Hatimae Michael Wambura Apigana Mpaka Kimeeleweka Simba

KAMATI ya Rufani ya Uchaguzi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), imemrejesha kuwania Urais wa Klabu ya Simba, Michael Wambura ambaye alikuwa ameenguliwa.

Habari zilizopatikana jana usiku wakati tukienda mitamboni, zilieleza kuwa Wambura amerejeshwa na Kamati hiyo inayoongozwa na Mwanasheria Julius Lugaziya, baada ya kikao cha vuta nikuvute.

Kikao cha Kamati hiyo chini ya uenyekiti wa Lugaziya, kilimalizika Dar es Salaam jana usiku, ambapo baadhi ya waandishi wa habari walitaka kufahamu hukumu ya rufani hiyo ya Wambura, na Ofisa Habari na Mawasiliano wa TFF, Boniface Wambura alisema majibu yatatoka leo.

“Taarifa mtapewa kesho (leo), leo siwezi kuongea lolote,” alisema Wambura mara baada ya kurejea kwenye ofisi za TFF, katikati ya Jiji akitokea kwenye kikao hicho cha rufani.

Alirejea ofisini kabla ya kumalizika kwa kikao hicho. Juzi, Kamati hiyo ilikutana hadi saa tano usiku kwenye Hoteli ya Protea Oysterbay, na jana waliendelea na kikao hicho kwenye ofisi za TFF kuanzia asubuhi hadi saa sita mchana na baadaye kuhamia Hoteli ya Southern Sun ambako walikamilisha kazi yao iliyokuwa inasubiriwa na mashabiki wa soka nchini.

Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana, inadaiwa kuwa kikao hicho kilikuwa na mvutano miongoni mwa wajumbe hasa katika kufikia maamuzi yao.

Hadi jioni, tayari wajumbe walikuwa wamekamilisha kazi yao, lakini maamuzi ‘yakawa magumu’ kufikiwa.

Kamati ya Uchaguzi ya Simba chini ya Mwenyekiti Damas Ndumbaro ilimuengua Wambura kuwania nafasi hiyo kwenye Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Juni 29, kwa madai si mwanachama halali wa klabu hiyo, kitendo ambacho mhusika hakukubaliana nacho na ndipo kukata rufaa ili kupata haki yake.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad