Ngorongoro Heroes Yapigwa Kipigo cha Mbwa Mwizi

TIMU ya taifa ya soka ya vijana wa chini ya miaka 20, Ngorongoro Heroes, jana walianza vibaya kampeni ya kuwania kufuzu kwa Fainali za Afrika kwa umri huo baada ya kukubali kipigo cha mabao 2-0 kutoka kwa Nigeria kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Mchezo ulianza kwa kasi huku wageni wakionekana kujiamini, ingawa iliwachukua dakika tano tu Ngorongoro kulifikia lango la Nigeria ‘Flying Eagles’, ambapo Saad Kipanga alikosa bao akishindwa kumalizia kazi ya Kelvin Friday aliyemimina krosi toka winga ya kulia.

Dakika ya 11, mlinda mlango wa Ngorongoro, Aishi Manula, alifanya kazi ya ziada kuhakikisha nyavu zake hazitikiswi, ambapo alimzuia Mathew Ifeanyi, tukio ambalo lilimsababishia kuumia na kulazimka kutibiwa mara tatu katika dakika 45 za kwanza.

Kupitia shambulizi hilo, Manula alikuwa katika hatari ya kufungwa ama kusababisha penalti kama angemkabili vibaya Ifeanyi, lakini kwa ustadi mkubwa alilala kwa umakini na kuokoa hatari, ambayo ilimfanya aendelee kucheza na maumivu kabla ya kutolewa wakati wa mapumziko.

Hadi filimbi ya mapumziko ya mwamuzi Jean Ndala Ngabo wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), si Ngorongoro Heroes wala Flying Eagles iliyofumania nyavu za mwenzake.

Kipindi cha pili kilianza kwa Ngorongoro kufanya mabadiliko mawili kwa kuwatoa Aishi Manula na nafasi yake kuchukuliwa na Manyika Peter, na Gadiel Michael ambaye nafasi yake ilijazwa na Juma Liuzio. Nigeria nao wakafanya mabadiliko kwa kumtoa Abdullahi Alhassan na kumuingiza Iheanacho Promise.

Katika dakika ya 49, Flying Eagles walijipatia bao la kwanza, likiwekwa kimiani kirahisi kwa shuti dhaifu la karibu la Yahaya Musa, akiunganisha krosi maridadi ya Mohammed Mussa.

Kuingia kwa bao hilo kuliwachanganya Ngorongoro, ambao walijikuta wakishambuliwa mfululizo na kama si umakini wa Manyika Peter langoni, wangeweza kufungwa bao la pili, lakini yoso huyo anayefuata nyayo za baba yake Peter Manyika, aliokoa mchomo wa mbali na kuwa kona tasa dakika ya 54.

Saad Kipanga aliikosesha Ngorongoro bao la kusawazisha katika dakika ya 60, baada ya kumiminiwa majalo safi na Friday, lakini kichwa chake kikapaa juu ya lango la Flying Eagles.

Dakika ya 82, Awoniyi Taiwo aliipatia Nigeria bao la pili kwa shuti la karibu na kuzima matumaini ya Ngorongoro. Kwa matokeo hayo, Tanzania itahitaji ushindi wa mabao 3-0 ugenini ili kusonga mbele.

Ngorongoro: Aishi Manula/Manyika Peter, Swalehe Mohamed/Mohamed Ibrahim, Mohamed Hussein, Pato Ngonyani, Abdullahi Kheri, Abdi Banda, Ally Nassoro, Kelvin Friday, Saad Kipanga, Idd Selemani na Gadiel Michael/Juma Liuzio.

Nigeria: Enaholo Joshua, Muhamed Mussa, Mustapha Abdullahi, Idowu Akinjide, Ndidi Onyinye, Omego Izuchukwu, Alfa Abdullahi, Abdullahi Alhassan/Iheanacho Promise, Awoniyi Taiwo, Mathew Ifeanyi na Yahaya Mussa/Nwakali Chidiebere.
Tags

Post a Comment

1 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
  1. Bao 3?halafu kuwafunga kwao ni ndoto.

    ReplyDelete

Top Post Ad

Below Post Ad