KOCHA wa zamani wa Yanga, Hans Pluijm ametamka kwamba Tanzania kwa sasa ina straika mmoja tu mwenye uwezo wa kucheza Jangwani naye ni MuivoryCoast wa Azam FC, Kipre Tchetche. Lakini kumpata ni kasheshe.
Pluijm ambaye amerejea Dar es Salaam kumaliza mambo yake ameiambia Mwanaspoti kwamba hajapendekeza timu hiyo kusajili straika kutoka ndani ya Tanzania lakini kama angefikiria kufanya hivyo angemnyooshea kidole Kipre.
Kauli hiyo ya Pluijm aliyeachana na Yanga, imekuja siku chache baada ya straika wa Yanga, Didier Kavumbagu kujiunga na Azam. Katika ripoti yake aliyoipendekeza kwa uongozi wa klabu hiyo, kocha huyo ameweka bayana kuwa wachezaji 11 wanatakiwa kutemwa.
Lengo lake kubwa lilikuwa kumsajili straika wa Azam, Tchetche kutokana na ubora wake, hata hivyo imeshindikana kutokana na mkataba wa mchezaji huyo na timu yake ya Azam.
Kwa mujibu wa chanzo cha uhakika ndani ya kamati ya usajili, Pluijm haoni wakuwazidi akina Emmanuel Okwi, Hamis Kiiza, Mrisho Ngassa,Saidi Bahanuzi, Jerry Tegete, Hussein Javu ambaye jana ametemwa katika kikosi cha Taifa Stars kitakachocheza na Zimbabwe Jumapili jijini Dar es Salaam.
“Sitaki kumzungumzia Domayo, sitaki kusikia habari zake, naamini kiungo atakayekuja kucheza Yanga atamfunika huyo ambaye amepata umaarufu akiwa Jangwani, wapo wachezaji wazuri wengi ambao wanaifaa Yanga na ninaamini watafurahia matunda yao,” alisema Pluijm.
“Sina mpango wa kushawishi kusajiliwa kwa straika sasa licha ya Kavumbagu kuondoka, unajua nimetazama kote Tanzania na sijamuona straika wa kuichezea Yanga kwani wote viwango vyao ni vya hali ya kulinganisha na wale waliopo katika kikosi changu,” alisema Pluijm.
“Yule Kipre Tchetche ndiye pekee anayefaa kucheza Yanga baada ya Kavumbagu kuondoka, lakini hatoweza kusajiliwa kutokana na aina ya mkataba alionao na Azam,”alisisitiza kocha huyo.
Pluijm alisema ameshafanya mazungumzo na kiungo mmoja hatari wa Ghana ambaye anakaba na kuanzisha mashambulizi zaidi ya Domayo hivyo haoni haja ya kumtaja kiungo huyo wa zamani wa Yanga.
Awali Pluijm alikuwa na mpango wa kuiletea Yanga kiungo na straika mmoja wa maana, lakini inaonekana kwanza ameanza na kiungo kwani bado uamuzi wa kumuacha mchezaji yupi wa kigeni unatatiza.
Yanga ina wachezaji wa kigeni wanne ambao ni Haruna Niyonzima, Okwi, Kiiza na Mbuyu Twite inayotarajia kumuongezea mkataba muda wowote.