IVO Mapunda wa Simba, amesema kuanzishwa kwa timu ya umoja wa makipa Tanzania, umemaliza tofauti za walinda mlango wote na sasa yeye pamoja na Juma Kaseja na Ally Mustapha ‘Barthez’ ni kitu kimoja.
Awali kulikuwa na minong’ono kuwa makipa hao hawana maelewano mazuri kutokana na sababu mbalimbali za ndani na nje ya Uwanja.
Lakini sasa walinda mlango hao, wanakula, wanakunywa na kufanya mazoezi kwa pamoja kila siku nyakati za asubuhi na jioni kwenye Uwanja wa Gadren, Kinondoni.
Ivo alisema: “Tunapokuwa kwenye timu yetu hii, watu huwa wanasubiri waone kitatokea nini baina yetu, lakini wanashangaa kuona tupo kwa pamoja na amani. Tunashirikiana kwa kila jambo kama kupongezana kwa mambo mbalimbali kama unavyojua tunakuwa timu moja, tunapata mialiko kwenda sehemu mbalimbali, tunakula na kunywa pamoja,”alisema Ivo na kuwataka wadau wajititokeze kuidhamini timu yao kwani wanajiongoza na kujitegemea wenyewe kwa kila kitu kwa sababu ya kukosa mfadhili.
“Hata ile imani ya kwamba sisi hatuelewani huwa ni mashabiki wenyewe tu lakini siyo sisi. Tunafanya mazoezi mara mbili ambapo asubuhi huwa tunafanya yetu ya ukipa na jioni, tunafanya ya kucheza uwanjani kama unavyojua hii ni timu ya wachezaji 11 wanaocheza ndani kama zilivyo nyingine za soka.”
Baadhi ya makipa ambao wapo na kikosi hicho ni pamoja na Shaaban Hassan ‘Kado’, Kaseja, Barthez, Ivo, Jackson Chove na wengineo.