USHINDI WA NGORONGORO HEROES NI KAMA ZALI LA METANTALI

TIMU ya Taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 20 ‘Ngorongoro Heroes’ juzi Jumapili ilivuka hatua ya awali ya mechi za kufuzu Kombe la Mataifa ya Afrika kwa vijana lakini timu hiyo haikubahatika kufunga bao hata la kuotea kwenye mechi mbili ilizocheza na Kenya.

Ngorongoro Heroes na Kenya zilitoka suluhu mjini Nairobi wiki chache zilizopita kabla ya kutoka sare ya aina hiyo hiyo kwenye mechi ya marudiano Jijini Dar es Salam. Ngorongoro ilishinda kwa penati 4-3 na kufuzu kwenye hatua inayofuata na ratiba inaonyesha kuwa itavaana na Nigeria katika hatua hiyo ya pili.

Akizungumzia ubutu unaoikabili timu hiyo, Kocha John Simkoko aliliomba Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuitafutia timu hiyo mechi nyingi za kirafiki ili iweze kujiandaa vizuri kabla ya mechi ya marudiano na kuwatengenezea vijana hao hali ya kujiamini pindi wanapofika kwenye eneo la hatari la timu pinzani na kuweza kufunga.

Kwa upande wake, Kocha wa zamani wa Azam FC, Stewart Hall aliyekwepo pia kwenye benchi la Ngorongoro Heroes alisema kuwa tatizo la ushambuliaji limekua sugu hapa nchini hivyo kuwataka waalimu na wakufunzi wa michezo kuanzisha program mbalimbali zitakazosaidia kutatua tatizo hilo.

“Ushambuliaji ni tatizo kubwa katika medani ya soka hususani hapa nchini Tanzania, ni vyema walimu wakalitazama hili kwa jicho la pili ili kuweza kulitatua,” alisema Hall anayefanya kazi kwenye Mradi wa Symbion unaohusika zaidi na soka la vijana hapa nchini chini ya usimamizi wa klabu ya Sunderland inayoshiriki ligi kuu ya Uingereza.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad