Barua kwa Rais: Mheshimiwa Jakaya Kikwete Umetisha Sana kwa Hili

Mheshimiwa Rais Jakaya Kikwete – natamani ningeonana na wewe ana kwa ana ili nikupe shikamoo yako nzito kwakuwa shikamoo ya kuandika siku zote huwa naiona ni yenye mapungufu. Heshima yako mkuu. Mimi kijana wako naliendeleza gurudumu la ujenzi wa taifa katika upande huu wa burudani kama kawaida. Upande ambao mheshimiwa umekuwa ukiuangalia kwa jicho la kipekee na lenye nia njema ya kuuletea neema. Upande ambao kwa viongozi wengi waliopita, ulikuwa ukichukuliwa kama wa anasa na wa kupoteza muda tu hivyo kushindwa kuupa heshima na ‘attention’ inayostahili.

Tangu uchukue madaraka, Mheshimiwa ulionesha nia njema na ya dhati ya kuwasaidia vijana walioamua kujiajiri kwa kutumia vipaji vyap walivyopewa na mwenyezi Mungu asiye mchoyo wa fadhila. Wengi walikuwa wamekwama kuendelea na masomo kutokana na sababu mbalimbali lakini kutokana na kuwa na kipawa cha kuimba ama kuigiza waliamua kutumia sauti zao kuwaburudisha watu kwa kutunga nyimbo.

Burudani ambayo kwa wengine wenye umri kama wako na waliopata nafasi kubwa serikalini wamekuwa wakiichukulia poa na kuiona kama aina moja miongoni mwa aina ya nyingi za uhuni zinazowatawala vijana wengi, imegeuka kuwa ajira muhimu kwa vijana wengi ambao maisha yao yamekuwa mfano kwa vijana wengine pia.

Mheshima Rais, tangu mwanzo, umekuwa karibu mno na vijana wanaofanya muziki wa Bongo Flava na kwao wewe ni kipenzi chao. Katika nchi hii ambayo kutokana na shida zetu, tumejikuta tukiona mabaya zaidi na kuwa watu wa kulalamika na yale mazuri tukijifanya hatuyaoni, hiki unachokifanya kwa vijana wetu kinaweza kionekane kwao cha kawaida tu. Mimi nakichukulia kwa mkazo mkubwa.

Nina imani kubwa, tasnia za burudani za majirani zetu zinatamani pia zingekuwa na Rais kama wewe, ambaye anaufahamu umuhimu wa msanii na kwa moyo mmoja amekuwa akiwajali. Naamini mheshimiwa Rais una imani kama niliyonayo mimi kuwa, wasanii wamekuwa wakitimiza wajibu muhimu katika jamii kwa kutuburudisha tuwapo na mawazo, furaha, huzuni na hali mbalimbali, kutuliwaza pale ya mambo ya dunia yanapotuelemea na kutusemea pale tunaposhindwa kuwasilisha nia zetu. Haipendezi kumuona mtu anayeitumikia jamii kwa hali hii, kuishi maisha ya tabu na ya kudharauliwa.

Na ndio maana umekuwa bega kwa bega kujaribu kuwapa ‘mashavu’ vijana wako ili maisha yao yawe mazuri. Ni ngumu kutimiza matakwa yao yote lakini ile hali tu ya kuwaweka karibu, kuwapa connection, imekufanya uonekane kuwa wewe ni rais wa pekee na ambaye umekuwa na mchango mkubwa kwenye kiwanda cha burudani.

Mheshimiwa Rais, nimeandika barua hii kwa lengo kuu la kukupongeza kwa hotuba yako inayotia moyo uliyoitoa Jumamosi iliyopita mjini Dodoma katika tamasha la uzalendo. Ile ni miongoni mwa hotuba zilizonifurahisha mno mheshimiwa. Ilinionesha jinsi ambavyo unafuatilia kwa ukaribu industry ya muziki duniani. Nilifurahi kukusikia mwenyewe jinsi ambavyo kutumia connection zako mwenyewe, umemtambulisha Diamond Platnumz kwa mdau mkubwa na muhimu katika muziki wa Marekani, Kevin Liles.

Kiukweli mimi Kevin nilimfahamu kupitia makala ya Trey Songz iliyorushwa miaka kadhaa kupitia MTV ambapo yeye alikuwa akiongea kama meneja wake. Nilivutiwa na jinsi alivyo na mchango mkubwa kwa Trey na hivyo nikaamua kumsoma zaidi kwenye mitandao. Niligundua kuwa alikuwa kuwa Rais wa Def Jam Recordings (pamoja na vyeo vingine) ambayo ni miongoni mwa label kubwa na zenye mafanikio nchini Marekani. Naamini kuwa maongezi yako na Kevin kuhusu Diamond yatazalisha kitu kikubwa hapo baadaye. Nilipenda pia uliposema kuwa unajivunia kwa hatua aliyofikia.

Ulitisha zaidi mheshimiwa pale ulipodai kuwa ulizungumza pia na meneja wa Ludacris, Chaka Zulu. Na zaidi pale ulipodai kuwa Usher na mtangazaji wa zamani wa kipindi cha 106 & Park cha BET, Terrence J ambaye kwa sasa ni mtangazaji wa E!News, watakuja Tanzania na kwamba ikiwezekana Trey Songz naye ataibuka.

Hawa watu ni muhimu mno katika burudani duniani hivyo wakija Tanzania kuongea na wasanii kuhusu masuala mbalimbali, watapandikiza masuala mengi ya muhimu kwao. Wasanii wa nyumbani watajifunza mengi kutoka kwao.

Mheshimiwa nimependa ulivyojiongeza hapa kwamba ni vyema ukamfundisha mtu kuvua samaki kuliko kumpa samaki ambao akiwala atapata njaa tena na ataendelea kuhitaji. Ungeweza kusema uwape fedha baadhi ya wasanii lakini fedha hizo zisingewasaidia kwa lolote. Kuwaleta akina Usher nchini kwetu itakuwa ni zawadi kubwa na muhimu kwa wasanii sababu watajifunza mbinu nyingi za kuboresha biashara ya muziki nchini ambayo kama ikitambuliwa kama ajira rasmi na serikali, itawanufaisha wengi.

Naamini kuna wengi watabeza, wataponda na wataongea kuchafua hatua hii lakini jambo unalopaswa kukumbuka kuwa hata Yesu Kristu licha ya kuja duniani kuwaokoa wanadamu dhidi ya dhambi, walimkejeli na kumsulubu bila huruma. Ungekuwa Rais usiyejali kama marais wengine madikteta duniani basi ungetumia uwezo wako kuwaleta wasanii hao waje wakuburudishe kwenye sherehe zako binafsi. Lakini unawaleta hawa kwa madhumuni na nia halisi ya kuwasaidia wasanii wa nyumbani. Hilo si la kupuuzwa.

Na pia wale ambao wataponda hatua hii, ndio walewale ambao bado wanauchukulia muziki kama anasa, uhuni, starehe na masuala ya kupoteza muda wakati kwa nchi zilizoendelea, muziki na filamu vinachangia pato kubwa katika serikali.

Nausubiria sana ujio wa watu hawa muhimu na bila shaka wasaidizi wako watakuwa werevu wa kutosha kutualika pia sisi waandishi kujifunza yanayotuhusu katika ziara hiyo. Wasiwasi wangu ni kuwa Rais atakayechukua nafasi yako atafuata nyayo zako? Anyway, nisikuchoshe kwa maneno mengi mheshimiwa, nakutakia majukumu mema.

Wako katika ujenzi wa taifa, Sky.
Tags

Post a Comment

19 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
  1. duuu raisi wa wasanii du ngoja na mm nitoe single maana bila ivyo sintopata msaada na kikwete

    ReplyDelete
  2. Hotuba imeandaliwa na clouds hiyo....na kuthibitishwa na ikulu kikwete hana muda mchafu na wasanii

    ReplyDelete
  3. Sasa nyie mnawazungumzia wanamuziki wa Hip Hop R & B. Mbona hamuwazungumzii wanamuziki kutoka nyanja nyingine zenye mafanikio. Wapo wanamuziki wa Rock and Roll, Pop music, Country music, Jazz music. Je ni kweli miongoni mwa wanamuziki woote toka nyanja hizo nyingine ni kweli sisi wanamuziki wa Tanzania tutamuhitaji Usher pekeee????? Sikatai kuhusiana na ujio wa Usher katika kuleta changamoto za hizo Hip Hop music lakini kama tungewaleta Wanamuziki nguli Duniani kama Kenny Rodgers, Lionel Ritchie, na pia watu kama Madonna na Patte Labelle nadhani hiyo ingesaidia zaidi kwani licha ya unguli wao katika fani hiyo pia ni watu ambao wamekaa muda mrefu kwenye hiyo fani ya muziki na pia sio siri licha ya mafanikio yao lakini pia uzoefu wao katika hiyo fani ya muziki ni wa hali ya juu sana. Nadhani pia tungempata mtu kama Michael Jackson kama angekuwa hai hilo nalo lingekuwa jambo bora. Watu kama Usher ni kweli wanaweza leta hizo changamoto lakini sio kama hao niliowataja hapo juu. Hekima na busara pia ni vitu vya kuzingatiwa katika kuamua ni mwanamuziki gani wa kumleta. Sasa mtu kama huyo Usher dah. Ana scandalous Dunia mzima mpaka muziki umemshindwa. Sio mtu anayeng'aa tena katika hizo anga za muziki achilia mbali Hip Hop R & B.

    ReplyDelete
  4. Na pia wasiwasi wangu isijekuwa Watanzania tunaanza kuingia kwenye hiyo Hip Hop music na kuachana na asili yetu ya hapa nyumbani na Africa kwa ujumla. Kuna nchi nyingi za Africa ambazo zimeizidi kwa mbali Tanzania katika nyanja hiyo ya muziki. Nchi kama South Africa, Ivory Coast,DRC na nyinginezo. Kwa nini tusiwatumie hao manguli wa Bara letu hili la Africa kuja kuwaboresha vijana wetu. Kwa mfano Alpha Blondy, Yvonne ChakaChaka na wengineo. Je ni kweli kwa wakati huu tunamuhitaji huyo Terrence J anchor wa E news????? Wa kazi gani?? Kwa jambo lipi ama historia gani aliyokuwa nayo katika fani ya muziki????? Hao managers wa Ludacris ni kitu gani hasa endelevu watakachotuletea sisi Watanzania kama sio kuja hapa na kutuibia hata kile kidogo tulichokuwa nacho kwa faida yao???? Jamani Watanzania tuache ulimbukeni, twendeni na wakati. Hawa wenzetu wana take advantage of the situation kwa ajili ya ulimbukeni wetu. Tusimame wima kama Nchi nyingine za Africa ambazo zimeukataa huo ukoloni mamboleo.

    ReplyDelete
  5. Ama sasa Watanzania ndio tumegeuka na Wamarekaaaniii kuliko hata Wamarekani wenyewe???? Wapi, huko ni kujidanganya. Vipi kuhusu Nchi kama Liberia na Sierra Leone ambao wao hasa wana hiyo historia ya Umarekani. Wa ndio wasemeje???????

    ReplyDelete
  6. Sasa akiangalia kukuza vipawa vya wanamuziki je na watanzania wengine wanao hitaji maendeleo mikoani watafanyaje? Maana gharama ya kumleta Usher Tanzania inaweza kujenga barbara angalau kilometer 5 au hata kusomesha watoto yatima angalau 10 tu kwa muhula mmoja mm ningependa tujenge Kwanza hapa kwetu pakiwa pazuri watakuja wenyewe tu.

    ReplyDelete
  7. iyo barua ameandika kinana

    ReplyDelete
  8. ki ukweli hata msemeje kikwete ni rais wa pekee na hana wa kufanana nae, kaitambulisha tanzania duniani nchi ambayo nchi nyingine ilikuwa haikulikani, kwa sasa hatutaona umuhimu wake, ni pale atakapondoka madarakani. lkn ukweli utabaki pale pale kikwete katutoa matongotongo na katufikisha mbali sana sijui huyo atakaeshika kijiti kama nae atakuwa na mbio kama za kikwete au la

    ReplyDelete
    Replies
    1. Katutoa au kakutoaa?kakufikisha mbaali kwa lipi?EPA,mikataba mibovu,wizi wa pembe za ndovu,mabilioni ya IPTL,kutokuwalipa mishahara walimu,huduma mbovu za afya,wizi wa mali za uma,safari za nje ya nchi mara kwa mara,madawa ya kulevya au nini kingine?ni kweli amekufikisha mbali na kukutoa matongo tongo manina zako.

      Delete
  9. hakuna jipya full range of politics hapo.Wanalalamika kunyonywa kila siku na clouds na genge la wezi kama kina Fella na Babu tale.Ukweli hata angekuja p diddy au Rick ross matatizo yao hayataisha.wameshindwa kuboresha miundombinu itayowafanya wauze kazi zao wanalukia la kuwafundisha,

    ReplyDelete
  10. Kama ni kutambulika kimataifa Tanzania ilikwisha tambulika kwa kupitia vyanzo mbalimbali kama kuwa na Mbuga nzuri za wanyama, Mlima Kilimanjaro, na hata michezo ya kimataifa na hasa riadha. Vuta kumbukumbu zako vizuri ujikumbushe enzi za Filbert Bay na Suleiman Nyambui. Pia kumbuka ushiriki wa Tanzania katika michezo ya jumuia za madola pamoja na Olympic ambapo ilikuwa inakusanya medali mbalimbali. Pia kumbuka bao la Peter Tino lililoiwezesha Taifa Stars kwa mara ya kwanza na pengine mara ya mwisho kushiriki michuano ya soka mataifa ya Africa. Kwa hiyo usijidanganye kama ni kujulikana kama Taifa Tanzania iliisha julikana kitambo.

    ReplyDelete
  11. Actually Mwl. Julius.K.Nyerere ndiye aliyeiweka Tanzania katika Map ya kimataifa zaidi kuliko kiongozi yeyote aliyewahi kutokea katika Nchi hiyo. Kwa hiyo vuta kumbukumbu zako vizuri.

    ReplyDelete
  12. UJINGA MTUPU,JAMAA ANATAFUTA UJIKO KWA WASANII MAMBO MANGAPI NCHI HII YANALALA.ANGEJISHUGULISHA NA UKUSANYAJI WA KODI TUNGEMSIFU,ANAJIPELEKA KWENYE MAKUNDI YA WATU WASIO NA UELEWA NDIO MAANA WANAMSIFIA UPUUZI.MTU YEYOTE MUELEWA HAWEZI SIFIA UJINGA HUU.

    ReplyDelete
  13. mkuu apo juu umeneba kwa mtu makini awezi msifia rais km uyu maana atufundishi kitu kabisa kuna wasomi kibao awana ajira anaangaik music why sijui hana mshauli aijawai tokea rais mwenye akil mbovu km uyu kwanza hana ofu ya mungu mtu anaye mjua Mungu awezi shabikia music

    ReplyDelete
  14. Hiyo ya kuwaleta hao wanamuziki ni danganya toto ya kusingizia kuleta changamoto. Kiukweli ni kwamba wanakuja hapo ku congratulate mtoto wake Ridhiwani kwa kupata Ubunge. That's the bottom line of it. Kwa yale yaliyotokea juzi uwanja wa Taifa kuhusiana na usaili wa uhamiaji ndio changamoto kwa Taifa na vijana. Tunataka ajira. Hatumtaki Usher wala Treyz Song kwa sababu hawatatusaidia kitu zaidi ya kuliingizia Taifa hasara......ni mambo ya aibu.

    ReplyDelete
    Replies
    1. Akili za Watanzania zipo katika maajabu kumi ya dunia!hivi nyinyi woote mnaosherekea na kucoment kuhusu usher reymond trey song sijui!hivi mmeshatembelea muhimbili hospitali kuu ya rufaa ya taifa la watanzania haina kifaa cha utra sound na serikali inajua ni kifaa muhimu sana kwa hospital?hospitali binafsi kama Regency,agakhan,Tmj wanacho.na muhimbili kilikuwepo kipimo ni elfu 50 lakin ukienda private hospital ghalama ni laki 4 na elfu 50!sasa watanzania hizo ni changamoto chache tu nilizotaja ila ziko changamoto mlima ambazo ufumbuzi wake ni kitendawili!sasa jiulizeni kipi cha muhimu Usher raymond au hicho kifaa maana ghalama zina fanana.watanzania jaribuni kuzinduka nchi inazama hii acheni kulewa na vitu vidogo.hapo hamna tofauti na wale wa tshirt na pilau kabisa.

      Delete
  15. Kwa kweli watanzania tunasilitisha sana, wananchi wanaulimbukeni lakini pia viongozi wetu wana ulimbukeni na ushamba wa ajabu, hivi kweli katika changamoto tulizonazo watanzania rais anapata muda, nia, gharama na sababu ya kuwaleta wanamuziki hao Wamarekani, wale wote ambao wanasherehekea na kufurahia hili wanafanya hivyo kwa ushabiki wao tu kwa Rais, au Chama au kwa sababu kwa namna moja au nyingine ujaji wa wanamuziki hao una tija kwao. Kiukweli raisi wetu amekuwa akijihusisha na mambo mengine ambayo hayana tija kwa wananchi kwa ujumla wao, badala ya kuwaleta kina usher raymond kwa mfano angejitahidi kuhakikisha zinatungwa sheria kali dhidi ya walanguzi wa kazi za wasanii, hili lingewanufaisha wasanii moja kwa moja lakini pia lisingekuwa na gharama yoyote ya moja kwa moja. Binafsi ninasikitishwa sana na baadhi ya maamuzi ya Rais wetu, kuna watu wengi wenye shida sana kwenye hii nchi ambao wanahitaji msaada wa serikali japo hata wa panadol kwenye zahanati zao lakini hawapewi kipaumbele.

    ReplyDelete
  16. hakuna nchi dunian inayoendelea kwa polical na economical pekee lazima ijiendeleze kisocially,ni watu wangapi wamepata ajira kwa ajili ya wanamuziki ukiachilia wao wenyewe kujiajili acheni ulimbuken wa kusema matatizo kibao hayajatatiliwa,hata akiwa nani rais things will b da same, shame on u msiopenda maendeleo ya wasanii wa bongo

    ReplyDelete
  17. mdau umeongea point sana yan tupende dans kuliko maendeleo ya nchi

    ReplyDelete

Top Post Ad

Below Post Ad