Mbeya City: Simba Imekula Kwenu

MBEYA City imewaambia Simba kwamba wamebugi kwa wanachokifanya kwa straika wao, Saad Kipanga na kwamba wao hawamuachii kwani wana mkataba naye.

Mchezaji huyo alizungumza na Mwanaspoti na kuihakikishia kwamba amezungumza kwa kina na matajiri wa Simba, lakini hajataka kuliweka bayana suala hilo kwa uongozi wa Mbeya City.

Mwanaspoti linajua kwamba Simba inafanya mambo yake kimyakimya na imejidhatiti kwamba lazima kijana huyo avae jezi nyekundu msimu ujao.

Mbeya City imefura na kumtaja Kipanga kwamba bado ana mkataba wa mwaka mmoja na nusu na kama Simba amewaeleza vinginevyo wamechemka. Katibu Mkuu wa Mbeya City, Emmanuel Kimbe, alisema kuwa uongozi wao bado haujapanga kuwauza wachezaji ingawa suala hilo linawezekana endapo pande zote mbili zitakutana na kukubaliana na si vinginevyo.

“Tumesikia, mchezaji tumemuuliza amekataa kuzungumza na viongozi wa Simba, ila ukweli anaujua yeye kikubwa ni kwamba hakuna mchezaji ambaye tumepanga kumuuza,” alisema Kimbe.

“Kipanga ana mkataba na sisi tena wa muda mrefu, hivyo kama Simba wanafanya mazungumzo na mchezaji huyo ni kosa, wanatakiwa kuja kuzungumza na viongozi ili wasikie sisi tunasemaje, huko ni kuwarubuni wachezaji.”

Alisema kuwa Simba wanafahamu kanuni zote za usajili ambazo wanatakiwa kuzifuata huku akisisitiza kuwa endapo Kipanga angebakiza mkataba wa miezi sita ilikuwa ni ruhusu kufanya naye mazungumzo.

“Sheria zipo wazi ambazo kila kiongozi wa soka anazifahamu, Kipanga tulimsajili wakati wa usajili wa dirisha dogo, wakiamua kuja ndipo tutajua cha kuwajibu zaidi na watajua mkataba wa mchezaji huyo umebaki wa muda gani, ila napo wanaweza kumkosa kwani hatuna mpango wa kumuuza kwa sasa,” alisema Kimbe.

Kiongozi Simba aonya

Mweka Hazina Msaidizi wa zamani wa Simba Humprey Laban, ameuonya uongozi wa klabu hiyo kwamba usithubutu kusajili wachezaji waliowahi kukipiga timu hiyo kisha kuhamia Yanga kwani endapo utafanya hivyo utakuwa unakaribisha hujuma.

Simba iko kwenye mazungumzo na kipa Ally Mustapha ‘Barthez’ aliyemaliza mkataba na Yanga. Laban alisema kwa uzoefu wake wachezaji waliowahi kuhama kutoka Simba kwenda Yanga kisha kurudi tena ndio wamekuwa wakihusika katika kufanya hujuma.

“Simba chonde chonde wachezaji waliohamia Yanga kutoka kwetu tusiwarudishe tena wengi wao ndio ambao wamekuwa wakihusika katika kutuhujumu, tatizo ni kwamba wachezaji wa namna hii wanakuwa na marafiki kutoka pande zote hivyo inakuwa rahisi sana wao kutumika kwenye michezo michafu naomba waachane nao kabisa,” alisema.
Tags

Post a Comment

1 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
  1. Deutoronomist6 May 2014 at 16:54

    Tetetetetete ngoja 2subr time will tell'

    ReplyDelete

Top Post Ad

Below Post Ad