Matarajio ya Bunge Maalumu la Katiba kukamilisha kanuni kwa maridhiano yaliyeyuka tena jana huku mambo ndani ya ukumbi yakionekana kuwa vululuvululu kwa baadhi ya wajumbe kuzungumza nje ya utaratibu na wengine kurushiana vijembe.
Baadhi ya wajumbe waliamua kutoleana lugha chafu na kuweka kando hoja za msingi zinazowafanya watofautiane na kuchelewesha kazi ya kuandika Katiba Mpya.
Hali ilichafuka mchana wakati wajumbe walipokutana kupitisha kanuni baada ya mmoja wao, Felix Mkosamali kuomba mwongozo kwa Mwenyekiti wa muda, Pandu Ameir Kificho. Hata hivyo, Kificho alimtaka kukaa chini kwa muda kwa maelezo kuwa wajumbe waliofika katika kikao hicho walikuwa wachache, hivyo mwongozo wake kama ulikuwa unahitaji majibu ingekuwa vigumu kutolewa.
Baada ya muda alisimama, James Mbatia na kuomba mwongozo, akihoji sababu za kutaka kuanza kikao cha kupitisha kanuni hizo wakati wajumbe hawajapewa vitabu vya rasimu ya kanuni zenyewe.
“Mwenyekiti ulitangaza asubuhi kuwa tutagawiwa kanuni kabla ya saa tisa lakini hadi sasa tunataka kusomewa kanuni wakati hatujagawiwa kanuni hizo,” alihoji Mbatia.
Kificho alitoa ufafanuzi kuwa kanuni hizo zilikuwa bado zinadurufiwa na kuwataka wajumbe wawe na nidhamu kwani anapotangaza wanapiga kelele.
Ghafla alisimama Mkosamali tena na kuwasha kipaza sauti na kuhoji kitendo cha mwenyekiti huyo kumpa Mbatia nafasi ya kutoa mwongozo wakati yeye amenyimwa... “Mwenyekiti hivi unaongozaje kikao, inakuwaje mimi nikuombe mwongozo uninyime na mwenzangu umpe? Mwenyekiti nakuheshimu sana, lakini sijui unatumia kanuni ipi kutoa nafasi kwa mjumbe wakati mimi ulinizuia nisiseme,” alihoji Mkosamali.
Baada ya kauli hiyo Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Hawa Ghasia aliwasha kipaza sauti na kwa sauti ya juu alisema “Mtoto mdogo hana adabu.” Kauli hiyo iliibua hasira za Mjumbe mwingine, Moses Machali ambaye naye aliwasha kipaza sauti na kumjibu: “Kubwa jinga halina adabu,” kauli iliyoibua miguno ndani ya Bunge.
Hata hivyo, licha ya Mwenyekiti kutoa onyo kwa kauli hizo kwamba hazifai, Mkosamali alisimama katika sehemu yake na kusema kuwa hakuna mtoto mdogo na kwamba tangu lini mtoto aliishinda CCM.
Chanzo cha tatizo
Chanzo cha mvurugano huo ambao wiki iliyopita kidogo usababishe ngumi kurushwa bungeni, ni mfumo wa upigaji kura katika kupitisha ibara za rasimu, ambao jana uliendelea kuwagawa wajumbe na kufanya ukumbi huo kuonekana kama eneo la mzaha.
Kauli za ‘ndiyoooo’, ‘hapanaaaa’ na vitendo vya kugonga meza viliongezeka katika kipindi cha asubuhi baada ya Mwenyekiti wa Kamati ya Kuandaa Kanuni, Profesa Costa Mahalu kuwaleza wajumbe kuwa kamati yake haijafikia mwafaka wa ama iwe kura za siri au wazi na kwamba suala hilo limerejeshwa kwa wajumbe wenyewe.
Profesa Mahalu alisema uamuzi unaachwa mikononi mwa Kamati ya Kudumu ya Bunge itakayoundwa baadaye. Alisema ili Bunge lisonge mbele baada ya kukwama kwa takribani wiki nzima, vifungu namba 37 na 38 vilivyozua utata vimerekebishwa.
“Tulizungumzia kanuni ya 37 na 38 zinazoelezea utaratibu kufanya uamuzi. Kanuni hizo sasa zitaeleza tu kwamba utaratibu wa uamuzi utakuwa ni wa kura, bila kusema ni ya siri ama ya wazi,” alisema na kuongeza: “Lakini tumeona ni vizuri tukaweka fasili nyingine katika kifungu cha 38 ambayo itaeleza waziwazi kwamba ni aina gani ya kura itakayotumika na kwamba hiyo itategemea itakavyoamuliwa na Bunge hili.
Wajumbe wapinga
Mjumbe Profesa Ibrahim Lipumba ambaye pia ni Mwenyekiti wa CUF, alisema walichokubaliana katika Kamati ya Mashauriano ni kinyume na kilichoelezwa na Kamati ya Profesa Mahalu.
Alisema walikubaliana kuwa kifungu cha 37 na 38 visomeke kuwa mambo nyeti yaliyomo katika rasimu ya Katiba, yapigiwe kura ya siri na ya kawaida yapigiwe kura ya wazi.
“Tulichokubaliana ni tofauti kabisa na hiki ambacho kamati imekiwasilisha. Hatuwezi kufanya uamuzi wakati hatujafikia mwafaka,” alisema Profesa Lipumba.
“Huku ni kukwepa uwajibikaji na haiwezekani tupitishe kanuni wakati baadhi ya vifungu havijakamilika. Kamati imepinga makubaliano yetu,” alisema.
Mjumbe David Kafulila alisema: “Kwa namna tunavyokwenda, hakuna kinachoendelea, bado pande mbili zinavutana na kusababisha masuala yakwame. Tukikutana jioni (jana) na bado hali ni hii ya kupata taarifa nusunusu ambazo hazina mwafaka kuhusu jambo hili, tukubaliane kwamba semina hii isimame kwa muda, watu warudi majumbani kwao ili wafanye makubaliano huko nje.”
Mwenyekiti Kificho alimjibu akisema Rais Kikwete ndiye aliyeitisha Bunge hilo na kwamba hata uamuzi wa kulivunja utafanywa na yeye.
Mjumbe Ezekiah Oluoch alisema iwapo Kamati ya Maridhiano iliyoanza kuketi Ijumaa imeshindwa kukubaliana, kilichopo sasa ni sekretarieti kuandaa karatasi za kura.
“Kwamba sisi tulikuchagua kwa kutumia kura ya siri, sasa tupige kura ya siri ambayo itaamua kura ambayo tunaitaka. Ikiwa tunakuja hapa jioni ukatuletea rasimu ya kanuni ambayo haina vifungu hivi 37 na 38 vya namna ya kufanya maamuzi, sidhani kama umetutendea haki kupitisha vitu nusu,” alisema.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi alijikuta katika wakati mgumu baada ya kuzomewa na baadhi ya wajumbe kwa madai ya kuwapotosha.
kazi kweli kweli
ReplyDeleteMie sihitaji katiba mpya. Ilele ya zamani inatosha
ReplyDeleteKatiba Mpya Muhimu..ila Wabunge wetu wanatuangusha..
ReplyDeletewanaendesha Bunge Kitoto.
Kama vile hawana Busara.. WAPITISHE UAMUZI WA KUPIGA KURA Ili WAFIKIA MUAFAKA.. Wanakula posho tuuuu.
bado siku 68 Bunge limalize Muda wake...BADO HALIJAFUNGULIWA ..Watadai muda hautoshi Na posho ziongezwe ..subiri tuone..hii ndio Bongo!!
Basi ni bola warudi nyumbani kama hawaelewani
ReplyDelete