TAMKO LA RASMI KUHUSU URAIA PACHA KUTOKA KWA WATANZANIA WAISHIO WASHINGTON DC

Sisi watanzania wa Washington DC, Maryland na Virginia pamoja na vizazi vyetu tunapenda kutoa pongezi kwa Serikali yetu ya Tanzania kwa Mchakato mzima wa Katiba mpya unaoendelea.

Tunapenda Kutoa Tamko Rasmi kwa Bunge la Katiba na Serikali kutoa haki ya Uraia kwa Watanzania Wote popote walipo Duniani. Uraia Wa Mtanzania aliezaliwa Tanzania na Kizazi chake usijali hali na mahala alipo Mtanzania Huyo.

Kutokubaguliwa kwetu kwenye swala hili la Haki ya Kuzaliwa na Kuruhusiwa kwa Uraia Pacha kwa Waliozaliwa Tanzania na Vizazi vyao ni muhimu katika kuimarisha nchi, kutoa haki kwa Watanzania wote waliozaliwa Tanzania pamoja na vizazi vyao. Haki ya kuzaliwa  kwa watanzania wote kutaimarisha Zaidi mahusiano kati ya watanzania tulio nje na serikali yetu tukufu.

Watanzania Hapa Washington, DC na tulio nje tumekuwa mbele kuitangaza nchi yetu, kuiwakilisha nchi yetu na kuibeba Bendera ya Tanzania huku nje . Watanzania tumekuwa tukishirikiana na Viongozi wa nchi yetu wanapokuja huku nje kwenye mambo mbalimbali ya kimaendeleo, kijamii na kielimu ili kuhakikisha nchi yetu inasonga mbele.

Watoto wetu waliozaliwa huku nje wamekuwa wakiimba nyimbo ya Taifa la Tanzania wanapokuja viongozi mbali mbali huku na kwenye shughuli mbali mbali za kitaifa na kimataifa ambazo huwa tunaiwakilisha nchi yetu huku ugenini. 

Watanzania wenye uraia wa Tanzania na Wale waliochukua Urai wa Hapa , pamoja na watoto wao waliozaliwa hapa ambao ni Wamarekani kwa kuzaliwa tunajisikia na tunaipenda Tanzania kama wenzetu walioko Marangu au Kimanzichana. Tofauti iliyopo ni kwamba sisi tuko huku na wenzetu wako Biharamulo. Watoto wetu wamezaliwa hapa na Binamu zao wamezaliwa Chalinze.  Sisi sote na watoto wetu ni watanzania na tunataka tutambulike na kuwa na haki sawa.

Watanzania wa Washington DC, tumekuwa tukishirikiana kwa hali na mali na Ubalozi wa Hapa  kuitanganza nchi yetu na kuitetea na kuiletea sifa nzuri Tanzania. Hivi Sasa Ubalozi wetu hapa Unaandaa sherehe za Miaka 50 ya Muungano na Ni sisi Watanzania wa Ughaibuni tutashiriki kwa Moyo Mmoja na nguvu zote kuipeperusha bendera ya Tanzania kwa niaba ya nchi nzima. Watato wetu wataonyesha utamu wa nyimbo ya Taifa la Tanzania. Viongozi wa Taifa watazungumza na watanzania wa hapa na kujadili maendelea na muelekeo wanchi.     Sisi Ni Watanzania.


Tanzania Itajengwa Na Watanzania. Sisi Na Vizazi Vyetu Huku Ughaibuni ni Watanzania.

Iddi Sandaly,

Rais Wa Jumuiya Ya Watanzania , 
Washington DC, Maryland na Virginia.
Tags

Top Post Ad

Below Post Ad