KIKWETE AKUBALI KUONGEZA MUDA BUNGE LA KATIBA

RAIS Jakaya Kikwete amekubali kuongeza muda wa Bunge Maalumu la Katiba katika mazungumzo aliyofanya na mwenyekiti wake, Samuel Sitta.

Hayo yalisemwa na Mwenyekiti huyo wakati akijibu swali la waandishi wa habari katika mkutano wake jana, Dar es Salaam, baada ya kumaliza mkutano wake na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo katika Kanisa la Mtakatifu Yosefu.

Ziara hiyo ambayo amesema ni utaratibu aliouanza kukutana na viongozi wa dini, pia ilimkutanisha na Mufti wa Baraza la WaislamU Tanzania (BAKWATA), Shekhe Issa Bin Shaaban Simba. Sitta alikutana na Rais Kikwete juzi.

Hata hivyo, kwa mujibu wa Sitta, Rais Kikwete hajataja ni lini Bunge hilo litaanza tena kwa nyongeza ya siku 20 kwa mujibu wa sheria, baada ya siku 70 zinazomalizika mwezi huu, kuisha ili kufanya jumla ya siku 90. Lakini amesema uongozi wa Bunge umekusudia lianze tena Agosti mwaka huu.

Alisema lengo la kukutana na viongozi hao wa kidini ni kuwaeleza kinachoendelea Dodoma, kwa kile alichodai viongozi hao wana ushawishi na wafuasi wengi nyuma yao, hivyo si busara kusikia mitaani.

Katika mkutano huo Sitta alikanusha habari ya gazeti moja lililodai anakwenda kuwaangukia viongozi hao na kusema hana dhambi za kufanya hivyo.

“Leo (jana) nimepanga kukutana na viongozi wa dini zetu na si hawa tu nitakaokutana nao, nitaendelea na utaratibu huu kwa viongozi wengi hata wenye wafuasi wachache, hawa wana ushawishi japo hawahusiki sana na siasa lakini ni viongozi wa jamii, wanapaswa kupata taarifa sahihi ya nini kinachoendelea Dodoma,” alisema Sitta.

Alisema katika mazungumzo yake na Kardinali Pengo jana asubuhi, amemweleza kwa kifupi mchakato unavyoendelea Dodoma na yeye (Pengo) alimhakikishia kuwa Kanisa Katoliki linaliombea Bunge Maalumu la Katiba na wajumbe wote ili lengo lifikiwe na Watanzania wapate Katiba mpya na yenye ubora.

Baada ya kutoa maelezo hayo mafupi ya mkutano wake na Pengo, Sitta akijibu maswali ya waandishi wa habari kuhusu mwenendo wa Bunge hilo, ikiwemo kama muda wa takribani wiki tatu uliobaki unatosha kumaliza kazi iliyo mbele yao, alisema muda huo hautoshi.

“Ni dhahiri mpaka Aprili 28 tutakuwa hatujamaliza Bunge, itabidi tupishe Bunge la Bajeti la Muungano, Wawakilishi watarejea Zanzibar na sisi wengine tutabaki Dodoma, bajeti itafanyika si chini ya miezi miwili, yaani Mei na Juni,” alisema na kuongeza: “Jana nilionana na Rais Jakaya Kikwete nikamweleza hali halisi ilivyo, kimsingi alikubali ataongeza muda ingawa hatukufikia kutaja ni lini. Ila sisi tunakusudia tuanze tena Agosti, nimemweleza kwa undani maana hata baadhi ya nchi nyingi zimechukua muda kuandika Katiba, akaona ukweli huu akatuongezea”.

Sitta alisema Bunge litatangaza rasmi utaratibu huo utakapokamilika ila alisisitiza kuwa, kwa hali inavyoendelea hawawezi kuendelea kubaki Dodoma kwa ajili ya Katiba kwa kuwa kisheria siku zitakwisha na pia mwingiliano wa sikukuu za Pasaka na Muungano Aprili 26, zitapunguza siku.

Muundo wa Muungano:

Awali, akizungumzia kuhusu muundo wa muungano hasa baada ya kuibuka kwa madai ya kutaka Hati ya Muungano wakati wa mjadala wa sura ya kwanza ya sita ya Rasimu ya Katiba uliofanyika katika kamati, Sitta aliwataka wabunge kutopoteza muda kujadili serikali ngapi ziwepo.

Aidha, Sitta amesema ipo hatari ya kupoteza muda mwingi kuzungumzia muundo wa serikali uweje, jambo analoona kwa baadhi ya watu, wanataka serikali nyingi kwa uchu wa madaraka wakijua wakikosa uongozi upande mmoja, watapata upande mwingine.

Alisema ingawa suala la serikali ni muhimu kwa kuwa ndio linalotoa dira, ila haja kubwa ipo katika kuipitia rasimu Ibara kwa Ibara kama alivyoagiza Rais Kikwete.

Alitolea mfano suala la uadilifu na kushauri wajumbe wakipitia vizuri, watashauri mfumo gani uwekwe kuwabana zaidi viongozi.

“Kiongozi anapaswa ajue anaingia katika utumishi wa umma si kuchota fedha na kufanya ufisadi bali suala kubwa ni maendeleo ya nchi, ustawi wa wafanyakazi, wakulima na vijana, kuhakikisha sheria zinakuwepo kuzuia mikataba mibovu, kwa mfano Tanesco (Shirika la Umeme Tanzania) inavyopandisha umeme, wananchi wanaumia.”

“Tukiingia katika sura nyingine za rasimu, Katiba lazima ibane tutunge sheria zilizo wazi, angalia suala la Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma, tunajaza fomu kisha zinakuwa siri, sasa zina haja gani, ni za nini, si bora tuache, maana naweza kujaza nina kijumba kibovu kimoja, kumbe nina majumba,” alitoa mfano Sitta.

Alisema, “Ili kuzuia viongozi kujitajirisha, ni lazima sheria ziwe kali la sivyo wizi utaendelea, sheria inapaswa kuwakwamisha wanaopenda madaraka…., maombi yangu kuhusu mchakato, pamoja na purukushani, kutaka kuonekana, vijana machachari, lakini wengi wanataka Katiba mpya ipatikane.”

Sitta akifafanua kuhusu ama serikali tatu ama mbili, alinukuu alichowahi kusema mwanasiasa mkongwe nchini, Kingunge Ngombale- Mwiru kuhusu suala hilo kwamba ni kama wanaotaka serikali tatu wanataka madaraka, kwamba akikosa uongozi katika upande mmoja, apate kwingine.

Hati ya Muungano;

Sitta aliwaambia waandishi wa habari kumekuwepo na madai ya hati ya Muungano katika kamati na kwamba, ni ajabu kuona ndoa iliyodumu kwa miaka mingi, wahusika sasa wamekuwa vikongwe, anatokea mtu anadai cheti cha ndoa.

“Ni kama haamini kwamba hiyo ndoa ilifungwa ama! Ni ajabu kweli, vielelezo ni pamoja na Sheria ya Bunge ya Aprili 5 mwaka 1964, Msekwa akiwa Katibu wakati huo alikwenda katika kamati kueleza yaliyotokea wakati ule, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema amekwenda kueleza.” “Ndoa watu wamefunga miaka, wamekuwa vikongwe, wajukuu leo wanadai cheti cha ndoa, ni upuuzi, mtu anayehitaji utafiti aendelee, hakuna anayemzuia ila haituzuii sisi kuendelea,” alieleza Sitta.

Ripoti za Kamati;

Kwa mujibu wa Sitta, Alhamisi na Ijumaa wiki hii, taarifa za kamati zitatolewa bungeni na maoni ya wengi na ya wachache yataelezwa ili kuruhusu mjadala kuanza ndani ya ukumbi na kwamba katika sura ya kwanza hadi ya sita, kila mjumbe atachangia.

“Baada ya hapo kazi itakuwa nyepesi, siwezi kutabiri kitakachotokea lakini hoja yenye maana itashinda, ukiacha wachache wenye utamaduni wa fujo, wengi wanataka ifike mahali tupate Katiba mpya, tusichezee mabilioni ya Watanzania bure.

Uzoefu wa Kenya;

Sitta alitumia nafasi hiyo kutolea uzoefu wa nchi jirani ya Kenya mwaka 2007 walipoingia katika machafuko ya kisiasa baada ya kushindwa kufanya mabadiliko katika Katiba yao na kufanya uchaguzi.

Alisema kazi inayofanyika Dodoma ni kubwa hivyo inapaswa kufanyika kwa umakini mkubwa vile vile. Akiwa na Mufti Mkuu Akizungumza mara baada ya kukutana na Mufti wa Tanzania, Shekhe Issa Bin Shaaban Simba, Sitta alisema ujumbe wake ulipokewa vizuri katika Ofisi za Bakwata, Dar es Salaam na kwamba Mufti alishukuru hatua hiyo ya Waislamu kushirikishwa.

“Ukweli Mufti amefurahia huu ujio wangu hapa na kuueleza kuwa anafuatilia kwa makini kile kinachoendelea kwa sasa kule Dodoma na zaidi ameuombea mchakato huu uweze kuisha kwa amani na utulivu hadi katiba mpya itakapopatikana” “Zaidi ametutaka wajumbe wote kuvumiliana na kufanya kazi yetu tukitanguliza maslahi ya Taifa na kuachana na misuguano ili hatimaye katiba iweze kupatikana,” alisema Sitta.
Tags

Post a Comment

2 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
  1. good work kip it up

    ReplyDelete
  2. Nadhani sitta anatapatapa hajuwi alitendalo .maana wawakilishi wa makundi yote wamo kwenye bunge hilo sasa hoja na vitimbi hivyo anavyovifanya kwa kumdanganya nani?waachieni waandishi wahudhurie kwenye hizo kamati ili ili ili wawe ni wawakilishi halali wa yanayotokea kwenye vikao hivyo unafiki hausaidii kitu na mwishowe ukweli huibuka tuu .bakwata limeundwa na serikali lenye lengo la kuikumbatia bila kujali dini ya kiislamu inavyoelekeza mradi wanapata mishahara basi .wafuasi wao ni hio serikali. Pengo ndio kiongozi alietajwa na mheshimiwa rais katika ufunguzi wa bunge .MSITUBABAISHE

    ReplyDelete

Top Post Ad

Below Post Ad