Baada ya ukimya wa muda mrefu tangu kuwe na habari kuwa kampuni ya Apple imepanga kununua headphones zinazotengenezwa na Beats Electronics ‘Beat by Dre’, Jana kampuni hiyo imethibisha mpango huo.
CEO wa Apple, Tim Cook amethibisha kuwa kampuni yake imeshafanya mazungumzo na Jimmy Lovine na Dr Dre na kwamba makubaliano yao ni kuwalipa Lovine na Dre kiasi cha dola bilioni 3.
Cook ameeleza uhusiano kati ya kampuni yake na Lovine na Dre akitolea taswira ya mahusiano ya wawili wanaojuana kwa miaka mingi na sasa wanaishia kwenye ndoa itakayokuwa imara.
“Tumekuwa tukiwafahamu hawa jamaa muda wote, tumechumbiana, tumekuwa na uhusiano imara na sasa tunafunga ndoa. Uhusiano huu umeanza muongo mmoja uliopita, kwa hiyo tunafahamu kuwa kuna utamaduni unaofit pande zote mbili.” Amesema Cook kwenye maelezo yake.
Kati ya dola bilioni 3, Apple watalipa fedha taslim dola bilioni 2.6 na kiasi kingine kitakuwa katika share ya bidhaa.
Lovine na Dre wote watapewa nafasi ya kuratibu katika kampuni ya Apple kwa upande wa muziki japo Cook hakueleza wazi wajibu na kazi watakayokuwa wakiifanya.
Manunuzi haya yanakuwa kati ya makubalino makubwa zaidi katika historia ya kampuni ya Apple kwa miaka 38.
Mchongo huu utakapokamilika, Dr Dre atakuwa anatembea kifua mbele ambapo Forbes itabadili orodha ya majina ya wana hip hop matajiri zaidi duniani na kumfanya Dr Dre kuwa mwana hip hop wa kwanza kuwa bilionea.