TANZANIA NA WASOMI WASIO KUWA NA MAADILI..WANAO IFILISI NCHI

Tunatumia fedha nyingi sana zisizolingana na uwezo wetu kuwasomesha watu wachache, ili baadaye na wao walete faida kubwa kiasi hicho hicho katika nchi.

Tunatumia fedha kutafuta faida katika akili ya mwanadamu...tunatarajia mwanafunzi tuliyemsomesha Chuo Kikuu aje kutusaidia kiasi kikubwa zaidi katika kazi za maendeleo kuliko yule ambaye hakupata bahati hiyo.

Tunatoa vingi kumpata mwanafunzi aliye chuo kikuu ili baadaye tuweze kupokea vingi zaidi kutoka kwake.”

Haya ni maneno ya Mwalimu Julius Nyerere aliyoyasema miaka mingi iliyopita.

Ili fikra za Mwalimu Nyerere na malengo ya elimu yafikiwe kuna kitengo muhimu katika mfumo wa elimu ambacho kinamjenga mtu awe kamili na afanye kama jamii inayotarajia.

Haijalishi una ujuzi na maarifa gani, kama huna maadili kwa ukamilifu wake huwezi kuisadia jamii au nchi, badala yake utakuwa mzigo wa nchi na jamii, yaani mmoja wa watu wanaoipora na kuifilisi nchi.

Maadili ya mtu yanazaliwa kwenye vipaji mahsusi vya utambuzi wa hisia za mwanadamu na kwenye vitendo na tabia za mtu za ndani ya roho na moyo wake. Udanganyifu hauko akilini uko rohoni. Wizi hauko akilini uko moyoni, chuki haiko akilini iko rohoni

Hivyo, maadili hubeba tunu kama uaminifu, amani, busara, hekima, uwazi, heshima, kujituma, haki, hamasa ya kazi, uzalendo, utu, wema, uadilifu. Hata kujitambua na kujiamini ni maadili kwenye kitengo cha weledi wa kiroho.

Matukio ya ufisadi na ubadhirifu wa mabilioni ya pesa za umma, kwa asilimia karibu 99 yamekuwa yakifanywa na wasomi.

Ripoti za chenji za rada, Richmond, uuzwaji wa wanyama, kughushi malipo hewa, kampuni bandia, matusi na kejeli bungeni, kufadhili uharamia na ujangili, wizi wa benki kuu na mamia ya matukio ya wizi mkubwa wa mali ya umma yanafanywa na wasomi.

Wananchi wa kawaida huko vijijini wametulia kimya wakiendeleza jitihada zao za kutafuta riziki kwa njia halali huku wakibinywa kwa kodi na Serikali, ili wasomi wanufaike.

Chuki inayopandikizwa sasa katika nchi yetu inafanywa na watu waliosoma wenye malengo dhalimu. Kuporomoka kwa uchumi wa nchi na hata kuanguka kwa elimu yetu sababu kuu ni wasomi waliojivika sura tofautitofauti kulingana na ofisi au mahali wanakofanyia kazi.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad