Tuhuma za ufisadi wa zaidi ya Sh200 bilioni katika akaunti ya Escrow ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) zinaonekana kuwa kaa la moto na jana zilitikisa Bunge na kuibua mvutano mkali.
Hata hivyo, suala hilo sasa limekabidhiwa kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) ili kubaini ukweli wake.
Tuhuma hizo ziliibuliwa juzi na Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila (NCCR-Mageuzi), ambaye alisema kashfa hiyo ni zaidi ya ile ya Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) ya BoT iliyotokea mwaka 2005.
Kafulila alisema ufisadi huo unamhusisha Waziri wa Nishati na Madini, Waziri wa Fedha, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Gavana wa BoT na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umeme (Tanesco).
Ingawa Kafulila hakutaja kwa majina, Waziri wa Nishati ni Profesa Sospeter Muhongo, wa Fedha ni Saada Mkuya, Katibu Mkuu wa wizara hiyo (Nishati) ni Eliakim Maswi na AG ni Frederick Werema.
Hata hivyo, akihitimisha hotuba ya bajeti yake na kujibu hoja mbalimbali za wabunge, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda alimwagiza CAG na Takukuru kuchunguza tuhuma hizo ili kubaini ukweli.
“Hoja iliyopo na inayoleta ubishani ni kuondoa pesa kutoka akaunti ya Escrow na kuzipeleka IPTL. Tunajiuliza kama ni ufisadi, ni ufisadi wa nini wakati fedha zile ni za IPTL?” alihoji Pinda.
Pinda alifafanua suala hilo lilipoandikwa kwa kirefu na gazeti dada la Mwananchi (The Citizen), CAG aliwasiliana na Katibu Mkuu wa Nishati, Gavana wa BoT na Mkurugenzi wa Tanesco ili kupata picha ya mchakato mzima.
“Wakati akiendelea hivyo, CAG akapata barua kutoka kwa Katibu Mkuu wa Nishati akimwomba afanye uchunguzi wa kina na wakati huo huo kamati ya PAC nayo ikamwelekeza kuchunguza jambo hilo.”
Waziri Mkuu aliongeza kusema: “Kwa tuhuma zenyewe zilivyo, itabidi tuwahusishe Takukuru nao wafanye kazi kwa upande wao ili kupata ukweli.
“Kwa maelezo na mtiririko ulivyo, kinachobaki ni tuhuma zinazojitokeza ambazo upo uwezo mkubwa wa vyombo hivi kuweza kuzibaini. Naliomba Bunge lako likubali CAG akubali kukamilisha kazi hiyo.”
Waziri Mkuu alisema wako viongozi wa Serikali ambao wametuhumiwa katika suala hilo hivyo ni vyema likachunguzwa kwa uzito wake ili wale watakaobainika wamekula rushwa washtakiwe.