shehena kubwa ya meno ya tembo yaliyohifadhiwa katika maghala hapa nchini.

Kongamano hilo ambalo ndilo lilikuwa habari kubwa ya dunia wiki hii sasa limemalizika. Bila shaka Rais Kikwete na ujumbe wake wamerudi nyumbani wakiwa wamepata somo la kutosha kuhusu umuhimu wa kupambana na ujangili pasipo kuyumba.

Kwa kuwa ameiambia dunia kwamba majangili nchini Tanzania wanafahamika, tunatarajia watatiwa mbaroni katika awamu ya pili ya ‘Operesheni Tokomeza Ujangili’, ambayo ameiahidi dunia kwamba itaanza muda wowote kuanzia sasa
Tags

Post a Comment

11 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
  1. Tunataka afanye vitendo sio maneno maneno wanyama walioangamia niwengi mno.sikio la kufa............

    ReplyDelete
  2. Majina hawatajwi serikali inaogopa nini? Basi nawao wanahusika wanaogopa wakiwataja yatabumbuluka mengi.

    ReplyDelete
  3. Kwa kweli hili Tatizo ni kubwa nchi mwetu si la kulikebei, yaani imekuwa ni biashara maarufu kwa kuangamiza wanyama wetu wenywe, wala serikali isinyamze au kubisha wakati tunajuana vizuri kwamba hili tatizo ni lipo, watu wengine ndio wamefanya ajila yao hii, kwa kuua wanyama hawa tembo na faru, unakuta kiongozi nae shughuli yake hii, watu wa kawaida nao shughuli yao hii. heee sisi wafrica sijui tuna matatizo gani? hatutumii akili bali tunataka vitu vya raisi raisi bila ya kuvitolea jasho sana, ndio maana tunangamiza mali asili yetu tuliobalikiwa na mwenyezi mungu kwa ajili ya tamaa tu na ainufaishi watu wote bali mtu binafsi, wanyama wakiishi wananufaisha taifa zima, kwanza nao wanaitaji maisha vile vile, ni viumbe, kesi za malbino zimeisha sasa ni wanyama gmmmm mbona shughuli sisi watu weusi, sisi kwa sisi tu twamalizana hmmm ndio itakuwa wanyama. Na kumpata faru kwa Tanzania imekua adimu sasa,

    ReplyDelete
  4. wizara ya mali asili na tanapa, wawajibishwe coz ndo wahucka wakuu wa ulinzi wa tembo hao

    ReplyDelete
  5. Kama twiga na wanyama wengine hai wamewahi kubebwa na ndege ya jeshi la nchi nyingine kwenye ardhi ys Tanzania na hatumsikia rais akisema chochote zaidi ya wapambe wake kupiga porojo tutaamini vipi kama kweli uongozi wa juu wa serikali haukuhusika?
    Mtakanusha sana lakini ukweli mnaujua!

    ReplyDelete
  6. Hizi porojo za kukanusha baada ya watu kuwachana mpeleke kwenu...kila siku mnajidai wahusika mnawajua, je mumewachukulia hatua gani? Madawa ya kulevya pia ni hivyo hivyo...

    ReplyDelete
  7. Hizi porojo za kukanusha baada ya watu kuwachana mpeleke kwenu...kila siku mnajidai wahusika mnawajua, je mumewachukulia hatua gani? Madawa ya kulevya pia ni hivyo hivyo...

    ReplyDelete
  8. huyo rais kikwete ameshazoea kukaa na kuwasamehe huenda na majangili kawasamehe kama wa change ya rada nk hvo tusitegemee atawafanya lolote

    ReplyDelete
  9. cku watajikuta wamebaki na tembo mmoja ndo watajuta

    ReplyDelete
  10. hiyo ni biashara ya mabosi hadi wa,ikulu

    ReplyDelete
  11. Bora waishe ili wafugaji wawe huru kufugia ng'ombe uko kwenye hifadhi.

    ReplyDelete

Top Post Ad

Below Post Ad