Ni maneno yenye kutia simanzi na ambayo yanaamsha kilio. Maneno ya ya Anna Sabai (20) mkazi wa Kitongoji cha Manyata Kijiji cha Nyamakendo Kata ya Mbalibali, wilayani Serengeti, ambaye anapaza sauti kutaka kujua walipo wanaharakati ambao kwa hali aliyonayo , angeweza kupata msaada kutoka kwao.
Ukatili aliofanyiwa Anna, mama wa watoto wawili katika ndoa yake na Hamisi Sabai (20) yenye migogoro na ambayo inazidi kuuweka Mkoa wa Mara kwenye taswira mbaya kutokana na uwingi wa matukio ya ukatili dhidi ya wanawake.
Agosti Mosi, 2013 ikiwa ni siku ambayo wakazi wa wilaya hiyo humiminika mnadani, Anna akiwa na uja uzito wa miezi tisa na akihesabu siku tu kwa ajili ya kujifungua, aliamriwa na mume wake kwenda kuchunga ng’ombe, bila kujali hali yake.
“Kwa kweli nilikuwa na hali mbaya sana,” anakumbuka Anna wakati anaongea na Mwananchi kuhusu ukatili dhidi yake. “Nikiwa malishoni nilikaa chini ya kivuli huku ng’ombe wakiendelea kula majani. Hali ilivyozidi kuwa mbaya nilisinzia. Alipokuja mume wangu akanikuta nimelala na hapo hapo akaanza kunishambulia kwa kipigo, akidai kuwa nilikuwa na mwanamume kutokana na mapenzi kunoga ndio maana nilisinzia na kuacha ng’ombe wanazagaa.”
Anasema pamoja na kujieleza na kwa kuzingatia hali yake, walipofika nyumbani mama mkwe wake Bhoke Sabai alizidi kumtia hasira kijana wake akidai kuwa nilikuwa na mwanaume, natakiwa kupewa kipigo ili iwe fundisho.
“Pamoja na kuwa wakati ananipiga sikuwa najitetea, bado akaona aache fimbo na akachukua panga na kunikata mguu wa kushoto,” anasema Anna huku akitokwa na machozi.
“Niliumia sana... nikatamani kufa, maana hali ilikuwa mbaya. Sikuwa na msaada. Baadaye akanifungia ndani ili watu wasijue; wala hakuna kwenda kutibiwa.”
Amwagiwa tindikali ili kuzuia damu isitoke
Huku akiwa amebeba mtoto wake na kutembea kwa shida, Anna anasema ili watu wasijue unyama aliotendewa, walileta maji ya betri na kumwagia kwenye kidonda.
“Maumivu yalikuwa zaidi ya uchungu wa kujifungua. Nilifikia hatua kama ningepata kitu cha kujimaliza, ningejiua. Nilikuwa nasumbuliwa na mimba na huku naumizwa hivi,” analalamika. “Jamani wanaharakati wanaotetea wanawake wako wapi maana nitakatwa mguu hivi hivi.”
Anasema matokeo yake mguu ukaoza kwa kuwa alikaa ndani muda mrefu na kwamba ndugu zake hawakuambiwa na mama mkwe wake alikuwa akiendelea kumkejeli kila wakati.
“Sijaona watu wenye roho ya kikatili kama hao, kwa kuwa walilenga kuniua bila kosa,” anasema.
Aokolewa na mama yake mzazi
Anasema kuwa akiwa amekata tamaa kwa kuwa alikuwa anafungiwa ndani ili majirani wasijue, kuna wakati alilazimika kumlilia Mungu, kwa nini afe bila ndugu zake kumwona. Ndipo bila kutarajia alishtukia mama yake mzazi, Mnanka Chacha (48) akifika hapo baada ya kutaarifiwa na majirani.
“Nilipomwona mama nikasema basi sasa hata kama nikifa, niko katika mikono salama kwa kuwa huenda maiti yangu itapewa heshima kama binadamu. Nilijua kama ningefia mkononi mwa hao huenda maiti ingetupwa kama mbwa. Nilijisikia ahueni kwa kumuona mama,” anabainisha.
Afikishwa hospitali kwa matibabu
Anasema kwa kupitia polisi mama yake alimfikisha Hospitali Teule ya Nyerere kwa ajili ya matibabu na madaktari walipomwona walimwambia kuwa hawana uwezo tena wa kumtibu kwa hali aliyonayo. Hivyo wakamwandikia barua kwenda Hospitali ya Rufaa ya Bugando ya jijini Mwanza.
Akosa pesa
Kutokana na ukata wake, alishindwa kwenda Bugando na kuamua kurudi nyumbani kwake kwa ajili ya kutafuta wasamaria wema, ili aweze kwenda naye Mwanza kwa ajili ya matibabu.
Mume achana barua ya rufaa
Katika kuhakikisha juhudi za kupelekwa hospitali hazizai matunda, akiamini kuwa mume wake alikuwa ameishajirudi, alimpa barua ya rufaa ili watafute fedha za matibabu, lakini yeye akaichana na kumuacha asijue la kufanya.
“Alichana barua ya rufaa ikawa sina namna yoyote ya kwenda kutibiwa Hospitali ya Rufaa ya Bugando. Ikabidi nikae tu nyumbani nikiangalia mguu wangu unaoza. Kwa kweli nahitaji msaada kwa watu wanaoguswa maana kula yangu na hata ya mtoto ni ya shida. Siwezi kwenda zaidi ya hapa,” anasema.
Anabainisha kuwa mumewe alichana barua kwa madai kuwa nimetoa siri polisi na kwa watu wengine na ndio maana akaamua kumkomoa kwa kuichana ili kupoteza ushahidi.
Ajifungua mtoto wa kiume
Agosti 24, 2013 ikiwa ni siku 24 tangu amefanyiwe ukatili huo, alijifungua mtoto wake wa pili wa kiume ambaye ndiye anazunguka naye kwa sasa na kama si msaada wa wasamaria wema kumpeleka Kituo cha Afya cha Machochwe, huenda angepata tabu zaidi.
“Kwa sasa hakuna fedha zozote za matumizi ambayo mume wangu anatoa kwa ajili ya mtoto. Dada amenichukua na sasa niko kwake Mtaa wa Bomani mjini Mugumu na mwanangu huyu maana yule wa kwanza alifariki dunia,” anabainisha.
Anawaomba wanawake wanaofanyiwa ukatili wafike polisi kutoa taarifa, kwa kuwa amebaini polisi kuna Dawati la Jinsia na mhusika wa dawati, aaliyemtaja kwa jina la Sijali, amekuwa kama ndugu. Anamnunulia dawa na amehangaika naye kwa muda mrefu bila kuchoka.
Dawati la Jinsia wafanikisha kuwanasa watuhumiwa
Katibu wa Dawati la Jinsia Polisi Wilaya ya Serengeti, Sajenti Sijali Nyambuche anasema kwa muda mrefu wamekuwa wakiwasaka watuhumiwa, lakini wanakosa ushirikiano kutoka kwa jamii ikiwemo baadhi ya viongozi.
“Tukajifanya kusahau, nao wakajisahau wakaendelea na maisha ikiwemo kilimo cha tumbaku na tukafanikiwa kuwakamata kirahisi, mama na mtoto kwa tuhuma za kujeruhi,” anasema Sijali.
Anasema wamewafungulia jalada namba MUG/DAW/IR/30/2014 kwa tuhuma za kujeruhi. Katibu wa dawati amekuwa akimpeleka hospitali ili kupata matibabu ya mguu.
Daktari anasema misuli ilivurugwa
Dk. Richard wa Hospitali Teule ya Nyerere anasema baada ya kupiga picha ya X-ray wamebaini kuwa mishipa haikukatwa wakati wa shambulio hilo, bali kuna misuli iliyoharibiwa, kutokana na hali hiyo mguu huo utakuwa kama mwenye ugonjwa wa matende.
“Ni bora akabaki hivyo, akawa anapata dawa inapotokea maumivu...kwa kuwa vidole vimeshakufa ganzi. Zaidi ya hapo ni kukata mguu na kumfanya mlemavu na pia kupata maumivu mapya,” alisema mganga huyo na kushauri aendelee kupata dawa badala ya kukata mguu.
Nasikia hasira nashindwa kucomment ngoja hasira ipungue zidi ya huyo mkundu na mama yake nitarudi wekeni namba yake nataka kumchangia kidoogo matibabu
ReplyDeletePole mpendwa name mungu akupe uvumilivu. Hayo ni mapito tuu
ReplyDeletehivi kwa nini watu wa huko ukatili umezidi? hata wanafuzi wanasema watu toka mkoa huo ndio wanaongoza hata katika migomo ya vuo kwanini je huo mkoa unashule ya ukatili?
ReplyDeleteKwanza na mpa pole mama huyu kwa matatizo aliyo yapata. Pili niujumbe kwa wanaume kama hao ambao wana ukatili kama huo nazaidi ya huo: kama hamjui nini ndoa na nini mapenzi acheni kuoa kwa aji ya tamaa, wanawake mnao wa owa nao nibinadamu kama ninyi. Mimi piya ni mwanaume kwa kitendo hiki amabacho huyu mwanaume na mama ye wamemtendeya uyu mama kweli piya inanitiya uchungu, kama umeshindwa nandowa ni bora uto basi talaka kuliko kuja kuhukumiwa na Mungu kwaji ya vitu kawaida.
ReplyDeletehv mimama mingine ikoje yan badala yy awe anasuluhisha lkn ndo anakuwa anachangia,mwanamke unaangalia kbsa mtt wa mwanamke mwenzio aliyeenda labour km yy na maumivu yaleyale anakatwa mguu na ww unashangilia,daaa imeniuma sana,yan hao ni wakuweka ndan na hakuna dhamana.me ctak kuamin km watt wakike tuna roho mbaya kiasi hcho nlikuwa nackia tu ooh mtu ambae anapaswa kuwa jasusi ni mwanamke cz hana huruma leo ndo nimeamin.yan bora niolewe na mchaga mbahil lkn anajal familia yake kuliko huko mapanga kila kukicha,chakuja kutolewa utumbo najiona kwan nataka,na nyie wapande hzo muelimike kila cku nyie kuchinjana tu mtakuja kukosa wake oooh
ReplyDeleteNumber ya kutuma hela tafadhali. Huyo baba will face the great wrath of God soon..
ReplyDeletemi na visista vyangu vinajifanya vijaji, we ngoja tu, vipate mabwana wa hivi. jeuri yote kwishney
ReplyDelete