WAKATI klabu ya Mbeya City ikibanwa jijini Dar es salaam na Ashanti United kwa kutoka sare ya kutofungana, mdudu wa sare aliibukia pia uwanja wa Kaitaba wakati kagera Sugar na Simba zilipofungana 1-1.
Mbeya City iliyokuwa ikipewa nafasi ya kuiengua Yanga kwenye nafasi ya pili japo kwa muda, ilishindwa kufurukuta kwa watoto wa mjini na kuambulia pointi moja iliyowafanya wafikishe pointi 46.
Pointi hizo ni sawa na za Yanga ambayo kesho inatarajiwa kushuka dimbani kucheza na JKT Ruvu katika pambano linalosubiriwa kwa hamu litakalochezwa uwanja wa Taifa.
Mjini Bukoba, wenyeji Kagera Sugar ilishindwa kufurukuta nyumbani baada ya kulazimishwa sare ya bao 1-1, wenyewe wakilazimika kusawazisha bao la Simba lililofungwa na Zahor Pazi katika dakika ya 45.
Bao hilo la kuwasawazisha, liliwekwa kimiani na Themi Felix 'Mnyama' katika kipindi dakika ya 61 na kuifanya timu yake kugawana pointi na Simba na kuendelea kusaliwa katika nafasi ya nne na tano.
Ligi hiyo inatarajiwa kuendelea kesho kwa mechi nne katika viwanja mbalimbali Coastal Union kuumana na Mgambo JKT kwenye uwanja wa Mkwakwani, Yanga kuumana na JKT Ruvu uwanja wa Taifa, Oljoro JKT itapepetana na Prisons ya Mbeya na Rhino Rangers itaikaribisha Mtibwa Sugar mjini Tabora, mecchi ya Azam na Ruvu Shooting imesogezwa mbele hadi Jumatano.