VITA ni vita! Siku mbili zimekatika tangu sakata la picha ya pozi inayodaiwa kuwa ni ya mheshimiwa Komba na msichana aliyetajwa kwa jina moja la Angel kutoka kwenye baadhi ya vyombo vya habari Bongo, lingine limeibuka!
Hili la safari hii ni zito pia. Lenyewe linamhusu mheshimiwa mmoja ambaye anadaiwa ni mbunge wa Chadema. Na yeye anasemekana kwamba alipiga picha katika pozi tata na ‘totoz’ ambaye jina lake halikupatikana.
Baadhi ya watazamaji wa picha hizo ambazo zimesambaa kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii, walisema kwa vile mheshimiwa Komba ni wa CCM na mwenzake ni wa Chadema ni kama ngoma droo!
KWA NINI NGOMA DROO?
Maoni ya watu yanasomeka kwamba, vyama hivyo viwili ndivyo vyenye ushindani mkubwa katika jamii hivyo viongozi wao kuning’inizwa kwenye mitandao kwa madai hayo hakuna atakayesema mwenzake anahusika na hujuma hiyo huku wale wa Cuf, NCCR-Mageuzi na vyama vikingine vikionekana kuachwa nyuma kwenye ‘fasheni’ hiyo mpya.
“Ingekuwa mwingine ni wa CCM pia, si ajabu CCM wangesema Chadema wanahusika, sasa ni CCM kwa Chadema. Hapo mnasemaje? Hamuoni kwamba ngoma droo?” Alihoji mmoja wa wachangiaji hao kwenye mjadala huo wa wanasiasa kuzidi kuchafuana kwa kasi.
MITANDAO YA KUCHAFUA
Habari zilizochimbwa na Ijumaa Wikienda zilidai kuwa, katika kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2015 kumeibuka kundi linalojiita Umoja wa Kambi Huru ‘Ukahu’ ambao kazi yao kubwa ni kuwachafua wanasiasa kwa habari za kweli au za kuwatungia.
“Kuna watu wanasema kuna Ukahu, yaani Umoja wa Kambi Huru wakiwa na maana hawapo CCM wala Chadema. Wao kazi yao ni kuwachafua wanasiasa tu kwa ajili ya kuelekea uchaguzi mkuu mwakani,” kilisema chanzo.
Kikaendelea: “Lakini nasikia hawa watu wanatumiwa na viongozi wa wapinzani wa wanasiasa. Mfano, Komba kama ana mwanasiasa anataka ang’oke kwenye jimbo lake mwakani, basi anawindwa kuanzia sasa ili achafuke na watu wasimame wakisema yeye si msafi.
“Unaambiwa hao jamaa wa Ukahu, hata kama ulifanya madudu mwaka 2005, wao wanayapata tu, kama huna wanakutengenezea madudu ya kufanana na wewe.”
WABUNGE WAJIPANGE, PICHA ZAIDI ZIPO
Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa bado kundi hilo lina picha ambazo baadhi ya wabunge walipiga au walitengenezewa wakiwa na vimwana ambazo zimepangwa kutolewa moja baada ya nyingine kadiri siku zinavyokwenda kuelekea uchaguzi mkuu.
WABUNGE WENGI KUANGUKA
Taarifa zanasema kundi hilo limejipanga kuhakikisha kwamba kwenye mizengwe hiyo, katika kila wabunge 10, 4 hawatarudi kwenye majimbo yao mwakani bila kujali vyama.
WABUNGE VIJANA WAKAE CHONJO
Ikazidi kudaiwa kuwa wabunge vijana, hasa wenye umri wa kuanzia miaka 25 hadi 50 ndiyo wapo kwenye tageti hiyo. Mheshimiwa Komba ana miaka 60, mwenzake 44.
KISA NINI HASA?
Ijumaa Wikienda liliendelea kuchunguza zaidi na kubaini kwamba, kisa cha mambo yote hayo ni kukomoana hasa kwa wale wanasiasa ambao wanatamani kuwa wabunge kwenye majimbo ambayo wanaamini kuwatoa wahusika waliopo sasa madarakani si rahisi.
“Mimi jamani najua siasa, wapo wanasiasa wanatamani sana majimbo ya wenzao, sasa kwa vile wanajua kuwatoa si rahisi, wanapendwa sana ndiyo maana wanatumia njia ya kuwachafua ili wapiga kura wasiwapende na wao washike nafasi,” alisema mbunge kutoka jimbo moja la Mkoa wa Dar.
Akaendelea: “Siamini kama wabunge wetu wako hovyo kiasi hicho, kwamba wanaweza kuwa wapo ndani ya vyumba vya gesti na wanawake halafu wakaamua kupiga picha chafu, wana akili zao.”
GPL