MSHAMBULIAJI wa Yanga, Mrisho Ngassa amesikia taarifa za kuondoka kwa Didier Kavumbagu na Frank Domayo akatamka: “Aisee hilo ni pigo kubwa kwa kikosi chetu naomba niwe muwazi.”
Akizungumza na Mwanaspoti kutoka Mwanza anakouguza majeraha ya nyama za paja, Ngassa alisema amepokea taarifa za kuondoka kwa Kavumbagu na Domayo kwa masikitiko na kuongeza wachezaji hao walikuwa wakihitajika katika kikosi chao.
Ngassa alisema maumivu zaidi yanakuja kutokana na ukweli kwamba wachezaji wote walikuwa katika kikosi cha kwanza cha Yanga, ambapo sasa uongozi unatakiwa kutuliza akili kutafuta mbadala wa nyota hao walioondoka wakiwa wachezaji huru baada ya kumaliza mikataba.
“Tuseme kweli kwamba kuondoka kwa Didier na Domayo ni pengo kwa timu, hili lipo wazi kwani walikuwa wachezaji muhimu katika timu yetu, walicheza mechi nyingi ambazo ni muhimu, ni wakati wa viongozi kufanya kazi yao ipasavyo kuhakikisha wanatafuta wachezaji wengine mahiri ili kuziba nafasi zao,”alisema Ngassa ambaye amewahi kucheza Azam na Simba.