MAKALA : SITTA, ULIOMBA, UKAAMINIWA, SASA TULIPE!

Mjumbe wa Bunge Maalum la Katiba na Mwenyekiti Mteule wa Bunge hilo Bw. Samwel Sitta akibadilishana Mawazo na Mjumbe wa Bunge hilo Mohamed Seif Khatib ndani ya Bunge Maalum la Katiba.
NIANZE kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia afya, mimi pamoja na wewe unayesoma hivi sasa makala haya. Bila yeye kutulinda, huenda hivi sasa tusingekuwa hapa tulipo, tungekuwa sehemu nyingine kabisa ambayo isingetupa fursa ya kuwasiliana kama hivi.
Wiki iliyopita Bunge Maalum la Katiba lilimchagua kwa kura nyingi, Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel John Sitta kuwa Mwenyekiti wake wa kudumu na Samia Suluhu Hassan kuwa makamu wake baada ya kazi kubwa kufanywa na Mwenyekiti wa Muda, Pandu Ameir Kificho, ambaye kwa siku 21, aliweza kukiongoza chombo hicho kutengeneza kanuni ambazo sasa zitatumika kuijadili Rasimu ya Katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kama ilivyowasilishwa na Tume Maalum ya Mabadiliko ya Katiba chini ya Jaji Joseph Sinde Warioba.
Sitta, ambaye aliwahi kuliongoza Bunge la Tisa la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akiwa spika, alijipatia sifa kubwa kwa kuruhusu mijadala bila upendeleo, akiweka mbele kile ambacho mwenyewe amekuwa akidai kuwa ni masilahi ya taifa.
Watu wengi, wakiwemo wanasiasa wa upinzani, walikuwa wakimuona Sitta kama mtu aliyestahili kuchukua nafasi hiyo kutoka CCM, kuliko watu wengine waliokuwa wakitajwa, kitu kinachoonyesha kuwa waliridhishwa kwa kiasi kikubwa na utendaji wake wakati akiwa amekalia kiti ambacho sasa kipo kwa Anne Makinda.
Ingawa mara nyingi historia imekuwa ikitufundisha kujikumbusha, wakati mwingine yapo mambo ambayo hatuhitaji historia ili kujiridhisha kuwa yanaweza kutokea.
Miongoni mwa mambo hayo, ni hili ambalo sasa lipo mbele ya Mheshimiwa Sitta. Analo deni analodaiwa na Watanzania wapatao milioni 45, wanaomtaka asimamie kwa umakini, uzalendo na masilahi ya taifa, wakati akiliongoza Bunge hili maalum kutupatia katiba mpya itakayokidhi matakwa ya wananchi wote.
Inafahamika Sitta ni kada mwaminifu na huenda mtiifu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na wote tunajua msimamo wa chama hiki katika baadhi ya mambo makubwa yanayotarajiwa kuchukua muda mwingi wa majadiliano ambayo yanagusa uhai wetu kama taifa.
CCM inataka Muungano wa serikali mbili kama ilivyo hivi sasa na pia inataka upigaji kura wakati wa kupisha vifungu vya katiba hiyo kufanywa kwa uwazi. Kwa nini chama chake kinataka iwe hivyo? Inafahamika. Muundo wowote wa serikali tofauti na nia ya CCM, maana yake ni anguko lao. Wasingependa litokee.
Na ili hilo lisitokee, ni lazima zipigwe kura za wazi ili wawaone watakaoenda kinyume na msimamo wa chama. Ni dhahiri, hakuna aliye tayari kwenda kinyume hadharani, huku akionekana na vigogo wa chama hicho.
Hatuna matatizo na msimamo wa CCM kwa sababu kila chama kilichomo kwenye bunge hili kina msimamo wake. Watu wote hawawezi kuwa na mawazo yanayofanana, hasa katika baadhi ya mambo yanayogusa masilahi ya taifa.
Ni kwa sababu hii, tunahitaji Mwenyekiti Sitta kutulipa kwa kututendea haki katika mchakato huu muhimu. Hatutegemei kama anaweza kukiangusha chama chake, lakini tunaamini atatuangalia zaidi sisi kama Watanzania na kujua tunachohitaji.
Hatutaki aweke mbele masilahi ya chama chochote, isipokuwa taifa kwanza. Vyama vinaweza kupotea siku yoyote na kusiwe na shida, nchi ikaendelea, lakini taifa likipotea vyama navyo vitapotea. Hoja ziamuliwe kwa busara inayotetea masilahi ya wengi.
Wapo watu wanaomnadi Sitta kama mtu anayefaa kuwa rais ajaye wa Tanzania. Sehemu pekee ya kuthibitisha uwezo huo, ni kutuongoza kupata katiba bora ambayo watu watapata haki zao za msingi na lazima bila kujali chama gani cha siasa kipo madarakani.
Katiba hii inahusu uhai wa Watanzania. Tunategemea itatufaa kwa miaka mingi ijayo, tukiishi bila uhasama wala manung’uniko. Na ili hili lifanikiwe, ni lazima tuwafanye wananchi, ambao hawapo bungeni, kuwa ndiyo walengwa wakuu, badala ya vigogo wanaotetea masilahi yao ya sasa.
Siku zote, mwenye dhamira njema hulindwa na Mungu na hili ndilo tunalolitegemea kutoka kwa Mhe. Sitta ambaye ameapa kwa Mungu kutopendelea. 
siwezi kuolewa na Mbongo.”
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad