Kinachoendelea Simba Kinakatisha Tamaa

KAMA zilivyo klabu nyingine, klabu ya Simba nayo ina nafasi yake ya kipekee katika suala zima la maendeleo ya soka la Tanzania.
Simba kama zilivyo klabu nyingine nayo inatakiwa kuwa imara ili kutoa ushindani ambao utakuwa na maana kubwa katika kuifanya Ligi Kuu Bara iwe na msisimko na hivyo kuwa na mchango wake katika kuiinua soka la Tanzania.
Hata hivyo kwa mambo yanayoendelea Simba kwa sasa tuna hofu kama Simba itakuwa moja ya timu tishio kwenye Ligi Kuu Bara msimu wa 2014-15.
Kinachoendelea Simba kwa sasa hakitoi dalili zozote za Simba  itakayokuwa tayari kutoa ushindani kwenye Ligi Kuu na hata kujiwekea mazingira ya kucheza michuano ya kimataifa kwa kushika nafasi ya kwanza au ya pili katika ligi hiyo.
Wakati tunaandika makala haya bado hakuna uhakika wa wachezaji gani watakaoichezea Simba msimu ujao, kocha atakuwa nani na benchi la ufundi kwa ujumla litakuwaje.
Unaweza kuona hali ya aina hiyo katika klabu nyingine lakini ukweli ni kwamba kuna tofauti kubwa kwa kuwa klabu hizo kwani tayari zimeanza usajili, zimekamilisha au zinafanya mazungumzo na wachezaji, makocha na benchi la ufundi kwa ujumla.
Kwa Simba ni tofauti na yote hayo hayafanyiki kwa sababu moja tu. Uchaguzi! Inashangaza kuona kwamba uchaguzi ambalo ni tukio la siku moja linakuwa sababu ya kukwamisha mambo mengi ya Simba.
Hali hii hasa ndiyo inayotusikitisha na kutushangaza kibaya zaidi kama ambavyo tulisema katika maoni yetu toleo lililopita kwamba huu uchaguzi unaosubiriwa, kwa hali ilivyo sasa ni kama haujulikani lini utafanyika.
Wakati uchaguzi haujulikani, ligi inajulikana itaanza Agosti 24 mwaka huu, wakati uchaguzi haujulikani ukomo wa kusajili wachezaji wa Ligi Kuu Bara unajulikana.
Sambamba na yote hayo muda wa kocha kuandaa timu nalo ni jambo muhimu ambalo haliwezi kusubiri muda.
Hata hivyo wakati tukishangazwa na kusikitishwa na kinachoendelea Simba bado tuna wajibu wa kujiuliza anayeitwa Mkurugenzi wa Ufundi Simba, Moses Basena kwa sasa anafanya kazi gani?

Hapo ndipo unapobaini kwamba Simba imejiwekea mfumo mzuri lakini haitaki kuusimamia mfumo huo kwani tulidhani huu ungekuwa wakati wa Basena kufanya kazi ya benchi la ufundi hadi kocha mpya atakapopatikana.
Tulidhani huu ungekuwa wakati wa sekretarieti ya Simba kukaa na Basena na kuangalia mambo yajayo ikiwamo usajili, maandalizi ya ligi na kocha ajaye ambaye atakabidhiwa jukumu la kuinoa Simba.
Pia tulidhani huu ungekuwa wakati wa Simba kuandaa programu ya muda mfupi ili ianze kufanyiwa kazi na hatimaye iwe na matunda hata uongozi mpya utakapoingia madarakani.
Lakini yote hayo hayaangaliwi na kibaya zaidi ni kwamba hata viongozi waliopo madarakani hawataki kufanya lolote kwa ajili ya Simba ya baadaye kwa sababu ya uchaguzi.
Ukweli ni kwamba pamoja na umuhimu wa uchaguzi bado jambo hilo halitoshi kuwa sababu ya kusimamisha kila kitu ndani ya Simba.
Na kama kweli uchaguzi ni tatizo basi ni kwa nini kusiwe na programu ya muda mfupi ambayo itatumika kukamilisha baadhi ya mambo likiwamo hili la usajili ambalo katika Simba ni kama lipo njia panda.

Post a Comment

3 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
  1. Wewe nawe huchoki?hawakutaki

    ReplyDelete
  2. Hayo hayakusemwa na Wambura, wabaya wake tuliyeni, wachache walaji hamumtaki, wengi tunamtaka, fair play imeshindikana mahakama itamua,na Wambura atapeta na Simba itakuwa bingwa bila friends of simba.

    ReplyDelete
  3. Huyo Wambura ni yule aliyesoma pale Morogoro. Kigurunyembe Secondary School. Alikuwa mbishi kama nini na mpenda madaraka ya ukilanja. Na sio kweli kuwa anaweza kuwa kiongozi mzuri.......ni mbabaishaji. Waulizeni watu waliosoma naye pale Kigurunyembe Secondary School. Ni mtu wa hovyooooooo..........

    ReplyDelete

Top Post Ad

Below Post Ad