Usajili Yanga: Kaseja Njia Panda


Hatma ya kipa Juma Kaseja, kuendelea kuichezea Yanga ipo mikononi mwa mashabiki wa klabu hiyo kutokana na mapendekezo ya benchi la ufundi yaliyowasilishwa kwa viongozi wa timu hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka ndani ya klabu hiyo zimesema kuwa kocha aliyemaliza muda wake, Hans Van Pluijm, alimpendekeza kipa huyo katika makundi mawili, la kuachwa (kutolewa kwa mkopo) na lile la kubaki kuichezea timu hiyo ndapo mashabiki wataonyesha tabia chanya kwake.

Chanzo chetu cha kuaminika kilisema Pluijm, ambaye kwa sasa ametimkia Saudi Arabia, alisema Kaseja ni kipa mzuri, lakini mashabiki wa klabu hiyo hawaonyeshi ‘kumkubali’, jambo ambalo liliwaweka katika hali ngumu kumchezesha.

Pluijm alisema uwezo wa kipa huyo ndiyo unaowafanya benchi la ufundi ‘kufikiria’ mara mbili hatma yake na hasa ikizingatiwa kuwa kipa Ali Mustafa ‘Barthez’ amemaliza mkataba wake na ametangaza kurejea klabu yake ya zamani, Simba. Ugumu wa suala la Kaseja pia unatokana na ukweli kuwa Yanga haina kipa mwingine zaidi ya Deogratius Munishi ‘Dida’, ambaye ndiye chaguo la kwanza kwa klabu hiyo.

Pia, suala la kuvunja mkataba kwa Kaseja ni gumu kutokana na Yanga kuogopa kulipa fedha nyingi, na mpango uliopo ni kumtoa kipa huyo kwa mkopo kwa timu nyingine za Ligi Kuu ya Tanzania Bara.

“Suala la Kaseja ni gumu, linahitaji uangalifu mkubwa na zaidi katika masuala ya mkataba na hali halisi ya Yanga, kipa anayetegemewa sasa ni Dida (Munishi), Barthez (Ali Mustafa) anarejea Simba, nani atakuwa msaidizi wa Dida, suala hilo ni gumu kutolea uamuzi na ndiyo maana Pluijm ameacha mtego huo,” kilisema chanzo chetu.

Naye kocha msaidizi wa Yanga, Charles Mkwasa ‘Master’, alisema wao wamependekeza kusajiliwa kwa kipa mmoja, lakini hawajui nani atakayeondolewa kati ya hao watatu.

“Kwa suala la kipa naweza kusema tumependekeza kipa mmoja mpya, na hii inatokana na ukweli kuwa hatuwezi kutegemea kipa mmoja msaidizi wa vijana (U-20), hivyo hatujui nani atasajiliwa kwani hata kama Barthez amemaliza mkataba wake, uongozi unaweza kumsajili kwa kuongeza mkataba…, lakini hiyo ni mipango ya uongozi, sisi tunasubiri mapendekezo yao ya mwisho,” alisema Mkwasa.

Wakati hayo yakiendelea, Kaseja alisema kuwa yeye bado ni mchezaji wa Yanga na kutokana na mkataba wake kama kuna taarifa za kumuacha au kumtoa kwa mkopo atazipata kutoka kwa uongozi wa klabu hiyo.

Kaseja alisema ana mkataba ambao anauamini na kamwe hawezi kufanyia kazi taarifa za kwenye magazeti kwani kuna njia ya mawasiliano ndani ya Yanga.

“Mimi nasubiri uongozi uniambie, kama naendelea au la, lakini kwa sasa mimi bado mchezaji wa Yanga mwenye mkataba halali ambao ninauheshimu, hayo maneno ya yakiwekwa katika maandishi na uongozi wa Yanga, ndiyo nitajua hatma yangu, kwa sasa hapana, naheshimu mkataba,” alisema.

Katibu Mkuu wa Yanga, Beno Njovu hakuweza kupatikana kuzungumzia suala hilo kwa kutojibu simu yake baada ya kupigiwa.
Tags

Post a Comment

3 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
  1. kaseja muuza match

    ReplyDelete
  2. kaseja atumtaki uwezo wa kudaka umeisha

    ReplyDelete
  3. Hee! Ataenda wap sasa?

    ReplyDelete

Top Post Ad

Below Post Ad