WAATHIRIKA WA MILIPUKO YA OSAMA UBALOZI WA MAREKANI WAFURAHIA FIDIA

Baadhi ya wanafamilia wa waliopoteza ndugu kwenye shambulio la ugaidi katika Ubalozi wa Marekani jijini Dar es Salaam mwaka 1998, wameelezea kufarijika kutokana na malipo ya fidia, licha ya kwamba hayawezi kurejesha uhai wa waliokufa.

Wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti, ndugu hao walisema, licha ya mahakama nchini Marekani kuwapa fidia lakini pengo la jamaa zao halitazibika.

Wiki iliyopita, Mahakama Kuu ya Marekani, ilitoa amri ya kuwalipa fidia ya dola za Marekani 957 milioni (Sh1.555 trilioni) waathirika 23 wa shambulio hilo.

Jaji Thomas Bates katika hukumu yake alisema kati ya fedha hizo, Dola za Marekani 420 milioni (Sh670 bilioni) watapewa ndugu wa marehemu watano na waathirika wanne wa Tanzania wakati kitita kilichobaki kitakwenda kwa waathirika ambao ni Wamarekani.

Jaji Bates alisema Serikali za Iran na Sudan zitawajibika kulipa fidia hizo kutokana na kuhusika na mashambulio hayo mabaya kuwahi kutokea Afrika Mashariki.

Mmoja wa jamaa waliopoteza maisha katika tukio hilo, Kulwa Ramadhan alisema anasubiri kuletewa taarifa zaidi kuhusu taratibu za kupata fidia hiyo.

“Huwezi kuwa umeridhika na fidia kwa kuwa tumepoteza ndugu zetu lakini pia hata hicho kilichopatikana hatukukitarajia kupata,” alisema Ramadhan.

Alisema kuna baadhi ya jamaa wa marehemu watano hawakuingizwa kwenye idadi ya watakaopata fidia kutokana na kuchelewa kujiandikisha katika kesi hiyo.

“Baada ya tukio uongozi wa Ubalozi wa Marekani ulituambia tutoe taarifa zetu zote za mawasiliano na kwamba tusibadilishe namba za simu kwa ajili ya kuwasiliana kinachojiri.

“Lakini kuna baadhi ya jamaa walibadilisha namba zao na kufanya mawasiliano kuwa magumu hivyo kushindwa kuingizwa katika idadi ya wadai katika kesi hiyo,” alisema.

Ramadhan aliyempoteza pacha wake, Dotto Ramadhani alisema baadhi ya jamaa walijitokeza baadaye baada ya hatua muhimu za kesi kufanyika kitendo ambacho kiliwazuia kushiriki katika kesi.
Tags

Post a Comment

2 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad