Daktari aliyewapokea watoto pacha waliokuwa wameungana katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na kuwapeleka India kufanyiwa upasuaji, Zaituni Bokhary anatarajia kuwasili nchini leo akitokea masomoni Misri na kwenda Mbeya kuwajulia hali watoto hao.
Pacha hao, Elikana na Eliud walizaliwa Februari 20 mwaka jana katika Hospitali ya Wilaya ya Uyole kabla ya kuhamishiwa Hospitali ya Rufaa ya Mbeya na baadaye Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kutokana na kuzaliwa wakiwa wameungana kiunoni.
Akizungumza kwa uchungu baada ya kusikia taarifa ya kuzorota kwa afya ya mtoto Eliud, daktari Bokhary ambaye yupo masomoni nchini Misri alisema: “Usinilize jamani naona uchungu, naomba tushauriane nini cha kufanya...yaani hadi tumbo linaniuma.
“Roho inaniuma sana kusikia utumbo wa Eliud uko nje, ingekuwa siyo shule ningekaa nao hadi wapone kabisa,” alisema Bokhary, ambaye alisisitiza kwenda Mbeya kuwaona watoto hao.
Afya ya Eliud yazorota
Hali ya mtoto Eliud inazidi kuwa mbaya kutokana na sehemu kubwa ya utumbo wake mpana unaotumika kutolea haja kubwa kutoka nje hali inayomfanya kudhoofu kiafya.
Baba mzazi wa watoto hao, mkazi wa Kasumulu Kyela, Eric Mwakyusa alisema jana kuwa hali ya mtoto wake inazidi kumchanganya kutokana na kuzidi kubadilika kila wakati.
Hivi karibuni alisema baada ya hali ya mtoto huyo kubadilika alimpeleka Hospitali ya Wilaya ya Kyela ambako daktari aliyemwona alishauri mtoto huyo asubiri hadi atakapokwenda India, Agosti mwaka huu. Hata hivyo, Mganga Mkuu wa Hospitali hiyo, Festo Dugange aliliambia gazeti hili kuwa hajawahi kusikia wala kumwona mtoto aliyetoka utumbo hospitalini hapo.
Wakati huohuo, baba wa watoto hao, Mwakyusa amepewa msaada wa pikipiki na msamaria mwema ili kukidhi maisha yake.
Mwakyusa amewashukuru wasamaria mbalimbali wanaomsaidia kwa njia tofauti ikiwemo wasamaria waliompatia pikipiki ili afanye kazi ya kubeba abiria na mapato yake yatumike kuboresha maisha ya familia yake.
‘’Nawashukuru waandishi wa Mwananchi kwa kuandika hali halisi ya watoto wangu, kwani jana nimepewa pikipiki na msamaria mwema wa jijini Dar es Salaam ambaye alipata taarifa za watoto wangu kupitia magazeti yenu’’, alisema.
Alisema kwa kipindi kirefu alikuwa akiendesha pikipiki ya mtu ambaye alikuwa akipewa Sh8,000 kila siku na yeye kubaki na kati ya Sh1,000 au 2,000 kwa siku ambazo ndizo zilikuwa zikitumika kuwahudumia watoto na familia nzima.
ee Mungu mponye mtoto
ReplyDeleteMungu atamponya mtoto huyo
ReplyDelete