Maisha ya baadhi ya watu wanaotumia dawa za kufubaza makali ya ugonjwa wa Ukimwi (ARVs), yapo hatarini, baada ya kupungua kwa dawa hizo nchini na hivyo kufanya wagonjwa kutumia dawa tofauti na zile wanazotumia siku zote.
Uchunguzi wa gazeti hili umegundua kuwa hali hiyo inatokana na urasimu wa baadhi ya taasisi za Serikali, ambazo zinachelewa kuagiza dawa za ARVs kwenye viwanda vya nje ya nchi.
Tayari Mfuko wa Kimataifa unaoshughulikia Ugonjwa wa Ukimwi, Kifua Kikuu na Malaria wa Global Fund, Shirika lisilo la Serikali linalojihusisha na masuala ya afya (Sikika) na watumiaji wa ARV nchini wamethibitisha kuwapo kwa upungufu huo na hatari zake kiafya kwa wagonjwa.
Global Fund katika ripoti yake ya robo ya mwaka huu (Januari- Machi), imekiri kuwapo kwa upungufu wa dawa za ARV nchini na athari ambazo wameanza kupata wagonjwa.
Ripoti hiyo inaonyesha upungufu huo wa dawa za ARV unatokana na uzembe wa baadhi ya taasisi za Serikali kuchelewa kuagiza dawa hizo pamoja na kuwapo kwa mabadiliko katika ununuaji na ucheleweshwaji wa kupatikana fedha za kununulia ambao umesababisha upungufu huo.
Taarifa hiyo inaeleza kuwa waathirika wakuu katika upungufu huo wa dawa ni wanawake wajawazito wanaoishi na virusi vya Ukimwi, ambao wanatakiwa kutumia ARV aina ya TLE ili kuzuia maambukizi ya mama kwenda kwa mtoto.
Upungufu huo, umesababisha wagonjwa kubadilishiwa dawa tofauti na zile wanazotumia hali ambayo imesababisha baadhi yao kinga ya mwili (CD4) kushuka.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili katika baadhi ya mikoa nchini unaonyesha tatizo hilo la kupungua kwa ARVs nchini, limewaumiza wagonjwa wengi na kwamba sasa wanapokwenda hospitali wanapewa dawa za kutumia wiki mbili au vidonge 10 badala ya dawa za mwezi mmoja au miwili.
Sikika
Shirika lisilo la Kiserikali (Sikika), linalojihusisha na masula ya afya, wamebaini kuwapo kwa upungufu wa dawa za ARV katika mikoa ya Kigoma, Kilimanjaro, Tabora, Shinyanga, Morogoro, na Dar es Salaam.
Mkurugenzi wa Sikika, Irenei Kiria alimwambia mwandishi wa gazeti hili kuwa taarifa walizozipata kutoka kwa watu wanaotumia ARV, upungufu mkubwa wa dawa hizo kwa Mkoa wa Dar es Salaam upo katika katika Hospitali za Mnazi Mmoja, Mwananyamala, Amana na Temeke.
Katika hospitali hizo wagonjwa wanabadilishiwa dawa za ARV na kupewa tofauti na zile ambazo wamezoea kuzitumia.
“Taarifa tulizopata Machi mwaka huu, ni kwamba tatizo hilo bado lipo na wagonjwa wanaendelea kupewa dawa pungufu, mfano badala ya kupewa za mwezi mara nyingine walikuwa wanapewa za wiki au kubadilishiwa dawa bila kupewa maelezo ya mabadiliko hayo,” anasema Kiria.
Kiria aliiomba Wizara ya Afya itoe tamko rasmi kuwaeleza wananchi hali halisi ya dawa za ARV, ili kuepusha hali ya wasiwasi na madhara ya kisaikolojia wanayoyapata wagonjwa hivi sasa.
“Ni haki ya kila mwananchi kupata taarifa sahihi ambazo zinahusu afya yake, ili naye aweze kutimiza wajibu wake wa kuilinda afya yake na za wenzake,” anasema Kiria.
Kiria anaishauri Serikali kutenga bajeti kwa ajili ya shughuli za dharura pale ambapo itatokea, huku akiitaka kupunguza utegemezi.
Anasema taarifa ya matumizi ya Serikali ya ugonjwa wa Ukimwi mwaka 2011 na Mkakati wa Tatu wa Kitaifa wa Kudhibiti Ukimwi (NMSF III) wa mwaka 2013/14 – 2017/18 unaonyesha kuwa bajeti hiyo imekuwa ikipungua na kwamba utegemezi wa wafadhili ni zaidi ya asilimia 97.
Naibu Waziri
Naibu Waziri wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Kebwe Steven, anasema kuwa licha ya kutegemea ufadhili, lakini Serikali ina fedha kwa ajili ya kununua dawa ndani na nje ya nchi kama itatokea kutakuwa na dharura.
Anasema kuwa hafahamu kuhusu kuwapo kwa upungufu, anachofahamu ni kuchelewa kufika kwa dawa kutokana na taratibu za uagizaji, kwani Global Fund ambayo ndiyo inayoagiza dawa hizo husambaza kwa nchi nyingi.
Anasema kuwa anadhani hilo ndilo tatizo lililosababisha kupungua kwa dawa hizo nchini.
Naibu waziri huyo anasema pamoja na Global Fund kutoa dawa hizo nchini, lakini Serikali wamekuwa wakichangia kiasi katika kuziingiza dawa hizo.
“Siyo kwamba hatuchangii kabisa, kuna vitu ambavyo tunafanya ikiwamo gharama za kutoa dawa hizo bandarini, hatuwezi kumwachia jirani atujengee nyumba,” anasema Kebwe.