Producer na CEO wa Bhitz Music Group, Hermy B ameandika barua ya wazi akielezea yaliyowahi kutokea Bhitz, uamuzi na mpango wao mpya.
Hivi ndivyo alivyoandika Hermy B:
Nikiwa kama CEO wa B’hitz Music Group na Producer ambaye napigana kama producers wengine kuusogeza muziki wa Tanzania katika level fulani, sikupendezwa kabisa na jinsi ambavyo baadhi ya watu walivyoizungumzia B’hitz na jinsi ambavyo baadhi yao wanaichukulia..
Kutokana na yote yaliyozungumzwa na baadhi ya wasanii ambao tulitofautiana nao kikazi, wengi wametuchukulia kama sisi ni wagomvi na wanyonyaji.
Lakini ukweli ni kwamba hakuna msanii ambaye alishatengeneza faida ya kifedha kwa B’hitz na wasanii hao walikuwa wakifanya kazi bila malipo yoyote na hata walipokuwa wakifanya shows tulikuwa tukiwaachia pesa kwa kuwa tulifahamu bado muda mzuri wa mavuno kulingana na ubinadamu, makubaliano na malengo, hivyo hakuna ukweli kuhusu hilo.
Hata hivyo, tumeyachulia yote yaliyotokea kama sehemu ya changamoto katika kazi hii ngumu ya muziki Tanzania ambayo kwa kiasi kikubwa watayarishaji wa muziki hawafaidiki nayo kama ilivyo kwa wasanii ambao wamejaliwa kuwa na ushawishi mkubwa zaidi kwa jamii na kuaminika mara moja kwa kile wanachokisema kuhusu sisi pale tunapotofautiana.
Kwa bahati mbaya, mipango tunayopanga nao tunapokuwa studio ama makubalinao mengi tunayoweka kwa ajili ya kazi zao hayajulikani kwa umma, na pindi wanapoyakiuka na kusababisha sisi kurudi nyuma tunaonekana wakosaji na wacheleweshaji wa maendeleo yao.
Naamini wasanii na sisi ndio tunaofahamu ukweli ni upi kati ya yote yaliyosemwa kupitia media kwa kuwa tunafahamu wapi tumetoka pamoja, tulikubaliana nini na wapi tulipotofautiana na yupi kati yetu aliacha reli ya makubaliano.
It’s a new chapter, na tunawatakia kila la kheri wasanii wote waliopita B’hitz na milango iko wazi kwa msanii yeyote wa Tanzania. Lengo letu ni kuendelea kuisupport jamii yenye vipaji kwa maendeleo ya taifa hili linalosifika kwa vipaji.
Nafasi ipo kwa wasanii wote walioondoka na kuacha kazi zao B’hitz, najua wanajua ni muziki mzuri na tusingependa kuona ukipotea au tukiutoa kwa kufuata ratiba tulizowekeana awali wakati ambapo wao hawapo.
Wasanii wanaweza kufuata nyimbo hizo na tutakuwa na makubaliano fair ili maisha ya muziki tulioutengeneza kwa ubunifu wa hali ya juu yaendelee na watanzania wafaidike kwa kuusikiliza.
Tunaamini uwezo wa Bhitz kuinua vipaji ambavyo havina majina makubwa na kuvifanya ‘brand’ ni baraka ambayo inabidi iendelee kwa vipaji vingine ambavyo bado havijajulikana na vina uwezo mkubwa.
Hivyo, tunapenda kuuarifu umma wa watanzania kuwa Bhitz imefungua ukurasa mpya na hatuendelei kuyashikilia tena matatizo yaliyokuwepo na wasanii hao.
Tunafurahi pia kuona muziki tuliotengeneza nao wakati tukiwa pamoja unawapa nafasi kubwa na kuwasogeza katika ngazi nyingine, tunaamini wanatoa shukurani zao kwa Mungu na zinatufikia kwa kiasi tunachostahili.
Tunaamini tutafika mbali na tumekomazwa zaidi na yaliyojiri kwa kuwa tumejifunza pia, yale ni mapito.
Music shall continue to live and flow in our bloods, we shall support Tanzanian music and musicians with all our hearts, We shall not give up because we are a part of this beautiful musical community in Tanzania.
