Kuna kila dalili mkoa wa Dar es Salaam kuporomoka kiuchumi na hivyo kushusha kiwango cha pato la taifa endapo hakutakuwa na jitihada za dhati kwa Jeshi la polisi na serikali kwa ujumla kukabiliana na makundi ya wahuni jijini humo maarufu kama ‘Panya Road’ na ‘Watoto wa Mbwa au Mbwa Mwitu’.
Uchunguzi wa kina uliofanywa sehemu mbalimbali za jiji hilo umebainisha kwamba, hivi sasa wafanyabiashara na wananchi wa kawaida wanaishi kwa hofu kubwa wakihofia vijana hao ambao umaarufu wao umekuwa ukizidi kukuwa na kushika kasi kila kukicha.
Kwa nyakati tofauti, mwandishi wa Times Fm alizunguka maeneo mbalimbali ya jiji hilo hasa maeneo ambayo yameathirika zaidi na uwepo wa Panya Road na Watoto wa Mbwa.
Uchunguzi unaonyesha asilimia kubwa ya wananchi waliozungumza na Times Fm walieleza kuwa wanaishi bila amani waliyokuwa nayo awali.
“Hivi sasa kaka jiji limechafuka sana na hawa watoto (Panya Road na Watoto wa Mbwa) hatuna hata amani ingawa polisi wanasema hali shwari lakini kiukweli hali bado ni tete…..jana tu kuna jamaa ameporwa pikipiki yake pamoja na kujeruhiwa tena mbele za watu….kwa kifupi bado hawa watoto hawajadhibitiwa,” Amesema Amina, mfanyabiashara wa kuuza vocha na kadi za simu eneo la Kigogo Mbuyuni .
Amina amesema tukio hilo lilisababisha kuuwawa kwa Panya Road mmoja na baadae kuzikwa eneo la Kigogo ambapo mara baada ya maziko hayo vijana ha wahuni waliingia mitaani na kuanza kufanya vurugu kubwa ikiwa ni pamoja na kupora na kujeruhi katika kile kilichoelezwa ni kulipiza kisasi baada ya kuuwawa kwa mwenzao.
“Nilishuhudia kwa jicho langu kuna mama alikuwa amepaki gari yake barabarani ambapo vijana walimvamia na kuvunja vioo vyake na kumtoa nje ya gari ambapo walimpiga na kumpora kila alichokuwa nacho! Baada ya hapo waliwavamia wakaanga chipsi na kuvunja mayai yao wakapora pesa na kuingia mitini.” Amina amesimulia.
Amina ambaye ingawa alikuwa anaongea hayo mbele ya kundi kubwa la watu, alionekana kuwa na hofu kubwa kutokana na kuwahofia vijana hao ambao inaelezwa ni zaidi ya watukutu.
Khamisi Mohamed Mkumbi mkazi wa eneo hilo hilo la Kigogo, anasema Panya Road ni vijana walioshindikana majumbani kwao na wapo tayari kwa lolote kwa sasa katika kile kinachoelezwa ni kutokuwepo kwa dhamira ya dhati katika kuwamaliza.
“Serikali inanguvu kuliko kitu chochote hapa nchini mimi naamini kama kutakuwa na dhamira ya dhati inaweza kuwamaliza vijana hawa na kuwa historia lakini kwa sasa naona kabisa serikali haijaamua kuwamaliza vijana hawa na wananchi tunaendelea kuishi bila amani,” Amesema.
Mkazi mwingine wa eneo hilo, aliyejitambulisha kwa jina la Mchaji Halisi, alisema panya road kwa kiasi kikubwa wamevuruga uchumi wa eneo hilo kutokana na wafanyabiashara muda mwingi kufunga maduka yao kwa hofu ya kuwavamiwa na kuporwa mali zao.
“Wao wakivamia dukani kwako mbali na kukupiga kwa mapanga ama visu, pia wanachukuwa kila wanachoona kinastahili kuwachukuliwa….wanaweza kuchukuwa unga, mikate, sabuni, pakta za sigara na vitu vingine yaani kwa kifupi wao hawaangalii nini kinawafaa chochote tu wao wanachukuwa.”
Mwenyekiti serikali za mitaa Kigogo Mbuyuni Bw. Mohamed Mnunga akizungumza na times fm, alisema serikali yake imejipanga kumaliza tatizo la panya road kwa wananchi wake ingawa alikiri kuwepo na kuleta madhara makubwa kwa wakazi wa eneo lake.
“Hawa vijana wapo sikatai na kiukweli wamewaathiri sana wananchi wangu na tunajitahidi sana kwa kushirikiana na jeshi la polisi kumaliza uwepo wao,” anasema.
Bw. Mnunga alienda mbali na kusema kwamba uwepo wa panya road mitaani hasa katika eneo lake limechangia kwa kiasi kikubwa kushuka kwa uchumi kwa wananchi wake kutokaa na wananchi wengi kuwahofia na kushindwa kufanya shughuli zao za kila siku.
Kwa upande wa eneo la Kinyerezi, huko napo hali ni tete kwa wananchi kuishi kwa mashaka kutokana na taarifa kwamba siku ya Jumanne walivamia maeneo hayo na kusababisha taharuki kubwa kwa wakazi wa Ulongoni Gongo la Mboto na Kinyerezi.
Mjumbe wa serikali za mitaa Kinyerezi ambaye alizungumza na times fm, Christina Lwiza, alisema eneo lake ni kati ya maeneo yaliyoathirika kwa kiasi kikubwa na vijana wa panya road na kumekuwa na hofu za mara kwa mara toka kwa wananchi na wafanyabiashara kiasi cha wengine kufunga maduka yao kwa kuogopa kuvamiwa!
Times Fm ilizungumza na Makamanda wa polisi mikoa ya Kipolisi Ilala na Temeke, ambapo kwa nyakati tofauti kila mmoja alijinasibu kwamba mkoa wake upo sawa na hakuna matukio hayo na kwamba zilizobaki sasa mitaani ni taarifa za uongo unaoenezwa na watu wasiopenda amani.
Anglibert Kiondo ni Kamanda wa Polisi Temeke, kwa upande wake alisema mkoa wake wa Temeke upo shwari na vijana wengi wanaofanya uporaji wanatokea maeneo ya Ilala, Magomeni na sehemu nyingine.
“Mimi mkoa wangu kiukweli upo salama na wananchi wangu wanaendelea nakazi zao kama kawaida, hao vijana wanaojiita Watoto wa Mbwa ana Panya Road hao ni wala unga tu hao ambao kwangu nimekabiliana nao na sasa hawapo kabisa wapo huko Magomeni na Ilala,” alisema RPC Kiondo.
Kwa upande wa RPC Ilala, Mariatha Minangi, alisema Panya Road katika mkoa wake hawapo na kwamba amepambana nao ipasavyo.
“Kwangu mimi hakuna kabisa hao wanaojiita Panya Road ninachoweza kuwema sasa waliokuwepo sasa ni watu tu wanauzusha uwepo wao lakini kiukweli ndani ya mkoa wangu kwasasa ni salama na wananchi wanaendelea na shughuli zao kama kawaida,” Alisema.
Kwa bahati mbaya Kamanda wa polisi mkoa wa Kinondoni hakupatikana kwenye simu yake kuelezea kwa upande wake amepambana vipi na makundi hayo ya kiharifu.
Aidha, Kamishina Msaidizi wa polisi (Kamanda Kanda Maalum ya Dar es Salaam), Suleiman Kova, akizungumza na times fm alisema jeshi lake limejipanga kila kona ya jiji katika kuhakikisha panya road hawapati nafasi ya kuendelea kuleta hofu kwa wananchi.
“Mimi nipo na vikosi vyangu vipo bado haujashindwa kazi hawa wanaojiita panya road wote watakwisha na labda nikuhakikishie mwandishi kwa sasa hawa vijana hawapo isipokuwa kuna watu ambao wapo kazi yao ni kueneza taarifa za uongo kwa wananchi na tunajipanga kuwakamata ha wanaotoa hofu na nitakapozungumza na waandishi wahabai tena nitakuwa na orodha kamili ya watu waliokamatwa,” alisema Kova.
Jitihada za kumtafuta Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Mecky Sadiq ili kupata taarifa kwa upande wake kuhusiana na taarifa hizi hazikuweza kuzaa matunda kutokana na taarifa tulizozipata ni kwamba alikuwa msibani hivyo asingeweza kuzungumzia tukio hili.
Kova chonde chonde kamata pants road,kova chonde chonde kamata panya road kova chonde chonde kamata panya road, kova chonde chance kamata panya road
ReplyDelete