CCM WAANZA KUVIZIANA BUNGENI

Wabunge wa CCM wamedaiwa kupokea vitisho, kama watakwenda kinyume na msimamo wa chama.
Dodoma. Mpasuko miongoni mwa wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba wanaotokana na Chama Cha Mapinduzi (CCM), umechukua sura mpya, baada ya kuelezwa kuwa wabunge 90 wameorodheshwa kwa lengo la kuhojiwa kwa tuhuma za kukisaliti chama.
Wajumbe hao wengi wao wakiwa ni wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, wamekuwa wakiitwa na mmoja wa viongozi waandamizi wa Serikali ya CCM na kuelezwa wazi kuwa chama hakiridhiki na mwenendo wao.
 Wengi wa wajumbe hao ni wale waliotamka hadharani kuunga mkono muundo wa Muungano wa Serikali tatu, badala ya Muungano wa Serikali mbili ulioboreshwa, ambao ndiyo msimamo wa chama hicho tawala.
Wengine ni wale wanaotajwa kuunga mkono upigaji wa kura wa siri katika kupitisha vifungu vya rasimu ya Katiba Mpya, ikiwa ni kinyume na msimamo wa CCM wa kutaka kura ya wazi.
“Ni kweli hata mimi niliitwa na (akimtaja jina) na kuniambia ametumwa aniletee ujumbe kuwa niko kwenye orodha hiyo na nikiendelea na msimamo huo nitachukuliwa hatua,” alidai mbunge mmoja.
Hata hivyo, mjumbe huyo alidai kuwa kinachofanywa na CCM ni sawa na kumpa mgonjwa wa saratani dawa ya kutuliza maumivu, lakini mwishowe ugonjwa alionao uko palepale.
“Mimi msimamo wangu ambao naamini ndiyo msimamo wa wabunge wengi ni kutaka kura ya siri na Serikali tatu. Nitasimamia msimamo huo, kwani ndiyo dhamira yangu kwa masilahi ya Watanzania,” alidai.
Mbunge mwingine anayetajwa kuwapo kwenye orodha hiyo (jina tunalo) alipoulizwa jana kama ana taarifa hizo alisema, “Ni kweli kuna orodha hiyo ya wabunge 90, lakini mimi sijaulizwa chochote.”
Mbunge huyo alisema, wabunge hao 90 wamewekwa katika orodha nyeusi (Black list) iliyoandaliwa na CCM kimeandaa kama njia mojawapo ya kuwatesa kisaikolojia ili waachane na msimamo wao.
Tayari CCM kupitia kwa Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye kilishaweka wazi msimamo wake kuhusu suala la muundo wa Serikali na kutaka wajumbe wake watetee kwa nguvu zote muundo wa Serikali mbili.


Nape: Huu ni uwongo
Nape alipoulizwa jana kuhusu kuwapo kwa orodha hiyo, alikanusha na kusema huo ni uongo ambao hata shetani ataona aibu kuusema. Chama hakina mpango wa kuwahoji, alisema na kuongeza;
“Msimamo wa Serikali mbili siyo wa mtu mmoja mmoja, ni msimamo wa CCM na msimamo wa Watanzania wengi…. Kama kuna haja ya kuwahoji wanaounga Serikali tatu watahojiwa na wapiga kura wao.”
Ngoma nzito kura ya siri
Wakati CCM wakifanya uamuzi huo, Mwenyekiti wa Muda wa Bunge Maalumu la Katiba, Pandu Ameir Kificho, ameunda kamati ya maridhiano itakayosaidia kufikia mwafaka wa kanuni zenye utata na zilizua mabishano makali bungeni, ikiwamo upigaji kura na Muundo wa Muungano.
Akizungumza bungeni mjini jana, Kificho alisema kamati hiyo imeundwa kwa ajili ya kutafuta maridhiano katika maeneo ya kanuni ya 32 hadi 43 ambayo yamekuwa na tofauti kubwa.
“Kamati hiyo itakuwa imejumuisha wawakilishi kutoka maeneo mbalimbali ya vyama vya siasa na makundi 201.  Kamati hiyo kamili natarajia  nitaitangaza baadaye saa 9:30 leo (jana), watakutana,”alisema.
Alisema makundi mbalimbali katika kamati za vyama vyao na makundi mbalimbali yanayotokana na uteuzi wa Rais kwenye wajumbe 201, ambapo kutokana na wingi wao walipewa nafasi ya kukutana katika Ukumbi wa Pius Msekwa.
“Kamati ya maridhiano inaweza kusaidia kuwajulisha wawakilishi wao nini ambacho tumefikia katika kamati ile ya mashauriano ili iwe rahisi na wao wawe wamepata ile taarifa. Kimsingi ili tuwe na mtazamo wa pamoja kuifanya kazi ya kumaliza kanuni hizo kwa wepesi,” alisema.
Kificho alisema amefikia uamuzi huo ili wiki ijayo waanze kazi ya kupitia na kuichambua rasmi Rasimu ya Katiba.
Hata hivyo, baada ya kauli hiyo, wajumbe kadhaa waliibuka wakiomba miongozo akiwemo, Dk Ave Maria Semakafu, aliyeshauri uteuzi wa Kamati ya Maridhiano kuzingatia usawa wa kijinsia katika upande wa kundi la watu 201.
“Ningeomba busara hiyo kuanzia siku tulipojadili iwe inaongoza uteuzi wote kwa kuhakikisha katika kila kitu ambacho tunakiweka watu tulioko humu ndani tuweze kuwakilishwa kihalali,” alisema Dk Semakafu.
Hali hiyo ilimfanya Kificho kuwataka wajumbe kumpendekeza mwakilishi ambaye anayewakilisha wajumbe 201 walioteuliwa na Rais Jakaya Kikwete ambapo baadhi yao walipaza sauti wakitaka Dk Semakafu kuwawakilisha.

Tags

Post a Comment

6 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
  1. Awa ma ccm sijui wakoje? mungu awalani pumbavu zenu mafisadi nyie

    ReplyDelete
  2. msimamo wa chama ndo mdudu gan kwenye katba, mbona cku mktaka kuiba kura mnata za siri, leo kukamatana uchawi mnata za wazi. mashetani wakubwa nyie.

    ReplyDelete
  3. muileke ccm yange itae! lo abantu baine midomo bwana yooo!

    ReplyDelete
  4. Ujinga kwanza hatukuelewi pumbavu

    ReplyDelete
  5. Katiba haina umuhimu ndio maana wanagongana,ilitakiwa awali kuwe na kura ya maoni kama muungano uewepo au hapana.Wananchi hawajaelezwa faida au hasara za muungano kwa kina ili waamue.Wamebaki wanajiuliza tu inakuwaje Mzanzibar anasuhusiwa kununua nyumba au shamba bara lakini mtu wa bara hawezi kuruhusiwa Zanzibar.Hii ni karne ya 21tujenge vitu vyenye ufafanuzi kuepuka mambo kama ya Ukraine!

    ReplyDelete

Top Post Ad

Below Post Ad