WARIOBA AWAKUNA WASOMI NA WACHAMBUZI WA SIASA

Baadhi ya wasomi na wachambuzi wa masuala ya kisiasa hapa nchini wamesema hotuba ya Mwenyekiti wa Tume ya Mabadilko ya Katiba, Jaji  Joseph Warioba itasaidia kubadilisha msimamo wa wajumbe wengi wa Bunge Maalumu la Katiba.

Kauli hiyo imekuja muda mfupi baada ya Jaji Warioba kuwasilisha Rasimu ya Pili ya Katiba katika Bunge hilo tayari kwa kuijadili, kuiboresha na hatimaye kutoka na Rasimu ya Tatu itakayopigiwa kura ya ama kuikubali kuwa Katiba Mpya au la.

Mwanasiasa mkongwe, Njelu Kasaka alisema hotuba hiyo imesaidia kutoa uelewa wa mambo kwa kuwa idadi kubwa ya wajumbe ndani ya Bunge hilo hawakuwa na uelewa juu ya hoja mbalimbali zilizopendekezwa kwenye rasimu hiyo.

“Kutokana na ufafanuzi huo, wengi watakuwa wameelewa kwa nini Tume iliamua kupendekeza muundo wa Serikali Tatu na wala siyo mbili. Itasaidia pia kuwajengea uwezo wa kuhoji katika mijadala ya Kamati itakapoanza kukaa rasmi,” alisema Kasaka ambaye alikuwa miongoni mwa Wabunge 55 walioasisi Kundi la G55 lililotaka kuundwa Serikali ya Tanganyika mwaka 1993.

“Lakini jambo jingine hotuba hii imeondoa ni unafiki na imewaaibisha kwa unafiki wao baadhi ya watu, kwa sababu pamoja na kuongoza Serikali moja ya Jamhuri ya Muungano, imefahamika wazi kwamba Waziri Mkuu kumbe hana mamlaka yoyote yale katika upande wa Zanzibar.”

Kwa upande wake, Profesa Boniventure Rutinwa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), aliunga mkono hoja hiyo akisema kinachotakiwa kwa wajumbe hao ni kujenga imani, kuondoa tofauti zao na kutokubaliana na hoja zenye masilahi ya vyama na  makundi yao badala ya Taifa.

“Kinachotakiwa kwa sasa ni kupima uwezekano kwa kuhoji, je, pamoja na ufafanuzi huo, Serikali Tatu inaweza kuwa mwarobaini wa kumaliza changamoto zote? Lakini pia wanatakiwa kufahamu kwamba inawezekana kuna changamoto nyingine ambazo zinaweza kujitokeza katika muundo huo,” alisema Profesa Rutinwa.

Kwa upande wake, Profesa Penina Mlama aliwataka wajumbe wa Bunge hilo kuchukua hoja hizo na kufikiri kwa mapana zaidi wakati wa majadiliano ili kuondoa athari zinazoweza kujitokeza baadaye.

“Wamerahisishiwa, na kazi imebakia kwao kupima na kufikiria zaidi hotuba hii. Wajumbe watambue kwamba si mawazo ya Jaji Warioba yaliyowasilishwa pale, bali ni mawazo ya Watanzania, ambayo yanatakiwa kupokewa kwa mtazamo chanya ili wasije kuaibika baadaye iwapo watashindwa kufanya uamuzi sahihi,” alisema.

Mjumbe wa Bunge, James Mapalala alisema Jaji Warioba amemaliza kazi ya kuelimisha juu ya  umuhimu  wa Serikali Tatu na anaamini watakaosimama kumpinga wataona haya.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad