TIGO KUTOA HUDUMA YA FACEBOOK KWA KISWAHILI

Kampuni ya simu za mkononi ya Tigo Tanzania imezindua mpango wa kutoa bure huduma za mtandao wa kijamii wa Facebook kwa lugha ya Kiswahili.

Huduma hiyo inayotolewa kwa mara ya kwanza, itawanufaisha wateja wake wote nchini na wale wa nchini nyingine za Afrika Mashariki.

Akizungumza kwenye uzinduzi wa ushirikiano huo Dar es Salaam jana, Mkurugenzi Mkuu wa Tigo, Diego Gutierrez alisema ushirikiano huo utawawezesha wateja wanaotumia mtandao wa Tigo kuperuzi kwenye Facebook kupitia simu zao za mkononi bila gharama zozote na kwa lugha ya Kiswahili badala ya Kiingereza.

“Ni fursa ya pekee itakayowawezesha watumiaji wetu wapatao milioni mbili kuungana na wenzao wanaotumia mtandao huo wa kijamii ndani na nje ya nchi bila kikomo,” alisema Gutierrez na kuongeza:

“Hii ni mara ya kwanza kwa mtandao wowote mkubwa wa kijamii kupatikana kwa lugha ya Kiswahili… lugha ambayo inatumika kwa Watanzania na watu wa Kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika.”

Mkurugenzi huyo alisema mtandao wa kijamii wa Facebook umekuwa chachu kubwa ya utumiaji wa data na kwa kulitambua hilo, wameamua kuwaletea wateja wao ladha mpya ya kutumia mtandao huo kwa lugha yao asilia ili kunufaika zaidi kulioko kutumia mtandao kwa lugha ya kigeni.

“Hii ndiyo maana halisi ya maisha ya kidigitali (digiti)… huduma hii mpya itafungua milango mipya ya kielimu, biashara na kiuchumi kwa watumiaji wa mtandao wetu duniani.”

Tanzania ni nchi ya pili kupata fursa ya kuzinduliwa kwa huduma hiyo. Paraguay ilikuwa ya kwanza kupata huduma sawia na hiyo ambayo ilizinduliwa Desemba mwaka jana na watuamiaji wa mtandao wa Tigo walianza kutumia huduma hiyo kwa lugha yao ya Kiguarani.

Mkurugenzi wa Mtandao wa Facebook wa Ushirikiano na Ukuaji wa Kimataifa, Nicola D’Elia alisema ushirikiano huo ni wa kwanza nchini kwa kushirikiana na kampuni hiyo ya simu kuwapatia Watanzania wengi uwezo wa kuwasiliana kwa lugha yao na kupata huduma za data bure.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad