Wafanyikazi wa usafiri wa mjini Sao Paulo wamepiga kura kuidhinisha mgomo wao uendelee kwa muda usiojulikana licha ya uamuzi wa mahakama ya nchini Brazil, kuamuru wafanyikazi hao kurudi kazini mara moja.
Amri ya mahakama ya kazi nchini Brazil imewataka wakuu wa vyama vya wafanyikazi wa usafiri wa mjini Metro, kufuata taratibu za kudai haki zao nasi kutumia mamlaka yao vibaya kwa kuanzisha mgomo ambao umedumu tangu juma lililopita.
Wakiandamana katika mitaa mbali mbali ya mjini Sao Paulo wafanyakazi wa idara ya usafiri walibeba mabango yaliyoonyesha malalamiko yao, kwa kudai nyongeza ya mishahara, huku nusu ya vituo vya usafiri vikiwa tayari vimefungwa na msongamano wa magari umezidi kuongezeka mjini humo.
Wafanyikazi hao wanadai nyongeza ya mshahara ya asilimia 12 ilhali serkali imesema itamudu nyongeza ya takrban asilimia 9.
Hali ya sintofahamu imeendelea kutanda miongoni mwa viongozi wa serikali ya nchini Brazil pamoja na wajumbe wa kamati ya maandali ya fainali za kombe la dunia, kwa kuhofia huenda hali ikawa mbaya zaidi juma hili ambapo siku ya Al-khamis mji huo utakuwa mwenyeji wa shamra shamra za ufunguzi wa fainali za kombe la dunia.