KUTOKA BRAZIL: Kumbe Timu ya Taifa Brazil kuna Usimba na Uyanga

UNASHANGAA mashabiki wa Simba wakiwa wako kimya pindi mpira unapokuwa miguuni mwa Kevin Yondani wa Yanga katika mechi ya Taifa Stars? Unashangaa mashabiki wa Yanga nao wakiwa kimya pindi mpira unapokuwa kwa Amri Kiemba wa Simba katika mechi ya Stars? Basi wala usishangae sana.

Hata Brazil ipo vivyo hivyo. Jana Alhamisi kulikuwa na pambano kati ya Brazil na Croatia. Hali hiyo ilitazamiwa kuwepo pindi mambo yanapokuwa magumu kwa upande wa Brazil. Nilikuwa nimekaa kijiwe kimoja cha jioni chenye mashabiki wa nchi mbalimbali na nikapata simulizi.

China Keya, kiungo wa zamani wa Pan Afrika ambaye anaishi hapa amenisimulia mambo yanavyokwenda ovyo pindi maisha ya timu ya taifa ya Brazil yanapokuwa magumu uwanjani, hasa timu yao inapocheza katika Jiji la Sao Paulo.

“Timu ya taifa ya Brazil inakuwa katika wakati mgumu pindi inapocheza soka hapa Sao Paulo. Mashabiki wa soka wa Sao Paulo hawana uvumilivu hata kidogo. Mechi ikifika dakika ya 20 bila ya bao, wanaanza kuwazomea taratibu wachezaji wao,” anasema China. “Lakini pia mashabiki wa hapa wakati mwingine wanawashangilia wachezaji kutokana na timu wanazochezea. Kwa mfano, kama kipa akikaa Julio Cesar na timu haifanyi vizuri basi wanaanza kulitaja jina la kipa Rogerio Ceni. Kila Cesar akigusa mpira wanalitaja jina la Ceni.”

“Ceni ni kipa wa Sao Paulo, timu inapocheza katika Jiji la Sao Paulo ndiyo wanamkumbusha kocha kwamba Ceni ndiye anayepaswa kukaa langoni na si kipa mwingine yeyote. Maisha ya Brazil jijini Sao Paulo ni magumu.

“Wakati mwingine mpira akiugusa Neymar wanazomea na kulitaja jina la Lucas Moura (wa PSG). Ni kwa sababu Lucas amezaliwa eneo hili hili la Sao Paulo. Neymar amezaliwa Sao Paulo lakini yeye anatoka kitongoji cha Santos ambacho kipo kando kidogo.

“Fred naye aliwahi kufunga bao katika mechi ya kirafiki na kwenda upande wa mashabiki wa timu pinzani ndani ya Brazil huku akiwaonyesha ishara ya sikio kuwasikiliza kama wanaweza kunyamaza na kelele zao za kumzomea.” Anamaliza China.

Hapa simulizi zinazidi kunoga zaidi. Majuzi Neymar alilazimika kuongea na vyombo vya habari vya Brazil kuwasihi raia wa Brazil kuacha kushangilia wachezaji kutokana na timu wanazochezea.

Kuelekea katika mechi yao ya jana dhidi ya Croatia, ungeweza kuona ni kwa kiasi gani Wabrazili wanaipenda timu yao. Mazungumzo yote yalikuwa ni namna ya kuifunga Croatia.

Biashara kubwa zaidi kwa sasa ni jezi namba 10 ya Neymar, rangi za kuchora bendera ya Brazil usoni, tarumbeta zao ambazo hazina kelele sana kama Vuvuzela.

Unadhani Waingereza wanaipenda na kuipamba sana timu yao? Hapana. Hawawazidi Wabrazili. Tatizo kubwa la Tanzania na ukanda wa Afrika Mashariki ni kupokea taarifa nyingi kutoka katika vyombo vya Uingereza. Lakini Wabrazil ni kiboko!

Timu inapokwenda kula chakula cha mchana kituo maarufu cha Televisheni cha hapa, Global Sports kinaweka tukio hilo laivu. Timu ikiwa inatoka katika korido ya hoteli kupanda katika basi kwa ajili ya kwenda mazoezini tukio hilo linawekwa laivu katika televisheni.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad