MASTAA MATAJIRI WACHUNGUZWA KISA MADAWA YAKULEVYA

Stori: MAKONGORO OGING’

KIMENUKA! Jeshi la Polisi Tanzania kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali za serikali zimeanza kuwachunguza watu wenye majina makubwa ‘mastaa’ Bongo ambao wameibuka na utajiri wa ghafla, Uwazi limeambiwa.

Kwa mujibu wa chanzo nyeti ambacho kiko ‘jikoni’ kwenye jeshi hilo, mbali na mastaa, wengine ambao tayari orodha yao ipo ni wafanyabiashara, wafanyakazi wa serikali na viongozi wa dini ambao wameibuka kuwa mamilionea kwa muda mfupi huku shughuli zao za wazi zikiwa haziwezi kuwatajirisha.

BIASHARA YA MADAWA YA KULEVYA NDIYO KIINI CHA YOTE
Chanzo: “Imeonekana kuwa mastaa wengi wanaibuka kuwa na utajiri siku hizi, huenda wanajihusisha na kusafirisha madawa ya kulevya.

“Ndiyo maana wengi wao kila kukicha, mara wapo China, mara India, wengine wanakwenda mpaka Thailand. Hao wanachunguzwa kwa mtindo wa nyendo, kila mmoja ambaye yumo kwenye orodha ya jeshi amewekewa askari wawili wa kumfuatilia.”

KUKAMATWA
Chanzo hicho kikaendelea kusema kuwa wale ambao watathibitika kwamba biashara zao za wazi haziwezi kutoa utajiri wa ghafla watakamatwa na kuhojiwa.


DIDA AMESHAKAMATWA, AMESHAHOJIWA
Chanzo hicho kilieleza kuwa katika oparesheni hiyo maalum, watu kumi wameshakamatwa, akiwemo Mtangazaji wa Kituo cha Redio cha Times FM, Hadija Shaibu ‘Dida’.
“Watu kumi tayari wamekamatwa na kuhojiwa. Yumo yule mtangazaji Dida wa Mchops (siku hizi si wa Mchops). Saba wamekwenda na maji, watatu akiwemo Dida waliachiwa baada ya kuthibitika kwamba mali zao ni halali,” kilisema chanzo.

IKOJE KWA VIONGOZI WA DINI?
Chanzo kilisema kuwa kuhusu viongozi wa dini ambao nao wameibuka kuwa matajiri wa kutupwa, wamejenga mahekalu ya maana, nao wanachunguzwa na kati ya watu kumi waliokamatwa, yumo mchungaji mmoja (hakumtaja jina) ambaye aliachiwa.

“Lakini orodha ya hawa ni ndefu, kumbe wengi wanajihusisha na kuuza madawa ya kulevya. Nao wamewekewa askari wawiliwawili ambao wanaingia hadi kwenye ibada zao lakini wenyewe hawajui,” kilisema chanzo. 

JOTI WA KOMEDI  ATAJWA
Katika hali ya kushangaza, chanzo hicho kilidai kuwa staa ambaye alikuwemo kwenye orodha na akafuatiliwa na kuachiwa ni msanii wa Kundi la Orijino Komedi, Lucas Mhuvile ‘Joti’ ambapo ilidaiwa hakuonekana kuwemo kwenye cheni ya wauza unga nchini.

“Lakini hata hiyo orodha nyingine si kwamba wamehukumiwa kuhusika kufanya biashara hiyo ila wanachunguzwa,” kilisema chanzo hicho.

YAMEKUJAJE?
Hatua hiyo, kwa mujibu wa chanzo, imekuja kufuatia madai ya wananchi wengi kwamba matajiri waliopo mtaani wengi ni wauza unga ambao hufanya biashara hiyo waziwazi, wengine wakisema kuna polisi wanaojua kila kitu lakini kwa sababu wanakatiwa kitu kidogo wanawalinda.

“Si kwamba serikali haitaki watu wawe  na maendeleo makubwa, bali utajiri wao uwe wa wazi wenye vielelezo vinavyokubalika. Kwa sasa vijana wengi wakiwemo wasanii na wachezaji wanashindana kwa utajiri lakini baadhi yao ndiyo hivyo tena wamegundulika wanajihusisha na biashara ya madawa ya kulevya, wengine wamekamatwa nje ya nchi na wanakabiliwa na hukumu ya kifo,” kiliongeza chanzo hicho.

UWAZI LAWASAKA WALIOIBUKA NA UTAJIRI
Kama kigezo kikubwa ni utajiri wa ghafla, Uwazi liliwasaka mastaa ambao walishaandikwa na Magazeti Pendwa ya Global Publishers (likiwemo Uwazi lenyewe).

DIDA
Katika Gazeti la Ijumaa Wikienda toleo la wiki mbili nyuma kulikuwa na kichwa cha habari ukurasa wa mbele; UTAJIRI WA DIDA GUMZO.
Katika habari hiyo Dida alisema:

“Mimi sipendi kuanika vitu ninavyomiliki ila ni kweli nina nyumba mbili, moja Kigamboni na nyingine Goba ya gorofa. Magari ninayo matatu, hilo Vogue mchakato unaendelea, ukikamilika nitaliingiza nchini.
 “Kuhusu miradi yangu mingine siwezi kuianika hadharani kwa sababu, kwanza sipendi kabisa mambo hayo.”

Hata hivyo, Dida alikiri kukamatwa Machi, mwaka huu na kuhojiwa kisha kuachiwa. Alikuwa anakwenda Hong Kong, China.
GPL

Post a Comment

1 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad