Mume wa Mwimbaji Nguli wa Injili adaiwa Kumbaka Shemejiye

 Mume wa mwimbaji maarufu wa nyimbo za Injili, (jina tunalihifadhi kwa sasa), anatuhumiwa kumbaka shemeji yake mdogo (17).

Taarifa za tukio hilo ziliripotiwa juzi saa 12 jioni katika Kituo cha Polisi Tabata (Tabata Shule), zikimtuhumu mwanamume huyo kwamba alimbaka binti huyo mara tatu na kumsababishia maumivu makali.

Binti huyo alifika katika kituo hicho cha polisi akiwa na ndugu zake wawili ambao walilalamika kwamba kulikuwa na jitihada kubwa kutoka upande wa mtuhumiwa wa kuzima kesi hiyo.

Akizungumza na gazeti hili nje ya kituo hicho, binti huyo alisema shemejiye alimbaka mara ya kwanza, Ijumaa iliyopita na Jumapili alipombaka mara mbili ndani ya gari.

Alisema mara ya kwanza alikaa kimya baada ya mtuhumiwa kumtishia kwamba angemdhuru kama angetoa taarifa ya tukio hilo alilofanyiwa wakiwa sebuleni nyumbani kwako Tabata Kimanga, lakini aliamua kutoa taarifa kwa ndugu zake baada ya kubakwa mara ya pili.

Polisi katika kituo hicho walithibitisha kupokea taarifa za tukio hilo lakini walishindwa kwenda kumkamata mtuhumiwa kwa maelezo kwamba hawakuwa na askari wa kutosha na kuahidi kwamba angekamatwa jana. Hata hivyo, hadi jana mtuhumiwa huyo alikuwa hajakamatwa.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Marietha Minangi kutwa nzima ya jana hakupatikana kuzungumzia tukio hilo na kila simu yake ilipopigwa (kati ya saa nane mchana na saa mbili usiku), ilipokewa na msaidizi wake akisema bosi wake ana kazi nyingine.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova alisema hakuwa amepokea taarifa yoyote ya aina hiyo.

Mwimbaji anena

Alipoulizwa jana, mwimbaji huyo alisema kwa sasa hawezi kuzungumzia kwa undani tuhuma zinazomkabili mumewe na kwamba alikuwa anajisikia vibaya kutokana na tukio hilo kuhusisha watu wake wa karibu.

“Of course (bila shaka), hili sio tukio zuri. Kwa sasa sina uwezo wa kuzungumza kwa sababu hili suala lipo Polisi. I am confused (nimechanganyikiwa), ukizingatia kwamba linasemekana kutokea wakati sikuwepo nyumbani, naomba tuzungumze baada ya akili kutulia,” alisema.

Kadhalika, jana saa 6:20 mchana, gazeti hili lilifanikiwa kuzungumza na mtuhumiwa ambaye baada ya kupewa maelezo kuhusu tuhuma zinazomkabili alisema: “Samahani sana ujue sikusikii kabisa,” kisha alikata simu.

Gazeti hili lilimpigia tena simu lakini ilikatwa na baada ya hapo kila alipopigiwa haikupokewa. Baadaye saa 6:35 mchana, mtu aliyejitambulisha kuwa ni mdogo wa mtuhumiwa alipiga simu chumba cha habari akitaka kuonana na mhariri wa gazeti hili, kwa maelezo kwamba alipewa namba husika na kaka yake.

“Samahani, mimi (anataja ina) niko hapa nje Ofisi za Mwananchi, nilifika hapa kutaka kuonana na mhariri maana nasikia mwandishi wenu alikuwepo polisi tangu jana kwenye tatizo lililompata kaka yangu, sasa wakati nasubiri kuonana na mhariri kaka amenipigia simu akisema namba hii imempigia, kwa hiyo naomba tuonane ili tuzungumze tuone jinsi ya kumsaidia,” alisema.

Baada ya kuonana na mwandishi wa habari wa gazeti hili, alisema suala hilo lilikuwa likijadiliwa katika ngazi ya familia, hivyo wasingependa liandikwe kwenye vyombo vya habari.

Vipimo vya hospitali

Juzi, baada ya tukio hilo kuripotiwa, mtoto huyo alipelekwa katika Hospitali ya Amana ambako alifunguliwa faili la matibabu na kupewa namba ya usajili 667. Aliingia chumba cha matibabu namba 21 kumuona daktari kwa ajili ya vipimo zaidi.

Matokeo ya vipimo yalionyesha kuwa binti huyo alikuwa amefanya ngono kwa nguvu. Katika fomu hiyo ya uchunguzi, daktari aliandika ‘High vagina swab’.

Baada ya vipimo, familia ilirudi katika Kituo cha Polisi kupeleka matokeo ya vipimo vya daktari, hivyo kufungua faili la kesi lililopewa namba RB TBT/RB/319/2014 na namba TBT/IR/1865/2014. Jana binti huyo alikwenda tena Amana ambako alifanyiwa vipimo vilivyobaki vya VVU na mimba. Vipimo vya awali vya VVU vilionyesha kuwa hakuwa ameathirika na hakupata ujauzito.

Mtoto alipo

Habari ambazo zililifikia gazeti hili jana jioni, zilisema mtoto aliyebakwa alichukuliwa na familia ya Mchungaji Josephat Gwajima.

Gazeti hili lilifanya jitihada za kumtafuta Mchungaji Gwajima bila mafanikio, lakini lilimpata mkewe, Grace ambaye hakuwa tayari kuthibitisha kuwapo au kutokuwapo kwa mtoto huyo nyumbani kwake.

“Naomba nisiwe msemaji katika jambo hilo, yupo msemaji mwenyewe ambaye naamini mnamfahamu naye ni Mchungaji Gwajima, kwa hiyo mtafuteni, yeye atasema kama mtoto yupo hapa au hayupo na kama yupo sababu zake ni zipi,” alisema Grace.

Alipoombwa atoe mawasiliano ya simu ya mchungaji huyo, Grace alisema: “Kwa kweli kama unaweza, kesho nenda pale Kanisani Kawe utapewa utaratibu wa kuonana naye.”

Post a Comment

1 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
  1. Yesu na mokozi kweli! Kweli wanamfanya huyu Yesu atukanwe Mmmmh!!! Labda Si kweli jamani!!! Uwiiiii!

    ReplyDelete

Top Post Ad

Below Post Ad