UTATA KESI YA MTANZANIA AFRIKA KUSINI..NI ALIYE TISHIA KUTOA SIRI ZA MKE WA ZUMA

Kesi ya Mtanzania Stephen Ongolo anayeshikiliwa na polisi Afrika Kusini akituhumiwa kutishia kutoa siri za mke wa pili wa Rais wa nchi hiyo, Jacob Zuma, Nompumelelo Ntuli Zuma (MaNtuli), imeibua mabishano ya kisheria ya kuhusu mahali anapotakiwa kushtakiwa.

Gazeti la The Star la Afrika Kusini liliripoti kuwa baada ya Ongolo kupandishwa kizimbani kwenye Mahakama ya Camperdown jijini Durban, Jumatatu wiki hii, ilibainika kuwa Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Ndoda January hakueleza ni wilaya gani ya kimahakama ambayo Ongolo alitenda kosa hilo. January alisema kuwa walishindwa kujua eneo alilofanya makosa Ongolo, kwani alikuwa akitumia ujumbe mfupi wa simu alioutuma kwa vyombo vya habari vya nchi hiyo.

“Tunashindwa kuelewa eneo gani ambalo mshtakiwa amefanya kosa kwa sababu mlalamikaji anaweza kuwa sehemu yeyote kati ya Camperdown na Nkandla ambako alipeleka ujumbe huo,” alisema January.

Kukamatwa kwa Ongolo

Ongolo alikamatwa na polisi jijini Durban mwezi uliopita kwa madai ya kumtishia mke wa pili wa Rais Zuma kuwa angetoa siri zake. Siri hizo zinahusiana na kifo cha mlinzi wa Rais Zuma, Phinda Thomo, ambaye alidaiwa kujiua bafuni kwake mwaka 2009.

Ongolo alikaririwa na Gazeti la Sunday Independent la Afrika Kusini akieleza kuwa Thomo hakujiua bali kifo chake kilipangwa baada ya siri kati yake na MaNtuli kubainika.

Gazeti la The Star la nchini humo, jana liliripoti kuwa hakimu anayesikiliza kesi hiyo, Thys Talijaard wa Camperdown alisema ili Ongolo apate dhamana hapo Camperdown, alitakiwa awe ameshtakiwa kwa makosa aliyofanya kwenye mahakama ya wilaya ambayo kosa limetendeka.

Ongolo alitakiwa kuomba dhamana Jumatatu lakini mwanasheria anayemtetea, Lekoa Le-koko hakuwapo mahakamani, na hivyo mashtaka kupangwa kusikilizwa tena jana.

Wakati mshtakiwa huyo akiwa mahakamani hapo ulizuka mjadala mzito kati ya January na Mdu Thuketana ambaye alishika nafasi ya Le-koko, wakijadiliana ni wapi mshtakiwa anaweza kushikiliwa wakati kesi yake ikiendelea kusikilizwa.

Thuketana aliomba Ongolo awe chini ya ulinzi wa polisi kutokana na afya yake kwani anasumbuliwa na maradhi ya pumu na pia walikuwa wakihofia usalama wake.

Wiki iliyopita, Ongolo alishindwa kwenda mahakamani baada ya kuugua pumu na kupelekwa hospitali.

Hata hivyo, January alisema mshtakiwa anaweza kuwekwa chini ya ulinzi wa polisi kwa siku saba tu, na baada ya hapo atapelekwa kwenye mahabusu za kawaida, jambo ambalo liliafikiwa na Hakimu Talijaard.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad