NAFASI mpya ya Rais wa Simba (zamani Mwenyekiti) ina watu wawili ambao ni Evans Aveva anayepewa nafasi kubwa ya kuibuka kidedea na mpinzani wake mkubwa ni Michael Wambura, Mwanaspoti limebaini.
Wambura alikiri kuwa ana harakati za kugombea lakini jana Jumatano alisema: "Sitaki kuzungumza sana, lakini katika hilo ningependa niseme kwamba sifa ya kwanza ya mwanachama wa Simba ni kuisaidia timu yake pale anapoweza.
Muda bado, naomba tusubiri tuone nini nitaamua, nitatangaza katika muda wa siku mbili kutoka sasa."
Aveva anapewa nafasi kubwa kutokana na kuonekana ndiye mtu muafaka katika nafasi hiyo baada ya kupitishwa na kundi lenye nguvu ya fedha katika klabu hiyo la Friends of Simba huku Wambura akionekana kuwa na mvuto wa kiasi chake.
Lakini pia inaelezwa kuwa yeye ndiye chaguo la kigogo mmoja mzito wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
Nafasi ya Makamu wa Rais ambayo awali ilikuwa ikitambulika kama Makamu Mwenyekiti hapa ndiyo kunaonekana kuwa na vita ambapo wagombea wanaopewa nafasi na watakaochukua fomu na kutoa upinzani wa kweli ni Sued Nkwabi, huku Mwina Kaduguda naye akitajwa wakati Ayoub Semvua naye akichomoza huku wote wakiwa msituni wakijipanga na mtifuano huo.
Alipotafutwa Nkwabi alisema: "Nitatangaza hilo rasmi hivi karibuni, tusubiri kwanza kupata taarifa kamili za kamati ya uchaguzi na baada ya hapo nitatoa tamko langu."
Mtihani mkubwa upo katika nafasi za wajumbe watano ambapo mpaka sasa wapo watu watano wanaopewa nafasi, nao ni Said Tuli, Juma Pinto, Patrick Rweyemamu, Rodney Chiduo na Collins Frish ambaye aliwahi kuwa Katibu wa kwanza wa kundi la Friends of Simba.
Mtihani zaidi katika wagombea hao wanaotajwa ni kwamba idadi yao ni watano lakini hapo wanatakiwa wanne tu kuingia katika uongozi mpya wa Simba ambapo nafasi moja itakayofanya watimie watano inatakiwa kujazwa na mjumbe wa kike ambaye bado hawajaanza kuonekana ingawa msemaji wa Simba, Asha Muhaji, anatajwa kuwa mbioni kuiwania.