Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba jana jioni alisimama kwa dakika tatu mbele ya kipaza sauti lakini akashindwa kuwasilisha Rasimu ya Katiba kutokana na vurugu zilizojitokeza bungeni.
Vurugu hizo zilitokea muda mfupi baada ya Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samuel Sitta kumwalika kuwasilisha Rasimu ya Katiba kwa muda wa dakika 120.
Jaji Warioba alisimama kwenye mimbari ya Bunge saa 11:02 jioni tayari kuhutubia lakini kabla ya kufanya hivyo, wajumbe kadhaa walisimama na kuomba mwongozo wa mwenyekiti.
Waliosimama ni Profesa Ibrahimu Lipumba, James Mbatia, Freeman Mbowe na Tundu Lissu.
Hata hivyo, Sitta aliwanyima fursa akisema: “Hakuna mwongozo hapa, naomba Mwenyekiti uendelee, waheshimiwa wabunge hakuna mwongozo naomba Mwenyekiti uendelee kwa ajili ya hansard.”
Kauli hiyo ilionekana kuchafua hali ya hewa kwani Jaji Warioba alipowasha kipaza sauti tayari kuanza kuhutubia, baadhi ya wajumbe walianza kupiga kelele, wengine makofi na kugonga meza hivyo kumfanya ashindwe kufanya kazi hiyo ya uwasilishaji.
Waliokuwa mstari wa mbele kupinga Jaji Warioba kuwasilisha Rasimu ya Katiba kwa sehemu kubwa walikuwa ni wajumbe wanaounda kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Jaji Warioba akiwa anatafakari mbele ya mimbari, Sitta aliwasha kipaza sauti na kumtaka aendelee kuwasilisha Rasimu ya Katiba ... “Endelea Mwenyekiti, endelea kwa ajili ya kumbukumbu rasmi (hansard).”
Lissu akisikika akijibu kauli hiyo akisema: “Fuata kanuni mwenyekiti... fuata kanuni mwenyekiti,… huku akipiga kelele na kugonga meza na wakati huo Profesa Lipumba akiwa amewasha kipaza sauti chake kutaka kuzungumza huku naye akiendelea kupiga meza kwa nguvu.
Wengine waliosimama ni Mchungaji Christopher Mtikila, Ezekiel Oluoch, Philimon Ndesamburo, Moses Machali na Mchungaji Peter Msigwa.
Dakika tatu zilikatika huku kukiwa hakuna dalili za hali kutulia na kuona hivyo, Jaji Warioba aliamua kuondoka kwenye mimbari na kuketi kimya akiwa na Makamu Mwenyekiti wake Jaji Augustino Ramadhani.
Baada ya hapo, Sitta alisimama na kuwasha kipaza sauti na kusema: “Waheshimiwa wajumbe, katika mazingira haya tuliyonayo, naomba kutangaza kuwa nasitisha shughuli za Bunge hadi hapo tutakapotangaziwa tena.”
Licha ya kauli hiyo, baadhi ya wajumbe waliendelea kupaza sauti zao wakisema kwamba walikuwa wanaburuzwa.
Wakati hayo yakitokea, kikosi cha askari wa Bunge kiliingia ndani ya ukumbi na kusimama katika lango kuu hali iliyoonekana kuwa ni kuchukua hadhari endapo hali ya usalama ingechafuka.
Baada ya tamko la kuahirisha mkutano, askari hao waliingia moja kwa moja hadi alipokuwa ameketi Jaji Warioba na kumsindikiza hadi nje na jitihada za waandishi wa habari kumfuata ili kupata maoni yake hazikufanikiwa.
Kilichofuata baada ya hali hiyo ni kurushiana maneno kwa baadhi ya wajumbe akiwamo Dk Ave Maria Semakafu ambaye nusura azipige kavukavu na mjumbe mwingine ambaye jina halikuweza kupatikana mara moja.
Hata hivyo, baadhi ya wajumbe akiwamo Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais (Utumishi), Celina Kombani waliamulia ugomvi huo kabla ya kuwa mkubwa.
Wajumbe walionekana kukaa katika vikundi ndani ya Bunge huku wakijadiliana juu ya kilichotokea wakati Sitta, Katibu wa Bunge, Yahaya Khamis Hamad na msaidizi wake, Dk Thomas Kashililah wakiwa katika kikao cha faragha.
Baada ya kujadiliana kwa nusu saa, Hamad akiwa ameongozana na Dk Kashililah, alirejea katika ukumbi wa Bunge na kuwataka wajumbe kutawanyika hadi hapo watakapojulishwa.
Hali hiyo iliibua kelele kutoka kwa wajumbe wakitaka kujua iwapo waondoke katika maeneo ya Bunge au la. Hamad alisisitiza kwamba warejee nyumbani hadi hapo watakapojulishwa.
Safi saana. Nchi hii tuko maskin kwa upumbavu wa viongoz wetu. Bora katiba huenda ikasaidia...
ReplyDeleteTatizo katiba wanataka hiwe ya ccm na sio yawananchi, ccm wooote wachumia matumbo na family zao, nikimaliza masomo yangu huku thailand sirudi tena huko tz, wananchi wanishi maisha ya shida sana, wakati viongoz wote wakubwa wanjilimbikizia mali na kufungua acount huku nje ambzo pesa zake zinatosha kabisa kuendeleza miundo mbinu ya hapo nchini ikawa ni faida kwa wote, polen sana viongoz wa ccm kuweni na huruma binadamu wengine
ReplyDeleteHahahaaaaa hicho ndyo chama cha mapinduzi Hapo kila kitu kitapinduliwa
ReplyDeleteukiona kelele ujue ndo panajengwa.
ReplyDelete