DUNIA nzima inampenda Mario Balotelli. Kuna kila supastaa wa soka hapa nchini Brazil kwa sasa, lakini ukiondoa Neymar na wachezaji wenzake wa timu ya taifa ya Brazil, hakuna anayefikia nyota ya Mario Balotelli.
Ndani ya ardhi ya Brazil kwa sasa kuna Cristiano Ronaldo, Lionel Messi, Robin van Persie, Arjen Robben, Diego Costa na wengineo, lakini ukizunguka katika mitaa ya Sao Paulo, Wabrazili wanavutika zaidi kumwangalia Balotelli. Wenyewe wanamwita ‘Maruku’ wakimaanisha kichaa.
Popote ambapo kikosi cha Italia kinapoonyeshwa katika televisheni watu wote waliopo katika baa mbalimbali za Sao Paolo wanakaa kimya na kusikiliza kinachozungumzwa kuhusu Balotelli ambaye ndiye anazungumziwa kwa muda mrefu na watangazaji.
“Tungependa kuwa na mchezaji kama yeye kikosini kwetu Brazil. Anachangamsha timu. Unamkumbuka Edmundo? Alikuwa kama yeye. Katika timu lazima uwe na mchezaji kichaa,” anasema dada mmoja mhudumu wa baa ya Carcio de Italiano, Suzanne Almeda.
Mtu mmoja anajitokeza kumsifu Balotelli lakini hapo hapo anatengeneza laana kwa Wataliano wasichukue ubingwa wa Kombe la Dunia kwa sababu wakichukua wataifikia Brazil kwa idadi ya mataji hayo.
Ikumbukwe kuwa katika fainali, Italia wamechukua mara nne wakiifukuza Brazil ambayo imechukua mara tano. Wajerumani nao wanaombewa dua mbaya na Wabrazili wa hapa kwa sababu wamechukua mara tatu.
Cristiano Ronaldo anapendwa kwa sababu kubwa moja. Anatoka katika nchi ambayo iliwatawala na kuwaachia lugha ya Kireno ambayo ni Ureno. Kwa sababu Ronaldo anazungumza lugha wanayoielewa huku kukiwa na Wareno wengi nchini Brazil, raia wa Brazil wanamuona kama mwenzao.
Sijachunguza kwa umakini, lakini nadhani naweza kuja na mjadala huu siku zijazo ukiendelea kusoma Mwanaspoti, nadhani Messi atakuwa anachukiwa kwa sababu anatoka katika taifa lao pinzani, Argentina.