KOCHA mpya wa Taifa Stars, Mart Nooij jana Jumapili ameanza kuiongoza timu hiyo na kutoka suluhu na Malawi katika mchezo wa kirafiki maalumu kwa maandalizi ya mechi za kusaka tiketi ya kushiriki Kombe la Afrika 2015 dhidi ya Zimbabwe.
Katika mchezo huo uliochezwa Uwanja wa Sokoine mjini hapa, Nooij raia wa Uholanzi alianzisha kikosi kilichosheheni nyota wa timu za Ligi Kuu Bara huku akiwaweka benchi wachezaji wawili tu wa timu ya maboresho waliocheza dhidi ya Burundi hivi karibuni.
Baada ya mchezo huo, Nooij aliliambia Mwanaspoti kuwa: “Nimekaa na timu wiki moja tu, nimeridhika na kiwango walichoonyesha haya ni maandalizi mazuri dhidi ya Zimbabwe. Tutarekebisha makosa niliyoona leo ili tuifunge Zimbabwe.”
Kocha wa zamani wa Yanga ambaye sasa ni Kocha Msaidizi wa Malawi, Jack Chamangwana, alisema Taifa Stars imecheza vizuri na kama ikikomaa inaweza kufika mbali katika kufuzu Kombe la Afrika.
Kipindi cha kwanza Taifa Stars ilifanya mashambulizi kadhaa ikiwemo dakika ya 11 beki Aggrey Moris alipopiga kichwa kilichoshindwa kulenga lango na straika John Bocco dakika 36 alipiga shuti lililotoka nje kidogo ya lango la Malawi.
Kipindi cha pili dakika ya 52 kidogo Malawi ipate bao baada ya Rodrick Gonani kuwazidi maarifa mabeki wa Taifa Stars, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ na Moris na kupiga shuti kali lililopanguliwa na kipa Deo Munishi ‘Dida’. Taifa Stars itacheza na Zimbabwe kati ya 16 na 18 Mei mwaka huu jijini Dar es Salaam kabla ya kurudiana baada ya wiki mbili.