YANGA inashuka dimbani leo Jumamosi kucheza dhidi ya watani wao wa jadi, Simba katika mchezo wa kufunga msimu wa Ligi Kuu Bara lakini katika kikosi chao hatakuwepo Golikipa, Juma Kaseja ambaye imefahamika kwamba amepata kibarua cha muda kukinoa kikosi cha vijana chini ya umri wa miaka 20 ‘Ngorongoro Heroes’.
Akizungumza na Mwanaspoti Kocha Mkuu wa Yanga, Hans Pluijm amsema kuwa walipokea maombi kutoka Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kupitia benchi la ufundi la timu hiyo ya vijana wakiomba Kaseja aende kuwanoa makipa wao.
Pluijm alisema mara baada ya kupokea barua hiyo benchi lake lilimruhusu kipa huyo kwenda kufanya majukumu hayo kutokana na kutokuwepo kwenye kikosi cha wachezaji waanaotarajiwa kushuka uwanjani kuumana na Simba leo.
“Ni kweli Kaseja hayupo, tulipata taarifa rasmi kuwa Ngorongoro Heroes ina tatizo la kocha wa makipa, wakatuomba tuwapatie Kaseja ili akawafundishe makipa wa timu hiyo kwa muda,” alisema Pluijm.
“Hatukuwa na sababu ya kumzuia kwa kuwa hakuwa kambini tangu timu ilipokuwa Arusha, tuliona tumpe baraka za kwenda kuwafundisha vijana hao lakini siyo kwamba hakuwa anahitajika katika timu.”