Mnyika Aishukia Serikali Utoroshaji Fedha Nje ya Nchi

Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, imeilipua Serikali kwa kushindwa kudhibiti utoroshwaji mkubwa wa fedha kwenda nje.

Msemaji wa kambi hiyo, John Mnyika alisema katika kipindi cha miaka 39 kuanzia 1970 hadi 2008, Sh9.6 trilioni zilitoroshwa kiharamu kwenda nje.

“Utoroshaji wa fedha hizi unasadikiwa kutokana na ukwepaji wa kodi, na misamaha mikubwa ya kodi,” alisema Mnyika na kuongeza; “Fedha nyingine zilitokana na usiri mkubwa wa mikataba baina ya wawekezaji na Serikali, upotoshaji wa bei katika biashara na rushwa katika mikataba na wawekezaji” alisema.

Mnyika alisema Serikali ya CCM haiwezi kukwepa kuwajibika kwa sababu utoroshaji wa mapesa yote haya umefanyika wakati na CCM ipo madarakani, ” alisema.

Mnyika alifafanua, utoroshaji huo wa fedha ulifanyika kwa mafungu na kutolea mfano mwaka 1980, Dola 570. 6 milioni zilitoroshwa.

Fedha hizo zilitoroshwa wakati hayati baba wa Taifa mwalimu Jullius Nyerere akiwa madarakani na dola 1,566 milioni zikatoroshwa 1985 wakati wa Rais Ali Hassan Mwinyi.

“Jambo la kusikitisha zaidi mwaka 2002 zilitoroshwa jumla ya Dola za Marekani 1,1010 milioni katika kipindi ambacho Rais Benjamin Mkapa yuko madarakani,” alisema Mnyika.

Mnyika alisema kambi hiyo imesikitishwa na kitendo cha Bunge kushindwa kuisimamia kikamilifu Serikali hususan Wizara ya Nishati na Madini.

Alisema fedha zote zilizotoroshwa nchini tangu mwaka 1970 mpaka 2008 zinaweza kurejeshwa nchini kwa kuanzia na kuzibaini zilipo.

“Uchunguzi wa kina ufanyike kuzuia fedha hizo katika akaunti za benki zilipotunzwa nje ya nchi na hatimaye kurejesha fedha hizo nchini,” alisema.

Kitengo cha Financial Intelligence Unit (FIU) cha Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kimetakiwa kukusanya taarifa za kiintelijensia na kuziwasilisha Takukuru ili uchunguzi ufanyike.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad