Barabara Mradi Mabasi Mwendo Kasi ni Janga, Usalama Wake ni wa Hatari kubwa Mabilioni Yameliwa na Wajanja?

Wakati wakazi wa jiji la Dar es Salaam wakiwa na matumaini makubwa ya kuondokana na msongamano wa magari kutokana na ujenzi wa barabara ya mabasi yaendayo haraka (BRT), uchunguzi wa NIPASHE umebaini kwamba mradi huo utaleta maafa makubwa.

NIPASHE imethibitisha kwamba barabara mpya inayojengwa sambamba na ya mabasi yaendayo haraka, imepunguzwa upana wake kutoka mita sita hadi tano, hivyo kufanya madereva kuwa na wakati mgumu wakati wa kupitana (overtake).

Upana wa mita tano kila upande ni kuanzia kwenye ukingo wa barabara ambako umejengwa ukuta (capstone).

Kuna kila dalili kuwa mradi huu ambao umekuwa gumzo kwa kila kiongozi anayetoa majibu ya kuondoa msongamano jijini Dar es Salaam, umegubikwa na ufisadi.

Ufisadi huu unatokana na ukweli kwamba wakati Mtaalamu Mwandamizi wa masuala ya usafirishaji wa Benki ya Dunia (WB), Mhandisi Yonas Mchomvu, anasema kwa mujibu wa makubaliano yaliyofikiwa katika BRT, barabara hiyo ingehamishiwa pembeni mwa ile ya mradi, ikiwa na upana sawa na ule wa awali, hali ni kinyume chake.

“Labda kama ni kwa mtazamo wa macho na baada ya kuweka zile kingo, upana wa barabara ile ukaonekana ni mdogo, lakini ilipaswa ‘kusogezwa’ kwa vipimo vya awali,” anasema alipozungumzia mradi huo hivi karibuni.

Hata hivyo, NIPASHE ilipima barabara hiyo eneo la Kimara-Korogwe na kubaini kwamba upana wake ni mita tano upande mmoja na mita upande wa pili.

Upande huo ni tofauti kabisa na ule ulikuwako awali wa mita sita kila upande, huku kukiwa na upana wa mita 1.5 kila upande kwa ajili ya waendesha baiskeli na watumiaji wengine.

Upanda huu mdogo wa sasa mbali ya kuwa kikwazo cha kutatua foleni na msongamano, pia unaibua suala muhumu wa thamani ya fedha katika mradi huo unaotokana na mkopo kutoka Benki ya Dunia ulitazamiwa kutumia dola za Marekani milioni 290 (Sh. bilioni 493 (kwa viwango vya Dola moja kwa Sh. 1,700).

NIPASHE imethibisha kwamba katika barabara kuu nne za Dar es Salaam, Mandela, Sam Nujoma na Ali Hassan Mwinyi zote zina upana wa mita sita na kuendelea, huku ya Morogoro inayojengwa upya ikiwa na upana wa mita tano.

Mandela ina upana wa mita sita kila upande, Sam Nujoma mita 6.5 kila upande na Ali Hassan Mwinyi mita sita kila upande.

Hofu ya udanganyifu katika barabara ya Morogoro inazidi kuwa na nguvu kwani vipimo vilivyochukuliwa na NIPASHE eneo la Kimara –Gereji ambako haijajengwa upya umeonyesha kuwa ina upana wa mita sita na pembeni mita 1.5 kila upande, hivyo kuonyesha dhahiri kuwa eneo la kuanzia mradi BRT Kimara –Mwisho hadi makutano na Bibi Titi Mohammed, barabara hiyo imeminywa sana.

Kulingana na upana huo mpya ambao ni dhahiri unaibua suala la usalama kwenye barabara hii, kiasi cha mita mbili zilizopunguzwa, kinaibua suala jingine ya kiasi kikubwa cha fedha ambacho hakijulikani kimekwenda wapi.

Kipande cha barabara ya Morogoro kutoka Kimara- Mwisho hadi makutano na Bibi Titi Mohamed, kinakadiriwa kuwa na urefu kilomita 15. Upana wa mita mbili unaopungua katika barabara hiyo ni sawa na urefu wa barabara yenye kilomita tano ikiwa na upana wa mita sita.

Kwa mujibu wa takwimu kutoka Wizara ya Ujenzi gharama za ujenzi wa kilomita moja ya barabara kuu ya lami inakadiriwa kufikia Sh. bilioni 1. Kwa maana hiyo, ni dhahiri kwamba kiasi ‘kilichookolewa’ kwa eneo lililopunguzwa kinafikia Sh. bilioni 5.

Hakuna taarifa zinazoeleza bayana sababu za kupunguzwa kwa upana huo wala mahali fedha ‘zilizookolewa’ zilipopelekwa.

Mbali na suala la uwezekano wa ufisadi katika mradi huu, mfumo wa ujenzi wake ambao umeongeza kona nyingi, nao umezidisha mazingira hatarishi yanayoweza kusababisha ajali za mara kwa mara kama ilivyowahi kutokea kwa nyakati tofauti hivi karibuni.

Siyo Wizara ya Ujenzi wala Wakala wa Usimamizi wa Barabara Dar es Salaam (Tanroad), walitoa maelezo juu ya sababu za kuminywa kwa barabara hiyo kwa kiwango hicho.

Barabara ya Morogo ni mfano mmoja tu juu ya mambo yanavyokwenda ovyo katika sekta nzima ya ujenzi wa barabara nchini.

NIPASHE imefanya uchunguzi na kubaini kuwa, ujenzi wa barabara ni miongoni mwa miradi ya maendeleo ambayo ufujaji wa fedha za umma unafanyika kwa namna tofauti, sehemu kubwa ikielekezwa katika huduma za kitaalamu.

Hujuma zinazofanywa katika miradi ya barabara, zimekuwa chanzo kikuu cha ujenzi duni unaochangia kuharibika kwa miundombinu hiyo muda mfupi baada ya kukamilika kwake.

Kwa kawaida, barabara zinazojengwa kwa viwango tofauti vya lami, zinatarajiwa kutumika kwa kati ya miaka 10 hadi 16 kabla ya kufanyiwa matengenzo makubwa.

Lakini barabara hizo zimebainika kuharibika chini ya muda huo baada ya kukamilika kwake.

UPUNGUZAJI WA VIPIMO VYA BARABARA
Moja ya mbinu zinazotumiwa na wadau wanaoshiriki ujenzi na kuikagua miradi ya barabara, ni kupunguza vipimo vya upana kwa kiasi kidogo kisichoweza kugundulika kwa urahisi hususani na wananchi wa kawaida.

Vyanzo tofauti vilivyofanikisha kufichuka kwa siri hiyo vinaeleza kuwa, mbinu hiyo inatekelezwa ili kuokoa kiwango cha fedha kwa mkandarasi, ambazo hata hivyo hazirejeshwi hazina, bali kuwafikia watu binafsi.

Hata hivyo, taarifa zinazohusu ufisadi huo zinapatikana huku vyanzo vyake, vikisisitiza usiri wa kutojulikana, kwa sababu za usalama binafsi na ulinzi wa ajira zao.

HALI ILIVYO SINGIDA
Mmoja wa wahandisi katika Manispaa ya Singida, ambaye hataki jina lake litajwe gazetini, anasema kwa miaka mingi, miradi ya ujenzi wa barabara imekuwa ikihujumiwa kwa namna tofauti.

Mhandisi huyo, anatoa mfano wa ufisadi unaofanywa kupitia upunguzwaji wa vipimo vya barabara, umekithiri kwenye miradi nyingi na kwamba inasababisha upotevu wa fedha na kudidimiza ubora wa miundombinu hiyo.

Chanzo hicho kinaeleza kuwa, kwa kawaida barabara nyingi kama zinazounganisha mikoa, zimekuwa zikijengwa kwa upana unaofikia mita nane.

Lakini, barabara hizo zimekuwa zikipunguzwa kwa kipimo (mathalani) cha kuanzia mita 0.5 hadi moja na ambazo si rahisi kubainika pale ujenzi wa mradi unapokamilika.

“Unapojenga barabara na kupunguza mita 0.5 kutoka upana wa mita nane, si rahisi ikagundulika kwa watumiaji wa barabara isipokuwa mpaka kwa wanaohusika na upimaji,” kinaeleza chanzo hicho.

Chanzo hicho kinaeleza kuwa, kiasi kama hicho kinapopunguzwa, kinaokoa fedha kwa kadri ya urefu wa barabara, ingawa kwa ujumla wake, fedha zinazopotea ni nyingi.

“Hapa unaweza kuziona mita 0.5 ni ndogo, lakini kwa hakika zinapojumuishwa kwa urefu wa barabara yote, unakuta ukubwa wake unahusisha kiasi kikubwa cha fedha kinachoishia mifuko mwa wajanja wachache,” kinaeleza.

MIRADI YA WAFADHILI
Ingawa ni hivyo, imebainika kuwa miradi mingi ya barabara inayojengwa kwa kutumia fedha za ndani, ama mikopo pasipo kuwapo usimamizi madhubuti, imetekelezwa kwa kiwango cha chini ikilinganishwa na thamani ya fedha.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano wa Zanzibar, Juma Malik Akil, anasema ushahidi wa kimazingira unaonyesha kutokuwapo usimamizi mzuri wa miradi hiyo, hivyo kusababisha kiwango duni cha barabara zinazojengwa.

“Hizi barabara zinazojengwa na kufuatiliwa kwa karibu na wafadhili, kwa kiasi fulani zinakuwa na ubora unaotakiwa, lakini zinazosimamiwa na mamlaka za ndani ya nchi, hapo kuna matatizo sana,” anasema alipokutana na ujumbe wa WM mjini Unguja hivi karibuni.

Miongoni mwa barabara zilizojengwa kwa ufadhili wa WB visiwani Zanzibar na zinazotajwa kuwa miongoni mwa zenye ubora ni zile za Paje-Pingwe, Matembwe-Pongwe na Mkwajuni-Nungwi.

SHINIKIZO LA MADIWANI/WABUNGE
Uchunguzi huo unabaini kuwa shinikizo za kisiasa zimekuwa miongoni mwa vyanzo vinavyochochea ujenzi duni wa barabara hususani zinazounganisha maeneo ya ndani ya mikoa.

Shinikizo za kisiasa, zinatajwa kupitia vikao vya mabaraza ya madiwani, ambapo wawakilishi wa wananchi wakiwamo wabunge ni wajumbe wake.

Mhandisi wa jiji la Arusha, Afwilile Lamsy, anasema katika utumishi wake kwenye fani hiyo kwa zaidi ya miaka 10, ameshuhudia kuwapo madiwani na wabunge wanaoshinikiza ujenzi wa barabara kuyafikia maeneo wanayoamini kuwapo wapiga kura wengi.

Mhandisi Lamsy, anasema shinikizo hizo zinafanywa wakati ambapo bajeti za halmashauri husika zinaposomwa na fedha kutengwa kwa ajili ya ujenzi wa barabara hasa kwa kiwango cha lami.

Inapotokea hali hiyo, baadhi wa wabunge na wenye nguvu ya kufanya maamuzi, wamekuwa wakihitaji mgawanyo wa fedha kidogo zinazotengwa, kuelekezwa kwenye ujenzi ama ukarabati wa barabara nyingi na zenye urefu mkubwa, pasipo kuwianisha na fedha zilizopo.

“Wapo wataalamu waadilifu wanaobuni mikakati mizuri ya ujenzi wa barabara, lakini inapowasilishwa na kujadiliwa kwenye baraza la madiwani, wawakilishi hao wa wananchi wanaipinga,” anasema.

Kwa mujibu wa Mhandisi Lamsy, hali hiyo ipo katika maeneo mengi ya halshauri za wilaya, manispaa na majini nchini.

Anatoa mfano kuwa, inaweza kutokea wahandisi wakapendekeza kujengwa barabara tatu kati ya 10 zilizopo kwenye halmashauri husika, kila moja kwa kilomita moja ya kiwango cha lami.

“Lakini ikifikishwa baraza la madiwani, wanapinga na kutaka fedha zilizotengwa zitumike kujenga barabara nyingi ikibidi zote kwa kupitisha greda na kumwaga vifusi,” anasema.

Barabara ni miongoni mwa miundombinu inayoligharimu taifa fedha nyingi na ambayo kama usimamizi wake ungefanikisha kuwapo kwa ubora, ni dhahiri kwamba zingechochea kasi ya maendeleo na kurahisisha mawasiliano.
CHANZO: NIPASHE

My Take:

Kifungu 27 (1) za Sheria ya barabara namba 13 ya 2007, Tangazo la Serikali No 21 ya tar 23 Januari 2009 kinataja upana wa chini kabisa kwa njia za barabara za lami (Roadway Lane) kwa Barabara Kuu zote hapa nchini (Trunk roads) kuwa usipungue mita 3.25.

Hivyo kama njia 2 (mbili) za Barabara ya Morogoro zimejengwa kwa Mita 5 tu badala ya mita 6.5 (yaani Mita 2.50 kwa kila njia badala ya Mita 3.25) Sheria ya barabara Na 13 ya 2007 na Kanuni zake za 2009 vitakuwa vimevunjwa hivyo Serikali isikubali kupokea barabara hiyo kabisa kwani hata kabla haijaisha tayari watanzania wameshaanza kupoteza maisha.

Na tunamtaka Mhe John Magufuli ahakikishe mkandarasi anaifanyaia barabara hiyo marekebisho mara moja.
Tags

Post a Comment

2 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad