Ni hali ambayo imekuwa kama kawaida kwa wachezaji wa Afrika kutafuta kwenye klabu mbalimbali barani Ulaya.
Kutokana na hali ya uchumi iliyopo katika nchi za Afrika, kijana anayecheza soka kwenye viwanja vyenye vumbi kwa sababu ya kukosekana viwanja bora hujikuta akiwa na ndoto ya kujiendeleza kucheza soka nje ya Afrika ili aweze kufanikiwa kimaisha kwa kutumia kipaji chake.
Lakini wakati wachezaji wengi wa Afrika wakiwa na ndoto za kucheza soka katika Ligi Kuu za England, Ufaransa, Ujerumani, Italia, Ureno na Hispania, ripoti iliyotolewa na Shirikisho la Soka Kimataifa (FIFA) hivi karibuni inaonyesha wachezaji wa Afrika wamezidi kumiminika sehemu mbalimbali za dunia kutoka Albania hadi Yemen kwa ajili ya kutafuta ‘malisho’.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya FIFA, katika kipindi cha miaka 25 iliyopita, ukiacha nchi zilizokuwa zikitamba kisoka barani Ulaya, wachezaji wa Afrika wameingia mpaka katika nchi za Ulaya ambazo zilikuwa hazitambi kisoka.
Ripoti hiyo inaonyesha katika miaka ya 1990 wachezaji wa Afrika walikuwa katika timu kubwa tu za Ulaya zinazoshiriki kwenye ligi za juu za nchi, lakini hivi sasa wachezaji wa Afrika wamesambaa mpaka kwenye ligi mbalimbali za chini.
FIFA inasema idadi ya wachezaji wa Afrika itaendelea kuongezeka barani Ulaya. Pia wachezaji wa Afrika wana nafasi kubwa nje ya bara la Ulaya na sasa wengi wapo katika Ligi Kuu ya Marekani, Vilevile wapo katika nchi za Mashariki ya Kati wanacheza soka na kunufaika na fedha zinazotokana na mauzo ya mafuta.
Ukitazama Ligi ya Mabingwa Asia, msimu uliopita kulikuwa na wachezaji wengi wa kiafrika kwa sababu wanacheza soka katika ligi mbalimbali za bara hilo kama ligi ya India, Indonesia, China na nyingine nyingi.
Katika hali ya kushangaza, taarifa ya FIFA inaonyesha wachezaji wa Afrika ni wachache katika Ligi ya Mabingwa ya Amerika ya Kusini.
cha muhimu ni maslah tu
ReplyDeleteTafuteni maisha kotekote duniani
ReplyDelete