ALIYEKUWA Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, ametoa siri ya msimamo wa majeshi ya Tanzania kuhusu muundo wa Muungano wa sasa.
Jaji Warioba ametoa siri hiyo huku kukiwa na vitisho kutoka kwa baadhi ya wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba wanaotokana na Chama Cha Mapinduzi (CCM) pamoja na viongozi waandamizi wa serikali kwamba muundo wa Muungano wa serikali tatu ukipitishwa jeshi litachukua nchi.
Akifichua msimamo huo wa majeshi, Jaji Warioba alisema wakati wa kukusanya maoni ya rasimu ya kwanza na ya pili ya Katiba, baadhi ya wanajeshi walieleza bayana kuwa moja ya kero kubwa ya Muungano wa serikali mbili wa sasa ni kupiga mizinga 21 kwa viongozi wawili tofauti walio katika nchi moja.
Jaji Warioba alitoa kauli hiyo jana jijini Dar es Salaam wakati akichangia mada katika uzinduzi wa ripoti ya utafiti ya taasisi ya Twaweza iliyolenga kujua ni jinsi gani Watanzania wanaiona Katiba.
Katika uzinduzi huo wa Twaweza wasemaji wengine walikuwa Dk. Khamis Kigwangwala, aliyemwakilisha Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahaman Kinana, na Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Julius Mtatiro.
“Kila nilipokwenda kukusanya maoni sehemu yenye makambi ya jeshi, tulifika na mara nyingi tulikuwa na Jaji Agustino Ramadhani na Dk. Salim Ahmed Salim, kero yao kubwa waliyokuwa wanatueleza ni kitendo cha kuwapigia mizinga 21 viongozi wawili walio katika nchi moja, mara Bara mara Visiwani,” alisema Jaji Warioba.
“Kama jeshi lina dhamira ya kuchukua nchi lingeweza kufanya hivyo kwa vitendo vya rushwa na ufisadi vilivyotamalaki nchini. Wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba wanapaswa kuwa makini na kauli zao katika kulihusisha jeshi na masuala ya kisiasa,” aliongeza.
Akizungumzia vitisho vinavyotolewa na baadhi ya viongozi kwa wananchi kwa kutumia mgongo wa jeshi, Jaji Warioba alisema wanaofanya hivyo hawalitakii mema taifa na badala yake wanataka kuwapa hofu ya bure wananchi.
“Mimi nasema wasinishambulie binafsi, wajibu hoja za wananchi kwa sababu walizozitoa za kutaka serikali tatu na huu mtindo wa kusingizia kuwa gharama zitakuwa kubwa, mara jeshi litachukua madaraka ni upotoshaji mkubwa unaofanywa kwa makusudi,” alisema.
Ingawa hakutaja majina ya viongozi waliotoa kauli kwamba serikali tatu zikipitishwa jeshi litachukua nchi ni dhahiri kuwa Jaji Warioba alimlenga Rais Jakaya Kikwete na William Lukuvi, ambao kwa nyakati tofauti wamepata kutoa kauli za kutishia jeshi kuchukua nchi.
Jaji Warioba ambaye amepata kuwa waziri mkuu, aliongeza kuwa ni jambo la hatari kwa viongozi wa serikali kutumia majukwaa ya dini kuligombanisha taifa kwa misingi ya imani.
“Kwa kweli hii ni hatari, tumezoea pale tunapokuwa na tofauti zetu kukimbilia kwa viongozi wa kiroho kupata nasaha zao, leo tunakimbilia kwenda kuwagawa wananchi na jambo hili linafanywa wazi wazi,” alisema Jaji Warioba.
Ahofia mchakato mwingine wa Katiba
Jaji Warioba alisema kwa hali ilivyo ndani ya Bunge la Katiba, hata kama Katiba itapatikana haitaishi kwa miaka 50 ijayo bali itaamsha ari ya wananchi kutaka katiba yenye ridhaa yao ndani ya miaka hata mitano tu.
Alisema kinachofanyika bungeni ni walio wengi kutaka kupitisha mambo yao na wachache kuzuia hali hiyo isitokee, huku rasimu nzima ikiwa imeachwa pembeni.
Jaji Warioba aliongeza kuwa kinachomshangaza zaidi ni kuona rasimu ambayo ni mawazo ya wananchi ikibezwa na baadhi ya wajumbe wa bunge hilo, huku wakiendelea kusema wametumwa na wananchi wawawakilishe.
Katika hali ya masikitiko Jaji Warioba aliwaomba wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba kutambua wajibu walio nao mbele ya Watanzania na wafanye kila wanaloweza kuhakikisha majadiliano wanayoyaendesha hayawi chanzo cha kuigawa nchi.
Alisema hatari kubwa inayoonekana ni kuligawa taifa kutokana na lugha inayotolewa na kila upande katika kutetea hoja wanazoamini.
“Kama leo unamuita mtu mtoto wa shetani, halafu unasema mkutane katika maridhianao, hii ni ngumu na tusipokuwa makini na lugha hizi nchi itagawanyia huku tukiona,” alionyo Jaji Warioba.
Hataki uteuzi wowote
Katika hatua nyingine, Jaji Warioba alisema hayupo tayari kushika nafasi nyingine yoyote ya uteuzi na badala yake anataka aachwe akalee wajukuu zake.
Alitoa kauli hiyo baada ya mwandishi wa gazeti hili kumuuliza kama atakuwa tayari kupokea uteuzi mwingine wowote baada ya wajumbe wa Bunge la Maalumu la Katiba na viongozi waandamizi wa serikali kuamua kumshambulia binafsi kutokana na maoni ya wananchi aliyoyaratibu chini ya usimamizi wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Alisema hali hiyo inamsikitisha na hawaelewi watu wanaomshambulia kwamba wanafanya hivyo kwa sababu gani.
“Kuna watu walikuja na kusema haya ya tume ni mawazo yetu ya zamani kwa kuwa tulikuwa katika tume ya Jaji Kisanga na Bunge la G 55, ninachoweza kusema katika tume ya Jaji Kisanga hatukuwa sehemu yao na G 55 wengine katika tume ya sasa wala hawakuwa wabunge, hivyo mashambulizi haya hayana msingi kwetu na mimi nimeshasema waniache niwalee wajukuu zangu, wao wajibu hoja za wananchi,” alisisitiza Jaji Warioba.
Kigwangwala aja na wazo jipya
Mchangiaji wa pili katika mjadala huo, Dk. Khamis Kigwangwala, aliyemuwakilisha Katibu Mkuu wa CCM, Kinana, alisema kilichofanywa na tume ya Jaji Warioba ni kinyume cha hadidu rejea walizopewa kukusanya maoni.
Alisema kama tume iliona kuna haja ya wananchi kujadili muundo wa muungano, wangerudi kwa mtu aliyewateua (Rais) ili wapate ridhaa ya kukusanya maoni hayo kutoka kwa wananchi.
Alisema tume haikutumwa kujadili muundo wa Muungano au kwenda kuifufua Tanganyika na badala yake ilitakiwa ihakikishe Watanzania wanapata Katiba mpya bila kuathiri muundo wa Muungano uliopo.
Aliongeza kuwa muundo wa Muungano unahitaji mchakato wa peke yake, tofauti na ilivyofanywa na tume ya Jaji Warioba.
Kuna mambo mengi na mazuri yaliyoletwa na rasimu sasa yanapitishwa bila ya kujadiliwa na badala yake tunajikita katika muundo wa Muungano, hili ni tatizo ambalo tume imezalisha,” alisema Dk. Kigwangwala.
Hata hivyo kauli hiyo ya Kigwangwala ilipata upinzani kutoka kwa washiriki mbali mbali, ambapo Maria Sarungi alisema sheria ya mabadiliko ya Katiba iliipa tume uhuru wa kujadili yale mambo watakayoona yanafaa, kauli iliyoungwa mkono na Jaji Warioba na Profesa Sharif Ahmad.
Katika hatua nyingine, Profesa Samuel Wangwe, alionyesha kumshangaa Dk. Kigwangwala kutetea hoja ya muundo wa serikali mbili na kusema ni msimamo wa CCM huku wanachama wakiwa hawajashirikishwa katika maoni hayo.
Mtatiro ataka utafiti uheshimiwe
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Julius Mtatiro, alieleza kuwa kinachofanyika katika Bunge Maalumu la Katiba ni kundi moja kutaka kujadili rasimu waliyotoa mfukoni na kuiacha iliyofanyiwa utafiti.
Alisema rasimu ya tume ipo na inaelekeza namna walivyofanya utafiti, na kupata maoni ya wananchi, lakini rasimu nyingine haielezi, jambo aliloeleza wazi kuwa hawako tayari kuijadili.
Alisema hatua ya Rais Jakaya Kikwete kutaka kuacha jina kuwa amewapatia Watanzania Katiba, ndiyo imelifikisha suala hili kuwa la kichama zaidi badala ya kuzingatia mapendekezo muhimu aliyofikishiwa.
“Sisi wapinzani tulimwambia suala la Katiba ni uhai wa taifa lolote, halihitaji haraka kama ya Voda fasta, tukapendekeza maeneo ya msingi ya kufanyiwa kazi kisha ndiyo tuanze mchakato mzima, wenzetu hawakukubali na rais alitaka aache jina kuwa amewapatia Watanzania katiba mpya lakini tunayokwenda kuipata haitakuwa ya wananchi,” alisema Mtatiro.
makubwa
ReplyDeleteCCM wanatumia nguvu kufanya mambo yasiyo na tija kwa wananchi, waache sera hewa@
ReplyDeletehuyu warioba mnafiki tu hajawahi kupita kambi yoyote ya jeshi kuhusu katiba mpya asitake kudanganya uma wa watanzania, jeshi limekaa kimya kusubir kuona hatma ya hilo bunge la katiba maana hata wao hawatimiziwi maslahi yao
ReplyDelete