KIKWETE"MUUNGANO WETU NI MFANO WA KUINGWA AFRIKA"

Rais Jakaya Kikwete amesema Bara la Afrika lina jambo la kujifunza kutokana na mafanikio yaliyopatikana kwenye Muungano wa Tanganyika na Zanzibar uliodumu kwa miaka 50.

Amesema kuwa kitendo cha Muungano kudumu, kuimarika na kuendelea kustawi kwa nusu karne siyo jambo linaloweza kubezwa na nchi yoyote kwa kuwa zipo baadhi ya nchi zilizojaribu kufanya hivyo, zikashindwa.

“Wapo wenzetu barani Afrika walijaribu, lakini hawakufanikiwa kama sisi, kwani Muungano wao ulidumu muda mfupi na kusambaratika. Wapo waliokaa miaka miwili, miezi na wapo ambao wameanza majadiliano mpaka leo hawajamaliza,” alisema Kikwete.

Kikwete alisema hayo jana Dar es Salaam, wakati akipokea matembezi ya vijana na kuzungumza na wananchi kupitia vyombo vya habari.

Akinukuu maneno ya Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere, Kikwete alisema: “Tanzania ni lulu ya pekee kabisa katika historia ya Afrika, nchi nyingine zote ni za kurithi kutoka ukoloni, Tanzani ni ya kuundwa na sisi wenyewe, kwa hiari yetu wenyewe baada ya kukomboa sehemu zake kutoka ukoloni.”

Alisema, mafanikio yaliyopatikana Tanzania yanaonyesha kuwa pia Shirikisho la Afrika Mashariki linaweza, na nchi za bara la Afrika kuungana na kuwa nchi moja inawezekana.

“Ikiwepo nia thabiti, mambo yakipangwa vizuri, hakuna kisichowezekana kwani njia itapatikana, sisi tumeweza na wenzetu pia wanaweza,” alisema.

Huku hotuba yake ikikatizwa mara kwa mara na vijana waliokuwa wakishangilia, Kikwete alisema kiini cha hotuba yake ni kutaka kujibu maswali mawili yanayohusu Muungano.

Aliyataja maswali hayo kuwa ni;  kwani nini muungano wa Tanganyika na Zanzibar umewezekana na kwa nini umedumu.

Akijibu maswali hayo, alisema kuwa kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012, asilimia 91 ya Watanzania walizaliwa baada ya Muungano na kwamba asilimia tisa tu, ndiyo waliozaliwa kabla ya Muungano huo.

Hivyo, aliamua kujenga hoja za majibu yake kwa kutaja mambo sita aliyoyataja kuwa ndiyo siri ya mafanikio ya Muungano.

Mambo hayo ni kwamba waasisi wa Muungano, Nyerere na Abeid Karume, walikuwa na nia ya dhati ya kuungana, walitanguliza maslahi ya taifa mbele na kuwa watu wa Tanganyika na Zanzibar ni wamoja.

Mambo mengine ni kuwepo kwa uhusiano wa karibu kati ya viongozi wa kisiasa wa Tanganyika na Zanzibar, nia ya kutatua matatizo yanayohusu Muungano na kwamba Muungano unawanufaisha watu, vinginevyo ungekuwa umeshakufa zamani.

Lugha za matusi bungeni

Kikwete alisema kuwa amesikitishwa na matumizi ya lugha za matusi na vijembe zilizotumiwa na Wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, hata baada ya kuwazuia kufanya hivyo wakati akizundua Bunge hilo.

“Inaelekea ushauri wangu hawakuuzingatia, wanatumia lugha za matusi yanayokaribia kuwa ya nguoni,” alisema.

Pia, aliwataka wajumbe wa Umoja wa Katiba wa Wananchi (Ukawa) kurejea bungeni kwa kuwa wananchi hawatawasaidia kutatua matatizo yao, badala yake watasikitika nao tu.

Alisema kuwa hakufurahishwa hata kidogo na kitendo cha Ukawa kutoka nje ya Bunge kwa kuwa anaamini suluhisho lao linapatikana ndani ya Bunge.

Vijana zaidi ya 3,000 kutoka mikoa mbalimbali nchini na maeneo tofauti jijini Dar es Salaam jana walikuwa miongoni mwa watu waliohudhuria katika ukumbi wa PTA, kusikiliza hotuba ya Rais Jakaya  Kikwete ya maadhimisho ya dhahabu ya miaka 50 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Huku wakiwa wamevaa fulana nyeusi zilizokuwa na ujumbe uliosomeka ‘2 zinatosha’, ukimaanisha muundo wa Serikali mbili unaoungwa mkono na CCM.


Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad