Ziara za Kinana zazua Ufisadi Mkubwa CCM

WIMBI la matumizi mabaya ya fedha za umma limezidi kukiandama Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambapo hivi sasa kinatuhumiwa kutumia fedha za umma katika ziara na ukaguzi wa miradi.

Tanzania Daima imedokezwa kuwa kila ziara ya CCM inakofanyika, mkurugenzi wa halmashauri husika hutoa magari au fedha za kuwakirimu wahusika.

Imedokezwa kuwa miongoni mwa ziara ambazo zinatumia fedha za halmashauri ni inayofanywa hivi sasa mikoani na Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana.


Inaelezwa kuwa ziara hizo hazipaswi kugharimiwa na fedha za serikali kupitia halmashauri mbalimbali kwakuwa zinatokana na wananchi wenye itikadi tofauti pamoja na wasio na itikadi.

Michango hiyo ndiyo inadaiwa kuwapa nguvu vigogo wa CCM na kuacha kupitisha bakuli kuomba misaada kwa makada wake kama ilivyozoeleka siku za nyuma.

Tanzania Daima limedokezwa kuwa vyama vya upinzani na CCM vimekuwa na utaratibu wa kuomba misaada kwa makada wao au wahisani, wafadhili wa ndani na nje ya nchi.

Hata hivyo, katika siku za hivi karibuni utaratibu huo unaonekana kutumiwa zaidi na wapinzani kutokana na kutokuwa na uwezo wa kuwaamrisha au kuwashawishi wakurugenzi wa halmashauri kugharimia ziara zao.

Tanzania Daima liliwasiliana na Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, ambaye alisema kuwa taarifa hizo zinalenga kukichafulia jina chama tawala.

“Madai hayo ni ya kiupuuzi na kwamba misafara yetu inawaumiza viongozi wa CHADEMA, sisi tunapoamua jambo tunakuwa na mipango sambamba na kujitosheleza,” alisema.

Hata hivyo, Tanzania Daima limepata taarifa kuwa baadhi ya halmashauri ambazo Kinana na timu yake wameshapita ziligharamia malazi, chakula na usafiri wa ndani ikiwemo magari ya serikali kutumika.

Halmashauri ambazo taarifa zake zimekusanywa na gazeti hili ni pamoja na Nzega, Igunga na Uyui zilizopo mkoani Tabora na Iramba iliyopo mkoani Singida huku wakurugenzi wake wakikiri kutumia magari ya serikali na baadhi ya watumishi kuhudhuria katika ziara hiyo.

Katika Wilaya ya Igunga, msafara wa Kinana ulikaa kwa muda wa siku tatu ambapo halmashauri kupitia viongozi wa CCM wa wilaya hiyo waligharimia usafiri wa ndani, chakula na malazi pamoja na kukodisha pikipiki 50.

Pikipiki hizo zilitumika kumpokea Kinana na magari 10 yaliyotumika kuwabeba wananchi kutoka maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo waliotakiwa kuhudhuria mkutano wa hadhara uliofanyika mjini Igunga.

Mbali na gharama hizo, pia ziara hiyo inaelezwa kusimamisha kazi mbalimbali za kiutendaji katika maeneo wanayopita kutokana na watendaji wa serikali kutakiwa kuwa sehemu ya ziara hiyo.

Chanzo kutoka ndani ya Halmashauri ya Igunga, kilieleza kuwa mbali na gharama ya malazi, vyakula, usafiri na malazi, pia hakukuwa na malipo iliyolipwa na chama hicho kwa kutumia ukumbi wa halmashauri kufanya mikutano yake ya ndani.

Chanzo hicho kilieleza kuwa msafara wa Kinana ulikuwa na magari zaidi ya 28 na kila gari likiwekewa lita 80 za mafuta kutembelea maeneo mbalimbali.

Kigogo mmoja wa CCM, alidokeza kuwa walitakiwa kuandaa chakula cha watu 200 huku sahani moja ya chakula ikiuzwa kwa shilingi 5,500.

Alisema walikodisha pikipiki 42 kwa sharti la kila mwenye pikipiki aliyehudhuria mapokezi ya Kinana, atalipwa sh 7,000 na kuwekewa lita mbili ya mafuta.

Alibainisha pia walitakiwa wahakikishe msafara wa Katibu Mkuu unapatiwa malazi.

“Sisi chama tulibeba jukumu lile kwa kuwa ni ugeni wa chama, lakini hakuna hata senti moja tuliyotumia kutoka mfuko wa chama zaidi ya fedha hizo kutoka ndani ya halmashauri yetu,” alieleza mtoa habari wetu kutoka Igunga.

Katika Wilaya ya Nzega, Uyui na Iramba, msafara wa Kinana ulipatiwa mafuta ya magari na chakula kwa fedha zilizotoka katika halmashauri na kukabidhiwa viongozi wa CCM wa wilaya, huku suala la malazi likiachwa kuwa jukumu la waliokuwa katika msafara.

Wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti, wakurugenzi wa wilaya zilizofanyiwa uchunguzi walikanusha kugharamia ziara hizo, lakini wakikiri kutoa magari yaliyozunguka katika miradi iliyokuwa ikikaguliwa na Kinana.

Mkurugenzi wa Wilaya ya Igunga, Rusika Turuka, alipoulizwa juu ya halmashauri yake kugharamia ziara ya Kinana, alitaka apewe muda kwa maelezo kuwa yupo katika mkutano na hata alipopigiwa tena simu hakupokea.

Mkurugenzi wa Wilaya ya Nzega, Abraham Mndeme, alikiri ofisi yake kutoa magari yaliyowabeba watumishi wa serikali na madiwani wa CCM kuongozana na Kinana katika ziara hiyo wilayani mwake.

Mndeme, alisema ugeni uliofika katika wilaya yake ni wa kitaifa, na kwamba miradi iliyohitaji kukaguliwa ni ile iliyosimamiwa na halmashauri ya wilaya.

“Walioambatana na msafara wa Kinana ni madiwani na sisi tulitoa magari ya kuwasafirisha kwenda kwenye miradi na kwa watendaji mimi nilitumia gari moja na mhandisi wa manispaa,” alisema Mndeme.

Mkurugenzi wa Wilaya ya Uyui, Hadija Mkauani, alipoulizwa juu ya kugharamia ziara ya Kinana, alimuomba mwandishi akutane nae ofisini na alipoambiwa simu inapigwa kutoka Dar es Salaam alikata simu.

“Baba naomba tuonane ofisini tuweze kuongea vizuri hayo mambo au umtume mwakilishi wako hapa mkoani si mnaye huku, tutaongea vizuri tu,” alisema Mkauani.

Kaimu Mkurugenzi wa Iramba, Mariam Mpita, alisema gharama za ziara hiyo zilibebwa na CCM huku yeye, watendaji wa halmashauri hiyo waliambatana na Kinana kukagua miradi ya maendeleo.

Nape afafanua

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, badala ya kujibu hoja ya ziara zao kutumia fedha za umma aliilaumu CHADEMA.

Alisema ziara zao zinawaumiza CHADEMA waliokuwa wakifanya ziara za aina hiyo ili kujiimarisha, lakini sasa wanaona zinafanywa na CCM wanahofia kuanguka mwaka 2015.

“Hata mtoto wa darasa la kwanza akisikia hayo madai atajua ni upuuzi, lakini ulizeni halmashauri iliyochangia hata shilingi moja. Najua ziara hizi zinawaumiza sana CHADEMA,” alisema.

Alipoulizwa kama ziara yao ina lengo la kuwaumiza CHADEMA au kuangalia changamoto zinazowakabili wananchi, na CCM itakavyoishauri serikali kutatua yatakayobainika, Nape alisema swali aliloulizwa ni fikra za kijinga za CHADEMA.

Nape alisema CHADEMA hawana ujanja wa kukwepa kifo chao, huku akisema uzushi na uongo hautawasaidia kupona.

Wakati Nape akikana halmashauri hizo kugharamia ziara za chama hicho, wiki iliyopita katika kikao cha Baraza la Madiwani wa Jiji la Arusha, Mkurugenzi wa jiji hilo, Juma Idd, alikiri kufanya hivyo.
Idd, alitoa kauli hiyo alipokuwa akijibu maswali ya madiwani wa jiji hilo waliohoji sababu za ziara za madiwani au viongozi wa CCM kutumia magari ya halmashauri.

Idd, alisema walitoa magari hayo ikiwa ni utekelezaji wa maelekezo ya serikali iliyotaka viongozi wa CCM kupita kukagua utekelezaji wa ilani yao.

Alisema kuwa jiji walitoa wataalamu na gari kwa ajili ya kwenda kutoa ufafanuzi juu ya miradi hiyo.

Source:Tanzania Daima.
Tags

Post a Comment

4 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
  1. Bongo uwajibikaji ni zero. Mijitu ya ccm bado wanaona pesa za serikali ni kama petty cash ya chama chao. Imagine shule zinakosa chaki lakini halmashauri zinagarimia ziara za chama cha siasa!!!

    ReplyDelete
  2. Bongo uwajibikaji ni zero. Mijitu ya ccm bado wanaona pesa za serikali ni kama petty cash ya chama chao. Imagine shule zinakosa chaki lakini halmashauri zinagarimia ziara za chama cha siasa!!!

    ReplyDelete
  3. uyo kinana mwenyewe fisadi, kauza sana pembe za ndovu na ngozi za wanyama nje ya nchi, tena akae kimya tucje funguka mengi hapa

    ReplyDelete
  4. Tetesi za kinena wa ccm kugombea urais zinazidi kujionyesha wazi,kaanza kampeni mapema mno huku akiwazuia kina Lowassa na membe wasijipitishe kwa wananchi.

    ReplyDelete

Top Post Ad

Below Post Ad