Katika hatua nyingine, ningependa kuungana na producers wengine kuyatoa ya moyoni pia kuhusu kilio cha watayarishaji wa muziki Tanzania ambacho kimeendelea kuonekana kama kilio cha samaki. Huenda ni kutokana na idadi yetu ndogo kulinganisha na wasanii hivyo kilio chetu hakina sauti kubwa au ni mfumo mzima wa Industry ya Tanzania ulivyo mbaya na umezoeleka!
Producers wengi Tanzania tumekuwa tukitumiwa na baadhi ya wasanii kama daraja la mafanikio yao na kisha kutupaka matope au kuuambia umma kuwa sisi ndio tumewakosea sana na tunawanyonya.
Laiti kama wasanii hao wangekuwa wanaeleza angalau mazuri wanayofanyiwa na producers. Kwa bahati mbaya sifa wanazotumwagia tunapokuwa studio tunafanya kazi huishia studio na umma husikia tu wimbo mzuri ukiwa umetoka. Sifa zetu tunazopewa zimekuwa ‘perishable’ ingawa kazi tunayofanya huishi miaka yote na hutumiwa na msanii husika.
*Kwa mazoea ya soko la Tanzania, producers wengi huwa na moyo wa mshumaa na hata kuwatengenezea wasanii wetu midundo au nyimbo bure. Lakini wapo pia ambao huwalipisha wasanii kiasi cha fedha ambacho kwa uhalisia wa kazi na matunda ya kazi hii sio halali/sio fair bali ni bei zilizozoeleka tu.
Kwa uhalali wa ‘intellectual works’ wahusika wakuu huvuna matunda pamoja kwa kugawana asilimia kila wakati ambapo kazi hiyo itakapokuwa ikiingiza pesa. Lakini kwa Tanzania ni kama producer humuuzia haki miliki ya kazi nzima msanii kwa shilingi kadhaa au hata bure na kisha msanii kuingiza mamilioni kwa miaka mingi kwa kuuza au ku-perform kazi ile.
Hata kama ni kweli tasnia ya sanaa ya muziki kwa Tanzania bado inawanyonya wadau kwa ujumla, kati ya hao wanaonyonywa tumkumbuke producer ambaye yeye ananyonywa hadi damu ya mwisho na kisha kuchafuliwa pale anaponyoosha mikono yote kutaka mambo yaende sawa.
Hebu fikiria, kama kweli mgao wa matunda ya kazi yangekuwa sawa kwa asilimia kadhaa kwa kila kazi ambayo producer amefanya, producer kama P-Funk Majani angekuwa na maendeleo kiasi gani kutoka kwenye muziki pekee? Sisemi moja kwa moja kama aliofanya nao kazi walimnyonya, inawezekana alinyonywa na mfumo ulivyo.
Lakini ni wasanii wangapi tumeshawasikia wakitaja mafanikio makubwa waliyoyapata kwenye muziki kwa hits chache au hata hit moja tu. Je, umeshajiuliza producer wake alipata nini?
Je, ni producers wangapi ambao wametengeneza hits kibao zilizowapeleka wasanii mbali sana lakini wao wamebaki na hali ngumu kimaisha huku wakiendelea kunyonga midundo na kuambulia sifa za studio?
Uzalendo na moyo wa pekee tuliopewa usiokata tamaa kwenye muziki huu ndicho kitu pekee kinachotufanya tuendelee kuwekeza kwenye huu muziki na kuinua vipaji vipya na kuendeleza vilivyopo kwa imani kuwa ipo siku tutavuna matunda kwa kiasi tunachostahili.
Lakini kwa nini hiyo siku isiwe LEO? Itawezekana kama tutaungana na kuungwa mkono na wapenzi wa muziki mzuri.
Nisingependa kutaja majina ya producers wanaowalilia wasanii lakini karibia producers wote wamekuwa wakifanya hivyo na vilio vyao hupuuzwa tofauti na vilio vya wasanii.
Ndugu yangu Master Jay yeye amewahi hata kutoa kauli nzito kuwa wasanii ni wezi wanatuibia na wanatunyonya sisi maproducer. Alikazia kuwa wizi huu wa wasanii ni wa aina yake kwa kuwa huiba nguvu ya producers na kisha kujitangaza kuwa wameingiza kiasi kikubwa cha fedha kwa kazi ile ile.
Lamar amewahi kusema wasanii wanapokuja studio huwa wapole na kukubaliana mengi kuhusu wimbo lakini wimbo unapotoka na wao kufanikiwa huwasahau kabisa producers walioumiza nao kichwa mwanzoni na hata ‘kuwavimbia’. Lamar pia aliwahi kupata matatizo ya kimkataba na msanii wa Tanzania ambaye aliamua kusaini tena na Candy n Candy ya Kenya ili hali akiwa na mkataba mwingine.
Mikataba mingi tunayosaini nao mara nyingi huishia mikononi mwetu pale wanapovunja japo sheria ya mikataba iko wazi lakini kiuhalisia wasanii hao ni vigumu kulipa fidia itakayotajwa. Producer huamua kufunika kombe.
Producer Dupy yeye aliweka wazi kuwa sisi producers wa Tanzania ni masikini kulinganisha na wasanii ambao tunafanya nao kazi na kueleza ukweli kuwa hata wale wanaoonekana maisha yao ni mazuri ni wale ambao wanaingiza kipato kupitia shughuli nyingine tofauti na muziki.
Mimi pia ni mmoja kati ya producers ambao wanapata fedha kupitia shughuli nyingine na fedha hizo naziwekeza tena kwenye muziki kwa imani kuwa ipo siku mambo yatakuwa mazuri lakini mara nyingi wasanii unaopanga nao studio wanapopata mabawa (mafanikio) huruka na kueleza mabaya na sio mazuri mliyofanya nao yaliyowapa hayo mabawa.
Sisemi kuwa sisi hatuwakosei wasanii, tunakoseana kwa kuwa sisi pia ni binadamu japo sio kwa kiasi hicho wanachosema. Kukoseana katika kazi ni jambo la kawaida. Kukwaruzana wakati wa ujenzi ni kawaida pia.
Lakini kwa kuwa msanii huyo tayari ni brand, hasara kubwa huwa kwa producer ambaye inabidi aendelee kufanya kazi nyingine na watu wengine kwa kuanzisha upya malengo yake huku akiwa amemfaidisha tayari msanii huyo (Tayari ni brand).
Nyimbo tunazotengeneza nyingi studio tukisubiri msimu wa ‘mvua’ tuupush zinapobaki huwa hasara kwa producer kwani wao wanaweza kwenda kwa mwingine na wakazirudia. Je, producer anapata faida gani kwa kazi aliyoifanya tayari?
*Imefika wakati ambapo producer inabidi aheshimiwe kwa sababu bila yeye kusingekuwa na wasanii wengi wanaotamba hivi sasa. Hii itaongeza nguvu pia ya kazi kwa producers wapya nchini.
Producer alipwe vizuri kwa sababu anapolipwa vizuri na yeye ubunifu na utendaji wake wa kazi unakua kwa kiwango kikubwa. Pia atapata uwezo wa kununua vitendea kazi bora zaidi vitakavyomsaidia kuingiza muziki wetu kwenye ushindani wa soko la muziki Afrika na duniani kwa ujumla.
Naamini ipo siku hata haki za producer katika muziki alioutengeneza Tanzania zitazingatiwa ikiwa ni pamoja na kuvuna asilimia fulani ya muziki wake pale unapotumika kwenye miito ya simu, na biashara nyingine.
B’hitz Music Group, inavishukuru vyombo vyote vya habari Tanzania kwa support yao ikiwa ni pamoja na websites na blogs mbalimbali. Tuendelee kushirikiana.
This is the time! Sisi tunaendelea na kazi na tunawakaribisha wasanii wote.
Regards.
Hermes B. Joachim
poleni sana maproducer, ni kweli hawa jamaa wananyonywa sana...yaan ukiangalia master j pamoja na p funk walitakiwa wawe matajiri wa kutupa...but hata huwasikii...
ReplyDeleteinabidi mpambane jamani, hakuna mtu atawapigania haki zenu but ni nyie wenyewe.
Mikataba iwe endorsed kisheria mbele ya advocate ili mpate haki zenu na muache mikataba ya kupeana kishkaji kwani hii Ni biashara.
ReplyDelete