Ilikuwa ni safari ya kawaida ambayo ilitarajiwa kuwapa faraja watoto. Lakini hali imekuwa tofauti baada ya matarajio hayo kugeuka majonzi kwa mtaa mzima kutokana na kuondokewa na watoto watatu kwa wakati mmoja.
Ni mara chache sana watoto hutoka pamoja kwenda mbali kufurahia na wenzao. Hivyo Janet, Ndimbumi na Eva waliamini kuwa siku hiyo ingewapa furaha na pengine hadithi za kwenda kusimulia shuleni, lakini haikutokea kama walivyotarajia; simulizi zikawa tofauti.
“Tulistuka kuuona mwili wa Janeth ukiwa unaelea juu ya maji,” anasema kaka yake, Goodluck Kihoko (14) ambaye siku hiyo alienda pamoja na watoto wengine 20 kwenye Hoteli ya Landmark iliyo Mbezi Beach, jijini Dar es salaam.
“Tuliwaita walinzi, lakini wakapuuza. Tuliwaita walinzi kwa muda mrefu ndipo wakafika na wakati huo mama na wale vijana walikuwa mbali na pale tulipokuwa tukiogelea. Baada ya muda walikuja na tukauona mwili wa pili ukiibuka,” anasimulia Gooluck kwa uchungu.
Wakisimulia tulio hilo, watoto waliokuwa katika msafara huo Florian Masonda (12) anasema walichukuliwa na jirani yao, Anita Mboka kwenda kusherehekea nao siku ya kuzaliwa kwa mtoto wake, Derick Mboka aliyekuwa anatimiza umri wa mwaka mmoja.
Florian anasema baada ya kufika hotelini hapo walianza kucheza mpira wa kikapu huku watoto wengine wakiogelea na mama Mboka aliyewapeleka pamoja na wale vijana wakiwa wamekaa wakipata vinywaji.
“Tulikuwa tunacheza mpira wa kikapu na ghafla tulisikia kelele baada ya mtoto mmoja kuja kutuita na kutupatia taarifa kuwa kuna watoto wamezama chini ya maji na hawaonekani. Tuliondoka na baada ya kufika kwenye bwawa la kuogelea ndipo tulipowaona wakiwa tayari wamekunywa maji mengi,” anasema Florian.
Naye Goodluck anasema yeye na watoto wenzake zaidi ya 20 waliondoka Kijitonyama wakiwa na vijana wanne kwenda kwenye sherehe hiyo.
“Tuliondoka hapa saa kumi na moja jioni, baada ya kufika kule tulianza kuogelea kwenye bwawa. Watoto wengine walikuwa wanakwenda kuogelea kwenye maji marefu, walizuiliwa mara tatu, lakini baada ya walinzi kuondoka walirudi na kuzama,” anasema.
Kwa uchungu alionao Bahati Sisala alikuwa amekaa akiwa ameduwaa macho yake yamevimba na mekundu kutokana na machozi yaliyomtoka kwa muda mrefu.
Akiwa amejiinamia bado haamini mkasa uliomkuta binti yake kipenzi Ndimbumi Sisala (9) uliosababisha kifo chake ambacho kilimkuta ghafla katika hoteli hiyo Aprili 27.
Lugano Mwakyosi, ambaye ni msemaji wa familia hiyo inayoishi Kijitonyama Mpakani A, anasema Sisala amechanganyikiwa kutokana na kifo cha binti yake aliyempenda sana.
Mungu azilaze roho za marehemu pepon amina
ReplyDeleteR.I.P kwa wote mliwapenda lakn mungu aliwapenda zaidi poleni wafiwa
ReplyDeleteSo sad
ReplyDeletepole
ReplyDeleteMungu azilaze roho za marehema Pema, Amen.
ReplyDelete