Simba Msipokuwa Makini, Mtalia miaka Minne

MAANDALIZI ya Uchaguzi Mkuu wa Simba sasa yameshika kasi huku wagombea 41 wakiwa wamechukua na kurudisha fomu za kuwania uongozi kwa ngazi mbalimbali. Uchaguzi huo utafanyika Juni 29.

Uchaguzi huo unafanyika baada ya kupita miaka minne tangu ule wa mwisho ulipofanyika na kuuingiza madarakani kwa mbwembwe uongozi wa Ismail Aden Rage ambao sasa unamaliza muda wake bila ya kukidhi matarajio ya wanachama.

Kwa miaka mitatu mfululizo sasa, Simba haijatwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara huku uwezo wa kikosi chake wakati mwingine ukitiliwa shaka kwani wachezaji wanaonekana kucheza kwa kufuata maelekezo mengine nje ya yale ya kocha.

Hata katika masuala mengine ya maendeleo ya klabu, Simba imeendelea kuwa na mambo yale yale yaliyojaa ubabaishaji.

Hilo ndilo soka la Tanzania, utegemezi wa klabu unakuwa shubiri wakati mwingine, tena katika wakati muhimu ambao timu inahitaji pointi za kutwaa ubingwa pengine.

Siku zote chaguzi za klabu kongwe za Simba na hata Yanga, hutawaliwa na makundi. Katika Simba inaelezwa kuna itikadi kali za makundi hayo yanayotajwa kuwa mawili. Inaelezwa kuwa ndani ya klabu hiyo, kundi moja likishinda basi jingine hujiweka kando na kutazama washindi wanafanya kitu gani.

Mbaya zaidi wakati Simba ikiwa katika mchakato wa uchaguzi, kuna kamati ya siri imeundwa ili kufanya usajili wa msimu ujao wa Ligi Kuu Bara. Usajili huo unafanyika kwa mikakati binafsi zaidi hasa katika utoaji fedha.

Hii inamaanisha kama Simba ilikuwa na tatizo la wachezaji kucheza chini ya kiwango kwa makusudi wakifuata maelekezo ya kiongozi fulani, basi hali hiyo bado itaendelea.

Kuna mfano wa kiongozi mmoja aliyekuwa akijitolea kuisaidia timu hiyo kwa kufanya usajili na kuiweka timu kambini kisha anajirudishia fedha zake kupitia mapato ya mechi za timu.

Alinogewa hadi akaingia katika uongozi, lakini akasahau kutimiza wajibu wa kuiwezesha klabu kuwa na mbinu zake za kupata fedha, pale wanachama walipobaini kuigeuza klabu mtaji, hakuwa na namna ikabidi atoke.

Simba haihitaji kuongozwa na mtu anayetaka yeye jinsi ya kuiendesha, inapaswa kuwa na uongozi wenye mipango ya maendeleo isiyo tegemezi kwa mtu au taasisi yoyote.

Hata siku moja wanajiita ‘wajanja wa mjini’ hawataweza kuisaidia klabu hiyo yenye rekodi ya pekee Tanzania na Afrika Mashariki. Viongozi wa aina hiyo wamekuwa wakiwapa kazi makocha asubuhi, jioni wanawafukuza.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad